Home Habari za michezo VIGOGO TFF WAFICHUA ‘MADUDU’ YA FEI TOTO….AAMBIWA ATAJE TIMU ANAYOTAKA KWENDA JAMBO...

VIGOGO TFF WAFICHUA ‘MADUDU’ YA FEI TOTO….AAMBIWA ATAJE TIMU ANAYOTAKA KWENDA JAMBO LIISHE…

Tetesi za Usajili Yanga

Wakati vigogo waliowahi kuongoza Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wakifichua kwamba sakata la Feisal Salum ‘Fei Toto’ linacheleweshwa na mchezaji mwenyewe na TFF haiwezi kulimaliza bila kuwepo kwa mazungumzo ya mchezaji na klabu yake, wameeleza kama Yanga italazimika kumuuza, basi dau lake halitazidi Sh 400 Milioni.

Feisal na Yanga wameingia kwenye mgogoro wa kimkataba, uliopelekea klabu hiyo kupeleka shauri kwenye Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji ya TFF iliyomrejesha kiungo huyo Yanga.

Klabu hiyo juzi pamoja na mambo mengine, ilieleza iko tayari kumruhusu Feisal kuondoka kwa kuzingatia sheria za uhamisho zinazotambuliwa na TFF na FIFA na ikiwa kuna klabu inamhitaji, Yanga iko tayari kufanya mazungumzo wakati wowote.

Hata hivyo, baadhi ya makatibu wakuu wa TFF kwa nyakati tofauti, Selestine Mwesigwa na Aden Rage (wakati ikiitwa FAT) kwa nyakati tofauti wamefichua kwamba, wanaomshauri Feisal ndiyo tatizo kwenye sakata hilo ambalo ni jepesi na mchezaji huyo hazuiwi kuondoka.

Rage alisema, Feisal kuingiza Milioni 100 kwenye akaunti ya Yanga halikuwa suluhisho la yeye kuondoka kwani hajui klabu inataka nini.

“Arudi Yanga akae nao mezani kwanza, inaweza ikamwambia hata Milioni 50, yeye kuomba TFF ili aondoke pia si suluhu japo ni kweli TFF ina mamlaka, lakini haiwezi bila kuwepo kwa mazungumzo ya Yanga na mchezaji,” alisema Rage.

Alisema Feisal anapaswa kuwa mkweli kwa Yanga, aeleze ni klabu ipi anahitaji kwenda na Yanga haiwezi kukataa kumuuza akifafanua kwamba dau lake halitakuwa zaidi ya Sh 400 milioni.

“Kama wakati anasainishwa ilikuwa ni milioni 100, sasa thamani imepanda haitokuwa chini ya milioni 350 hadi 400 kwa klabu inayomtaka kumnunua, Yanga wakiweka hesabu za ajabu, Fifa wanaweza kuingilia na utaratibu huko hivyo,” alisema Rage.

Alisema tatizo liko kwa wanaomshauri Feisal, akitolea mfano suala la Neymar alipotaka kuondoka Barcelona na kujiunga na PSG ya Ufaransa.

“Mwanasheria wake alikwenda kuzungumza na Barcelona, wakamuuza, lakini kwa alichokifanya Feisal mwanzo hakikuwa sahihi, asiogope wala kufanya siri ni timu ipi anataka kwenda, arudi Yanga aseme anataka kuvunja mkataba kwa sababu hizi na hizi,” alisema.

Kuhusu barua ya Yanga iliyobainisha kuhusu kuwa na utaratibu wa kuboresha maslahi ya wachezaji wake, Rage alisema sio kwa Feisal hata akirejea.

“Tayari ameonyesha nia mbaya kwa klabu na hana dhamira tena ya kucheza Yanga, hata wakisema wamlipe hela nyingi kiasi gani, italeta mgogoro tu baadae hata na wachezaji wengine,” alisema Rage.

Mwesigwa mtendaji wa zamani wa TFF alisema kwa hiki kinachoendelea, Yanga imeonyesha ustaarabu wa hali ya juu kwa Feisal ambaye kwa mujibu wa klabu hiyo ana mkataba nayo hadi Juni 30, 2024.

“Mkataba wake na Yanga utavunjwa na wao wawili, kama kungekuwa na mazungumzo ya pande hizo na hayaendi sawa, basi mmoja angeweza kuomba TFF ivunje mkataba huo, lakini bado hakuna mazungumzo ya pande hizo. “Kwa suala hili, Yanga wamekuwa wastaarabu, lakini kisheria kuna ugumu kwa Feisal katika njia alizopita kabla, arudi Yanga wakae mezani wamalizane, ikishindikana ndipo anaweza kuiomba TFF kuingilia,” alisema.

SOMA NA HII  VIDEO: YANGA KUSUKA UPYA KIKOSI CHAKE,