Hesabu za kuimaliza Vipers zimetawala kichwani mwa kocha wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ ambaye anaamini kama watavuna pointi nyingine tatu dhidi ya bingwa huyo wa Uganda watakuwa wamejiweka pazuri katika msimamo wa kundi C kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
Awali Simba iliibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na beki, Henock Inonga ikiwa ugenini kwenye Uwanja wa St Mary’s, Kitende.
Kocha huyo raia wa Brazil, ameonyesha kuwa na imani kubwa kwenye hesabu zake na mshambuliaji Moses Phiri.
Robertinho alisema Phiri ni mshambuliaji mzuri na yupo tayari kuendeleza kile ambacho alikuwa akikifanya mwanzoni mwa msimu kabla ya kupata majeraha ambayo yalimweka nje ya uwanja kwa takribani miezi miwili.
“Yupo kwenye mipango yangu ya mchezo, ni mshambuliaji mzuri ambaye yupo tayari kujitoa kwa asilimia zote kwa ajili ya kuisaidia timu,”
“Sina shaka naye, lakini tusubiri kuona uamuzi wa mwisho ni upi juu ya nani ambaye anaweza kuanza ila ninafuraha kuwa na machaguo mengi na kila mmoja amekuwa akifanya vizuri mazoezini,” alisema kocha huyo.
Phiri ambaye alicheza kwa dakika 61 dhidi ya Vipers na kutoa asisti ya bao la ushindi kwa Simba na kupiga mashuti mawili ndiye kinara wa mabao kwenye kikosi hicho cha Robertinho kwenye ligi akifunga 10 sawa na Saido Ntibazonkiza.
Alimuelezea Phiri kiufundi kwamba ana jicho la kuona nafasi, anashambulia kwenye maeneo yote kwa maana ya kati na pembeni “Ana maamuzi ya haraka ya kufunga anapopata nafasi, kuwa fiti kwake kutasaidia safu ya ushambuliaji kuzalisha mabao mengi, akisaidiana na wenzake,”alisema.
Upande wake Phiri alisema,”Kwa sasa nipo fiti nahitaji dakika nyingi ili niweze kufunga mabao, malengo yangu mwanzoni mwa msimu ilikuwa ni kufikisha zaidi ya 15 ambapo mabao 10 niliyofunga kwenye mechi za mzunguko wa kwanza,” alisema Phiri na kuongeza;
“Ndio maana nasema angalau nifikishe idadi ya mabao 15 ambayo nitahitaji muda zaidi wa kucheza ambao utanijengea kujiamini zaidi, tofauti na dakika chache ambazo zinakuwa na presha kubwa.”
Hata hivyo, ni kama kocha kasikia ombi lake baada ya kusema ni mshambuliaji anayemtegemea zaidi kwenye michezo iliopo mbele yao ya Caf, ASFC na Ligi Kuu.