Home Azam FC AZAM FC WAGOMEA MAKOCHA WABONGO…IBENGE KUMWAGA WINO

AZAM FC WAGOMEA MAKOCHA WABONGO…IBENGE KUMWAGA WINO

AZAM FC WAGOMEA MAKOCHA WABONGO...IBENGE KUMWAGA WINO

Wakati Azam FC ikibakiza mechi tano kumaliza msimu wa Ligi Kuu Bara, tayari imeanza kimyakimya kutafuta kocha mpya
atakayeiongoza msimu ujao ambao imepania kutwaa ubingwa huku kocha wa Al Hilal ya Sudan, Mkongomani Florent Ibenge akitajwa.

Azam ilianza msimu huu ikiwa na kocha Mmarekani mwenye asili ya Somalia Abdihamid Moalin, ikiwa na malengo ya kuchukua ubingwa ikafanya usajili mkubwa, lakini baadaye akaondoshwa kutokana na mwenendo mbaya na mikoba yake kuchukuliwa na Mfaransa Denis Lavagne.

Hata hivyo Lavagne alifukuzwa na timu kubaki chini ya kocha wa makipa Mhispania Dani Cadena akisaidiwa na Kally Ongala na kocha mchezaji Aggrey Morris ambao uongozi upo kwenye mchakato wa kuwaletea bosi wao.

Taarifa kutoka ndani ya Azam zinaeleza, mabosi wana majina ya makocha wanne mezani akiwemo Ibenge ambao wanajadiliwa ili apatikane mmoja atakayetua Chamazi kabla ya msimu huu kumalizika ili akione kikosi kilichopo, apendekeze usajili na aende na timu kujiandaa na msimu kuhakikisha lengo la ubingwa linatimia.

Chanzo kimeeleza, katika majina hayo hakuna kocha mzawa hata mmoja lakini moja ya majina ambayo matajiri hao wa Chamazi wanawaza kumwaga pesa kulipata ni Ibenge anayekinoa kikosi cha Al Hilal ya Sudan.

Inaelezwa mabosi wa juu wa Azam wanaamini wakimpata Ibenge ataibadili timu ndani ya muda mfupi kama alivyofanya Al Hilal na kufikia malengo na tayari wamemtumia ofa ambayo bado hajaijibu licha ya kuwepo na mawasiliano ya mara kwa mara baina ya pande zote mbili.

Azam kwa sasa ipo nafasi ya nne kwenye msimamo na alama 47 nyuma ya vinara Yanga wenye 65, Simba (57) na Singida Big Stars (48).

SOMA NA HII  MSHAMBULIAJI BONGO...APEWA SHAVU UBELGIJI...KUKIPIGA NA SAMATTA