Home Habari za michezo KUELEKEA MECHI YA SHIRIKISHO LEO…REKODI YA YANGA CAF YASHTUA AFRIKA…KAZI IKO HAPA…

KUELEKEA MECHI YA SHIRIKISHO LEO…REKODI YA YANGA CAF YASHTUA AFRIKA…KAZI IKO HAPA…

Habari za Yanga

Mashabiki wa Yanga kwa sasa wana furaha kubwa. Ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo katika mechi ya Kundi D ya Kombe la Shirikisho Afrika umewapa mzuka mwingi.

Ni kama vile hawakutarajia kuona timu hiyo ikipata ushindi huo wa kishindo kwa vigogo hao wa Afrika kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Huenda hii ilitokana na rekodi za nyuma za mechi mbili baina ya timu hizo katika michuano ya CAF ikishindwa kufurukuta.

Mwaka 2016 timu hizo zilishakutana kwenye kundi moja la michuano hiyo ya, lakini Yanga ilipasuka mechi zote mbili, ikianza kulala 1-0 kwa Mazembe kisha kwenda kucharazwa 3-1 ugenini.

Matokeo ya wikiendi iliyopita, yameifanya Yanga ikifikishe pointi tatu za kwanza kundini, kwani ilipoteza meechi ya kwanza ugenini dhidi ya US Monastir kwa kuchapwa mabao 2-0.

Leo itakuwa Bamako, Mali, kukabiliana na Real Bamako iliyochapwa mabao 3-1 katika mechi ya kwanza na TP Mazembe ugenini kabla ya kulazimishwa sare ya 1-1 na Monastir ikiwa nyumbani.

Ushindi ilioupata dhidi ya Mazembe sio wa kwanza kwa timu hiyo katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho, kwani illishafanya hivyo mechi za mwaka 2016 na 2018, lakini ikaishia kumaliza mkiani kama ilivyokuwa pia katika Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 1998.

Mwanaspoti linakuletea rekodi za mechi za makundi ya Kombe la Shirikisho ambazo Yanga ilishiriki mara mbili ikiweka rekodi ya kuwa timu pekee ya Tanzania kufanya hivyo kabla ya Namungo na Simba kujibu mapigo hivi karibuni.

KAZI ILIANZIA HAPA

Mwaka 2016 Yanga illiandika rekodi ya kuwa timu ya kwanza ya Tanzania kutinga makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuing’oa GD Sagrada Esperance ya Angola kwa jumla ya mabao 2-1, ikishinda nyumbani 2-0 na kulala ugenini 1-0 na kujikuta ikiangukia Kundi A.

Katika kundi hilo Yanga ilipangwa na TP Mazembe ya DR Congo iliyomaliza kinara wa kundi, MO Bejaia ya Algeria iliyomaliza nafasi ya pili, huku Medeama ya Ghana ikimaliza ya tatu mbele ya Yanga iliyoshika mkia.

Tofauti na ushiriki wake na kuwa timu ya kwanza katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika 1998 ilipomaliza mkiani, bila kupata ushindi wowote kwenye Kundi A, kwenye michuano hiyo ya 2016, Yanga ilishinda mechi moja na kutoka sare moja nyumbani, huku ikipoteza michezo minne iliyosalia.

Ilianza kwa kipigo cha 1-0 ugenini kutoka kwa Mo Bejaia, kabla ya kulala 1-0 nyumbani mbele ya Mazembe na mchezo wa tatu ikiikaribisha Medeama uliisha kwa sare ya 1-1 na ilipoenda kurudiana nao Ghana ikachapwa mabao 3-1.

Waalgeria walipowafuata Kwa Mkapa, Yanga iliilipa kisasi kwa kuichapa 1-0, ukiwa ndio ushindi pekee ilioupata msimu huo kwani ilienda kumaliza mechi zake Lubumbashi, DR Congo dhidi ya Mazembe na kucharazwa mabao 3-1.

Matokeo ya jumla yaliifanya Yanga imalize kundi ikiburuza mkia kwa kukusanya pointi nne tu, ikifunga mabao manne tu na kufungwa tisa.

2018 IKARUDI YALEYALE

Baada ya kupita mwaka mmoja tangu iliposhiriki hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho 2016, Yanga ilirudi tena kwenye hatua hiyo ikiwa ni rekodi pia kwa timu za Tanzania kucheza makundi mara mbili ndani ya miaka mitatu.

Yanga ilitinga makundi ya michuano hiyo mwaka 2018 baada ya kutolewa Ligi ya Mabingwa na kuangukia kwenye play-off ikipangwa kuvaana na Welayta Dicha ya Ethiopia ambayo iliing’oa kwa jumla ya mabao 2-0, ilishinda nyumbani kwa mabao 2-0 na kulala ugenini kwa bao 1-0.

Safari hii, Yanga ikiwa Kundi D likiwa na timu za Rayon Sports ya Rwanda, Gor Mahia ya Kenya na USM Alger ya Algeria.

Yanga ilianzia ugenini kwa kipigo cha mabao 4-0 kutoka kwa USM Algers na kurudi nyumbani kulazimishwa suluhu na Rayon na kuifuata Gor Mahia iliyowakandika mabao 4-0 jijini Nairobi na kupotezea dira kabisa vijana na Mwinyi Zahera ambaye ndiye aliyekuwa akiinoa kipindi hicho akichukua nafasi ya Mzambia George Lwandamina.

Yanga iliikaribisha Gor Mahia na kuchapwa tena mabao 3-2 kabla ya kuwakaribisha Waalgeria na kuwachapa mabao 2-1, uliokuwa ushindi pekee kwa msimu huo.

Mechi ya mwisho iliifuata Rayon Sports jijini Kigali na kujikuta ikifumuliwa bao 1-0 lililoifanya imalize tena mkiani ikikusanya jumla ya pointi nne tu, ikifunga mabao manne na kufungwa 13.

ILIVYOKUWA 1998

Msimu wa kwanza tu tangu michuano ya Klabu Bingwa Afrika ibadilishwe na kuwa Ligi ya Mabingwa mwaka 1997, Yanga iliandika rekodi ya kuwa timu ya kwanza ya Tanzania kutinga makundi ya michuano hiyo mwaka 1998.

Enzi hizo ilifahamika kama Nane Bora ya Ligi ya Mabingwa na Yanga iliangukia Kundi B na ASEC Mimosas ya Ivory Coast, Raja Casabalanca. Pia Manning Rangers ya Afrika Kusini ambayo ilifungua nayo dimba jijini Dar es Salaam na kulazimishwa sare ya 1-1.

Sare hii ilionekana kuwa ya kizembe kwani Yanga iliongoza kwa muda mrefu bao la kusawazishwa ‘jioooni’.

Baada ya sare hiyo ya, Yanga ilisafiri hadi Abidjan, Ivory Coast kuifuata Asec Mimosas iliyoikaribisha kwa kipigo cha mabao 2-1, kisha kuunganisha safari hadi Casablanca nchini Morocco kuvaana na Raja na kutandikwa 6-0, huku ikiimpoteza nahodha wake, Kenneth Mkapa aliyelimwa kadi nyekundu dakika za mapema kabisa na kuidhoofisha ngome ya timu hiyo.

Yanga ikarudiana na Raja na kutoka nayo sare ya 3-3, licha ya awali kuonekana kama ilikuwa ikiondoka na ushindi nyumbani kabla ya Waarabu kubadilika dakika za lala salama.

Yanga ikaenda Sauzi na kuchapwa 4-0 kutoka kwa Manning na iliporudi nyumbani dhidi ya Asec Mimosas, ikalala tena mabao 3-0 na kumaliza mkiani ikiwa na pointi mbili tu, ikifunga mabao matano na kufungwa 19.

KAZI IPO HAPA

Kwa msimu huu, licha ya ushindi wa nyumbani wa mabao 3-1 mbele ya Mazembe, Yanga bado ina mechi nne zisizotabirika na kama haitafanyia kazi ya ziada inaweza ishindwe kutoboa kundini kwa mara ya nne mfululizo ya ushiriki wake kwenye michuano ya CAF.

Leo  hii inapepetuana na Real Bamako, moja ya timu ngeni kwenye michuano hiyo, lakini isiyotabirika kutokana na kuibana Monastir wikiendi iliyopita na kutoka nayo sare ya 1-1.

Kama Yanga itaenda kwa kuidharau inaweza ikashindwa kuendeleza furaha iliyopata dhidi ya Mazembe, kwani Real Bamako katika mechi zake mbili za awali imefunga mabao na kuruhusu pia kufungwa. Ililala 3-1 ugenini, lakini sare ya 1-1 inaonyesha ni timu inayofunga na inayoruhusu mabao, hivyo Yanga ijipange mapema kabla ya kuifuata timu hiyo nchini Mali.

Baada ya mechi hiyo ya Bamako, timu hizo zitarudiana tena wikiendi ijayo Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Mara baada ya mchezo huo wa Machi 7, Yanga itabaki nyumbani kuikaribisha Monastir ili kuona kama italipa kisasi cha kipigo cha mechi ya ugenini au itaendeleza unyonge wake mbele ya timu za kutoka Afrika Kaskazini msimu huu, kwani kwenye mechi ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa ililazimishwa sare 1-1 nyumbani na Al Hilal ya Sudan kisha kwenda kulala ugenini 1-0 kabla ya kutoka suluhu na Club Africain nyumbani katika mechi ya play-off na kwenda kushinda 0-1 ugenini.

Ikimalizana na US Monastir, itasaliwa dhidi ya TP Mazembe Aprili Mosi mjini Lubumbashi.

Mechi hiyo ya mwisho itapigwa huku ikiwa tayari dira ya kundi hilo ikiwa imeshafahamisha timu zipi mbili zitakazoweza kusonga mbele kwenye robo fainali.

Kama vijana wa Nasreddine Nabi watazichanga vyema karata za mechi zao tatu za awali, zikiwamo mbili za nyumbani, basi huenda mchezo huo wa mwisho kule DR Congo usiwaumize kichwa. Lakini kama mambo yataenda kinyume, watarajie upinzani mkali, kwa vile TP Mazembe haitakubali kirahisi kupasuliwa nje ndani na hapo ndipo mchezo huo wa mwisho utakavyokuwa mgumu zaidi.

SOMA NA HII  SENZO - ETI YANGA TUSAHAU UBINGWA KISA SARE..!!? AHH WAPI..!!