Upo msemo mmoja wa Kiingereza unasema ‘Trust the process’ kwa maana ya kuamini katika mchakato, huku ukitarajia matokeo chanya, msemo ambao kwa sasa unaendana kwa ukaribu na maisha ya mchezaji wa Simba SC, Kibu Denis Prosper.
Kutoka moja ya kambi za wakimbizi mkoani Kigoma alikolelewa, Kibu ndoto yake kuu ilikuwa ni kucheza soka katika viwango vya juu na akaamini katika mchakato wake ambao ni kucheza kwa juhudi na kufuata misingi ya soka ilivyo bila kujali nini na nani anasema nini.
Alicheza timu kadhaa Kigoma katika ngazi za chini akiamini katika mchakato na baadae akafunga safari hadi Mkoani Kagera na kujiunga na klabu ya Kumuyange FC iliyokuwa ikishiriki Ligi Daraja la pili wakati huo ikitafuta kupanda Ligi Daraja la Kwanza lakini kwa sasa iliuzwa Dodoma na inaitwa Fountain Gate iko Championship.
Timu hiyo iliyokuwa na masikani yake mitaa ya Kumuyange na Kumunazi wilayani Ngara ilimuamini Kibu na kuwa moja ya mastaa wake na yeye akaamini katika mchakato akakiwasha na mwisho wa siku kuonekana na Geita Gold kipindi hicho ikiwa Daraja la Kwanza na kumsajili.
Pale Geita alicheza kwa msimu mmoja kwa kiwango cha hali ya juu akiamini katika mchakato na misingi ya soka huku ndoto yake ikiwa ni kucheza katika ngazi za juu na imani ikamlipa kwani alisajiliwa Mbeya City ya Ligi Kuu msimu uliofuata.
Kutoka Geita hadi Mbeya kujiunga na wababe wa jiji hilo, ilikuwa ni safari ya matumaini na furaha kwa Kibu kwani alifikisha ndoto yake ya kwanza kucheza Ligi Kuu na pili aliamini pale City ni sehemu sahihi kwake kufikia ndoto zake kubwa kubwa.
Kama ilivyokawaida yake kuishi katika imani ya mchakato, Kibu akiwa Mbeya City msimu wa 2020/2021 alicheza Ligi Kuu kwa kiwango bora na kuwa miongoni mwa wachezaji tegemeo wa kikosi hicho.
Ubora wake akiwa City ulizifanya timu za Simba SC, Yanga na Azam ambazo zinajinasibu kuwa vigogo wa ligi ya Bongo, kuanza kupigana vikumbo kutaka saini yake na mwisho wa siku Simba ikashinda na kumsaini kwa mkataba wa miaka miwili pia wakati akiwa City aliitwa kwa mara ya kwanza timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’.
Msimu wa 2021/2022, Kibu alivaa uzi wa Mnyama kwa mara ya kwanza ikiwa ni miongoni mwa ndoto zake kubwa kucheza katika klabu kubwa nchini lakini hapo ndipo akajua kuwa bado anahitaji kuendelea kuamini katika mchakato.
Usajili wa Kibu kutua Simba uliibuka na mambo mengi, lakini kubwa zaidi ilikuwa suala lake la uraia kwani hakuwa na uraia rasmi wa Tanzania na asili yake ikiwa ni DR Congo.
Hapo mengi yalisemwa na kutaka kumtoa mchezoni lakini alikaza nafsi na baadae kukamilisha taratibu zote na kupewa uraia wa Tanzania na ruksa sasa kuanza kukiwasha ndani ya Simba.
