Simba imepanga kufanya mabadiliko makubwa ya kikosi na hata katika safu yake ya uongozi malengo yakiwa ni kuhakikisha inarudisha mataji yote iliyoyapoteza msimu huu na kuwa na muendelezo wa kufika hatua za juu zaidi za mashindano ya klabu Afrika.
Lakini wakati hayo yakiendelea tayari Wydad imeshatanguliza watu wao Dar es Salaam tayari kwa mechi ya wikiendi hii na Simba wameshashtukia mchecheto wao.
Hadi sasa Simba haijafanikiwa kutwaa kombe lolote, lakini ikiwa na nafasi ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho pamoja na kuwa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mmoja wa viongozi wa juu wa Simba, alilihakikishia SOKA LA BONGO kuwa wanaendelea na vikao vya ndani vya kimkakati kabla ya kuweka mambo hadharani na kwamba mabadiliko hayo yataanzia kwenye uongozi.
Alisema kuwa bodi ambayo inasimamiwa na Mwenyekiti Ally Salim Try Again’ imekubaliana kurudisha kamati ya mashindano ambayo kwa muda mrefu haikuwepo na itahusisha wanachama wenye msuli wa kifedha na wenye uzoefu na soka la Tanzania na Afrika kiujumla na baada ya hapo yatahamia kwenye kikosi cha kibingwa.
Sababu kuu ya kuundwa kwa kamati hiyo ni kupunguza mzigo wa majukumu kwa bodi na sekretarieti ya Simba katika kuisimamia na kuratibu shughuli za timu kutokana na uwingi wa mashindano ambayo imekuwa ikishiriki hasa yale ya kimataifa. “Kuna tathmini ambayo imefanyika na imeonekana tuna uhitaji wa kamati ya mashindano ambayo haikuwepo kwa muda mrefu sasa.
Baadhi ya wajumbe kwenye hiyo kamati wameshaanza kutekeleza majukumu yao kimyakimya. Kuna mengi sana tumejifunza na tunaendelea kujifunza ambayo tumekuwa tukiyafanyia kazi siku hadi siku na tunazidi kufanikiwa,” alidokeza kigogo huyo na kusisitiza wanafanya mambo kwa umakini mkubwa.
Ingawa chanzo hicho hakikuwa tayari kutaja majina ya wajumbe wanaounda kamati hiyo, SOKA LA BONGO linafahamu kuwa miongoni mwao ni Hassan Hassanoo ‘Mpiganaji’, Hassan Dalali, Swedy Nkwabi na Rashid Hamsini ambaye alikuwa anagombea nafasi ya ujumbe kwenye uchaguzi uliopita.
Lakini wakati wakisuka kamati hiyo ya mashindano, Simba imepanga kufanya mabadiliko makubwa ya kikosi chake ambapo imempa rungu kocha Robert Oliviera ‘Robertinho’ kupendekeza nyota ambao hawahitaji katika kikosi chake ili wapitishiwe panga wakati wa usajili, lakini wenyewe wakiwa tayari na majina ambayo yakatwa na mengine yanaingia.
Eneo ambalo Simba imepanga kulifanyia marekebisho makubwa ni lile la kiungo na safu ya ulinzi na kuna kundi kubwa la wachezaji ambao wataonyeshwa mlango wa kutokea kutokana na viwango vyao kuonekana kushindwa kumshawishi kocha Robertinho.
“Tutakuwa makini zaidi katika usajili wa msimu huu hasa kwa wachezaji wa kigeni.
Tunataka kusajili wachezaji wazuri ambao wanacheza kwenye timu zao hapa Afrika ambao wataleta ushindani kwenye timu na sio kuja kukaa benchi. Tutasajili wachezaji ambao watamfanya hata kocha aumie kichwa nani amuanzishe na nani aanzie benchi kama ilivyo sasa hivi kwa Jean Baleke na Moses Phiri.”
“Hata wazawa watakuwa ni wale ambao viwango vyao havitii shaka. Mfano beki kama Kennedy Juma huwa hapati nafasi ya kucheza lakini unaona kila anapoingia amekuwa akiisaidia timu, tutaongeza wachezaji wa aina hii.