WAKATI kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Uganda, kikiiweka Taifa Stars katika mazingira magumu ya kufuzu fainali zijazo za Mataifa ya Afrika (Afcon), nyota mwenye historia na fainali hizo, Augustino Magali ‘Peter Tino’ amesema ni muda wa benchi la ufundi, viongozi na wadau kubadilika.
Tino aliyefunga bao mwaka 1979 dhidi ya Zambia katika sare ya 1-1 na kuipeleka Stars fainali za kwanza kwa zilizofanyikia Nigeria, alisema soka la sasa la Tanzania, ni jina mbele uwezo nyuma, jambo ambalo haliwezi kuipa nchi matokeo chanya kwenye mpira.
“Zama zinabadilika, hakuna mafanikio ya soka ya kutanguliza jina, ni uwezo wa mchezaji ndiyo uwe mbele jina lake nyuma, Stars ikikubali kubadilika tutapata matokeo mazuri,” alisema staa huyo wa zamani wa Yanga, Pan Africans, Majimaji, African Sports na Taifa Stars.
Alisema ni wakati wa kocha wa timu hiyo na washauri wake kuwapa fursa damu changa kuipigania timu ya taifa ambayo anaamini kama watawaaminiwa watafanya vizuri.
“Watoto wa kuipa matokeo Stars wapo wengi, tatizo hawaaminiwi na kupewa nafasi, bado tuna zile zama za kuangalia jina na si kiwango cha mchezaji,” alisema na kuongeza.
“Soka la sasa watu hawaogopi jina wanaangalia uwezo wako tu, tatizo sisi bado tuna mambo ya kizamani ya kuangaliana usoni ambayo yamepitwa na wakati hata sisi tulipofuzu mwaka 1980 hayakuangaliwa majina bali uwezo wako ambao ndiyo ulitubeba na kuendelea kulinda jina lako kwenye timu.
Kuhusu nafasi ya kufuzu kwa Stars iwapo itazifunga Algeria au Niger au timu zote mbili ili kwenda Ivory Coast zitakapofanyuika fainali zijazo, Tino alisema nafasi hiyo ni finyu kwa wawakilishi hao wa nchi.
“Nafasi ya kufuzu sasa ni finyu sana, itabidi ifanyike kazi ya ziada, watu wajitolee wafumbe macho na kuacha kuangalia majina, ambayo sasa Stars wapo wengi wanacheza kwa kutanguliza majina mbele na uwezo nyuma, tusioneane aibu, huenda bahati ikawa upande wetu kwa mechi mbili zilizosalia japo nafasi ya kufuzu upande wetu ni finyu,” alisema.