KILA nikiwafikiria Mamelodi Sundowns, siombei wakutane na Simba kwenye Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Jamaa wanatisha balaa.
Kama Simba watafanikiwa kupenya kuingia katika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ni bora wakutane na kinara wa kundi A ambaye kuna uwezekano mkubwa akawa Wydad ya Morocco au kinara wa kundi D ambaye kuna uwezekano mkubwa akawa ni Esperance.
Licha ya ubishi wote ambao umekuwepo kijiweni, kwenye hili la Mamelodi, hakuna hata mmoja aliyethubutu kubisha zaidi wengi wametikisa kichwa kuashiria kuwa wanaunga mkono sala zangu kuwa Simba isikutane na Mamelodi Sundowns.
Jamaa kwanza wana bonge la timu halafu limeundwa na kundi kubwa la wachezaji wa nyumbani kwao Afrika Kusini lakini wengi wamekulia katika njia sahihi za kimpira maana kule Afrika Kusini kuna vituo vya soka la vijana vingi kuliko hata idadi ya timu zao.
Safu yao ya ulinzi sio tishio sana ila tatizo kubwa ni ile safu yao ya ushambuliaji. Ina watu wana njaa kweli na kumpiga mtu tatu, nne, tano na hata sita kwa ni jambo la kawaida wakiongozwa na yule Mnamibia, Peter Shalulile.
Sawa Simba inaweza kupata bao au hata mabao dhidi yao lakini je kwa ile beki ya Simba inaweza kuwazuia wale wasifunge? Kwanza Simba yenyewe imekuwa butu katika hatua hiyo ya makundi ya ligi ya mabingwa Afrika ambapo hadi sasa imefunga mabao sita tu, je inaweza kuwafunga nyingi wale Mamelodi hata kama ukuta wao ndio dhaifu kama tunavyoaminishana?