WAKATI baadhi ya wadau wa soka nchini wakionesha wasiwasi kwa Simba kupenya mbele ya wapinzani wao, Wydad AC ya Morocco, beki wa zamani wa timu hiyo ambaye kwa sasa ni Kocha wa KVZ, Amri Said ‘Jaap Stam’ ameivusha timu hiyo hadi nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Simba imepangwa na Wydad katika mechi za robo fainali kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayoanza Aprili 21 kabla ya kurudia Aprili 28, ili kukata tiketi ya nusu fainali na tangu droo hioyo ifanyike baadhi ya wadau na mashabiki wamekuwa na wasiwasi kwa Simba kuweza kupenya.
Hii inatokana na ubora wa kikosi ilichonacho Wydad ambao ni watetezi wa taji la michuano hiyo, lakini Stam alisema Simba inaweza kushangaza wengi kwa kuwatoa Wamorocco bila kujali ubora na ukubwa wake na kufuzu nusu fainali ya michuano hiyo.
Alisema kitu cha msingi inachopaswa kufanya Simba ni kujiandaa kisaikolojia na kujipanga kiufundi kuhakikisha wanatoboa na kwamba inawezekana.
“Naamini kwa benchi ililonalo Simba inaweza kufanya vizuri, ni kweli ni mechi ni ngumu, lakini inawezekana kabisa kwenda nusu fainali iwapo itajiandaa vyema kwa siku zilizosalia,” alisema.