KIPA chipukizi wa Simba, Ally Salim amesema kuwa licha ya kuwa namba tatu na kukosa nafasi kwenye kikosi cha kwanza lakini alikuwa anajiandaa vizuri ili kukabiliana na dharura yoyote ambayo ingetokea.
Salim alidaka kwenye dabi ambapo Simba iliondoka na ushindi wa mabao 2-0 yaliyofungwa na Enock Inonga na Kibu Denis.
Alisema kutokana na ubora wa Aishi Manula na Beno Kakolanya ulimpa matumaini ya kufanya vizuri na kuamini mchezo huo ni kama mingine.
“Kaka yangu Aishi alinitumia ujumbe muda mchache kabla ya mchezo na kuniambia kuwa nicheze kawaida kama ninavyocheza nikiwa katika mazoezi kwani hiyo ni mechi tu kama nyingine nilikuwa najiandaa mapema huku nikijua wao wanaocheza ni binadamu ipo siku wataumia”,alisema Salim ambaye alionyesha kiwango kizuri.