Home Habari za michezo KUELEKEA MECHI NA WATUNISIA…NABI ‘AWASNICHI’ NDUGU ZAKE….APENYA KIMYA KIMYA MPAKA ‘CHUMBANI’..

KUELEKEA MECHI NA WATUNISIA…NABI ‘AWASNICHI’ NDUGU ZAKE….APENYA KIMYA KIMYA MPAKA ‘CHUMBANI’..

Habari za Yanga SC

Kocha wa Yanga, Nabi Mohammed ni mjanja sana. Jamaa kawapiga US Monastir chenga ya mwili pale kwenye Uwanja wao Jijini Tunis, Tunisia na kuwasoma kila kitu ndani na nje ya uwanja.

Saa chache baada ya Yanga kuichapa Namungo ya Lindi kwa mabao 2-0 kwenye mechi ya ligi, mabosi wa Yanga walimtanguliza kimyakimya nchini Tunisia Nabi kuwafanyia umafia wapinzani wao US Monastir na Msemaji wao, Ally Kamwe alithibitisha jana.

Yanga itakutana na Monastir Februari 12, jijini Tunis katika mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika kabla ya kurudi Dar es Salaam kukiwasha na TP Mazembe.

Alichofanya Nabi amesafiri kimyakimya akitangulia kuiwahi mechi moja ngumu ya ligi wakati Monastir wakiwakaribisha nyumbani Ben Guerdane na ulipigwa Jumapili Februari 5, Monastir walilala kwa bao 1-0 matokeo ambayo yamewafanya Guerdane kuongoza msimamo wa kundi lao B kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa huku wakilingana pointi 26 baada ya kila timu kucheza michezo 13.

Nabi ambaye ni raia wa Tunisia alikuwa amebana zake jukwani kama shabiki wa kawaida akiwasoma vizuri wapinzani wake hao huku akiwashtukia kumpumzisha mmoja wa mawinga wake machachari katika mchezo huo lakini wao hawakujua chochote.

Nabi pia leo ataishuhudia Monastir ikicheza ugenini dhidi ya vibonde wanaoshika mkia katika kundi lao Rajiche ikiwa ni muda mfupi baada ya kikosi cha Yanga kutua Tunis na kwenda kwenye kambi maalumu iliyoandaliwa nje ya mji ambayo walikaa huko wakapata ushindi kwenye mechi ya mwisho dhidi ya Club Africain.

Yanga itakwenda moja kwa moja mji wa Swiss ambapo ndio wataweka Kambi fupi kabla ya kurejea jijini Tunis Ijumaa jioni tayari kwa maandalizi ya mwisho ya mchezo huo.

Kocha huyo ambaye ameweka rekodi ya kuwa kocha pekee kuipa ushindi timu inayotoka Tanzania ndani ya ardhi ya nchi za Afrika Kaskazini baada ya kuifunga Club Africain kwao,anaamini kwamba Monastir itawapa wachezaji wake watakaocheza mechi dhidi yao nafasi ya kutosha kuwapima kwa utimamu wa mwili kabla ya mchezo wao.

Ratiba ya Yanga

US Monastir vs Yanga Feb 12

Yanga vs Mazembe Feb 19

Bamako vs Yanga Feb 26

Yanga vs Bamako Machi 8

Yanga vs US Monastir Machi 19

Mazembe vs Yanga Aprili 2

SOMA NA HII  KOCHA SIMBA 'AMPIGIA UPATU' MBRAZILI MWENZAKE ASAJILIWE SIMBA...NI YULE GOLIKIPA...