Home Habari za michezo YANGA SC YASHEREKEA UBINGWA…”SIMBA WATAKIMBIA UWANJANI…WALITUFUNGA MIDOMO

YANGA SC YASHEREKEA UBINGWA…”SIMBA WATAKIMBIA UWANJANI…WALITUFUNGA MIDOMO

Habari za Yanga SC

BAADHI ya mashabiki wa Yanga Nyanda za Juu Kusini wamesema wapo kwenye maandalizi ya sherehe za ubingwa wa Ligi Kuu, huku wakitaja mechi dhidi ya watani zao, Simba kuwa ndio itawapa mwanga zaidi.

Hadi sasa Yanga ndio kinara kwenye Ligi Kuu kwa pointi 65 ikiwaacha alama nane Simba waliopo katika nafasi ya pili kwa pointi 57 baada ya timu zote kucheza mechi 24 wakibakiza sita.

Yanga ambao wanatetea taji hilo kwa msimu wa pili wanahitaji ushindi wa mechi tatu kati ya sita ili kufikisha alama ambazo timu yoyote haitazifikia ikiwamo Simba.

Pia mabingwa hao mara 27 wanapiga hesabu za mechi tatu dhidi ya Kagera Sugar, Simba na Singida BS ambapo wakishinda hizo watatangaza ubingwa msimu huu kwa kufikisha alama 74.

Mechi zilizobaki kwa ‘Wananchi’ ni dhidi ya Kagera Sugar, Simba, Singida Big Stars, Dodoma Jiji, Mbeya City na Tanzania Prisons.

Ally Nzowa ambaye alikuwa mwenyekiti wa Yanga mkoani Songwe, alisema kwa sasa hawaoni timu yoyote ya kuwazuia kuchukua taji la Ligi Kuu msimu huu na kwamba tayari wameanza maandalizi ya sherehe.

“Kwanza tukimfunga Simba ndio hesabu rasmi za ubingwa zinaanzia hapo na lazima wafungwe, mipango yetu kwa sasa ni kushona suti kujiandaa na sherehe,” alisema Nzowa.

Habibu Mzava aliyewahi kuwa katibu mwenezi wa Yanga mkoani Katavi alisema katika mechi zilizobaki hawaoni timu ya kuwazuia hata kwa sare akitamba kuwa watabeba ubingwa kwa misimu mitano mfululizo.

“Kwa misimu minne nyuma watani zetu walitufunga midomo sasa nao acha waumie, Yanga tutabeba kwa miaka mitano mfululizo kisha tuamue kumuachia mwingine au tuendelee,” alitamba Mzava.

Shabiki wa timu hiyo jijini Mbeya, Jackson Fundi alisema mwenendo ilionao Yanga unaonyesha kwamba itazidi kutesa akisisitiza kuwa kwa sasa wanapaswa kufikiria mechi za kimataifa na siyo za ndani.

“Kwa ndani sioni wa kutuzuia, hivyo lazima nguvu ziwe kwenye mchezo ujao wa Kombe la Shirikisho (Afrika) dhidi ya US Monastir ili tuingie robo fainali na hiki ndicho kiwe kipaumbele zaidi,” alisema Fundi.

SOMA NA HII  UNAMKUMBUKA KAHATA..HUYU HAPA...KALA SHAVU TIMU YA POLISI KENYA...AFICHUA HAYA MAPYA...