ILIANZA Yanga. Ilisafiri hadi Highland Estate, Mbarali mkoani Mbeya kucheza na Ihefu katika mechi ya Ligi Kuu Bara ikiwa haijapoteza mechi 49, ikalala mabao 2-1. Kuna mashabiki walidhani Ihefu iliwaotea tu watetezi hao, lakini juzi kati ikaenda Azam FC nayo ikapigwa kidude.
Aprili 10, itakuwa zamu ya Simba kuifuata Ihefu kwenye uwanja huo kwa mechi ya Ligi Kuu na mastaa wa timu hiyo ya Mbeya wametuma salamu mapema kwa Wekundu wakitamba kwamba hata wao nao wakikaa vibaya watapigwa kama vigogo waliotangulia.
Simba watakuwa wageni wa Ihefu siku chache baada ya kuvaana kwenye mechi ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) itakayopigwa Uwanja wa Uhuru, Aprili 7 na mmoja wa mastaa wa timu hiyo, Yacouba Songne amesema kama walizisimamisha Yanga na Azam, ndivyo walivyojipanga kuwasimamisha Wekundu hao.
Yacouba aliyesajiliwa dirisha dogo na kuanza na moto alisema kama walivyofanya kwenye mechi zilizopita ikiwamo Yanga na Azam, wataendelea hivyo hata kwa Simba.
“Tunashukuru matokeo siyo mabaya na Mungu akitujaalia tunaenda kushinda mechi zote dhidi ya Simba kama tulivyofanya kwenye michezo iliyopita,” alisema nyota huyo mwenye mabao mawili na asisti tatu.
Kuhusu kiwango chake, alisema kupambana ndio siri ya kuonekana bora uwanjani na kwamba mkakati wake ni kuendelea kuonesha uwezo wake uwanjani.
Alisema mpira ndio kazi yake na anachofanya ni kutimiza wajibu akisema kiu yake ni kuona timu hiyo ikiendelea kufanya vizuri kusaka nafasi za juu na kufika mbali kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho.
“Ni kupambana ukizingatia mpira ndio kazi yangu. Natamani kuona Ihefu ikiendelea kufanya vizuri na kumaliza nafasi nzuri kwenye ligi na kufika mbali kwenye kombe la ASFC,” alisema Mbukinafaso huyo.