Home Habari za michezo SIMBA KUKUTANA NA VINARA HAWA…LIGI YA MABINGWA AFRIKA

SIMBA KUKUTANA NA VINARA HAWA…LIGI YA MABINGWA AFRIKA

KIUNGO HUYU WA CONGO ATUA MSIMBAZI....USAJILI WA KIBABE...ROBERTINHO AUPIGA MWINGI

SIMBA imerejea nchini ikitokea Morocco ilikoenda kucheza mechi ya mwisho ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuchapwa mabao 3-1 na vinara wa kundi C, Raja Athletic, ila kwa sasa tayari kuna vyuma vitatu ambavyo Wekundu hao watalazimika kuchagua kusuka au kunyoa tu.

Simba iliyomaliza nafasi ya pili ikikusanya pointi tisa, kwa sasa imepata uhakika wa kukutana na timu tatu vigogo vilivyomaliza kama vinara wa makundi ya A, B na D kwenye mechi za robo fainali wakati droo ya mechi hizo ikifanyika kesho kutwa jijini Cairo, Misri.

Iwe isiwe ni lazima Simba kwenye droo hiyo ikutane na Wydad Casablanca ya Morocco iliyoongoza Kundi A au Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, vinara wa Kundi B ama Esperance ya Tunisia iliyoongoza Kundi D na hapo chini ni wasifu wa wapinzani hao watakaokutana na Mnyama katika mechi hizo za robo na Wekundu hao kuamua kukomaa waende nusu fainali au wakubali yaishe.

MAMELODI

Timu hiyo inayofundishwa na kocha mzawa Rulan Mokwena, ina taji moja la Ligi ya Mabingwa iliyobeba mwaka 2016 mbele ya Zamalek ya Misri, pia imewahi kumaliza ya pili mwaka 2001 ilipochapwa kwenye fainali na Al Ahly pia ya Misri kwa jumla ya mabao 4-1.

Msimu huu, wanaume hao wanaovaa jezi za rangi ya njano na bluu ni kati ya timu zilizo kwenye kiwango bora, ikifuzu robo fainali kupitia Kundi B lililokuwa na vigogo wengine wa Al Ahly na Al Hilal ya Sudan sambamba na CotonSport ya Cameroon.

Walimaliza wakivuna pointi 14, kupitia ushindi wa mechi nne nne na sare mbili, huku ikiwa haijapoteza mchezo wowote kama ilivyo kwa Raja Casablanca na imefunga mabao 14 na kufungwa saba katika mechi hizo sita za makundi.

Endapo Simba itaangukia mikononi mwao, basi italazimika kutumia vizuri mechi ya kwanza ya nyumbani kupata ushindi mnono kwani Wasauzi hao wapo vizuri zaidi nyumbani kuliko ugenini.

Kwenye makundi Mamelodi imeshinda mechi moja tu ya ugenini dhidi ya vibonde CotonSport, huku ikitoa sare mbili dhidi ya Al Hilal na Al Ahly, lakini nyumbani imeshinda mechi zote tatu.

Kinara wa mabao wa Mamelodi ni kiungo mshambuliaji Cassius Mailula aliyefunga matatu katika hatua hiyo, akifuatiwa na beki wa kulia Khuliso Mudau na mshambuliaji hatari Peter Shalulile kila mmoja akitupia mawili na wenye bao mojamoja ni Thapelo Morena, Marcelo Allende, Themba Zwane, Teboho Mokoena na Abubeker Nasir raia wa Ethiopia ambaye Simba ilimkosa kumsajili dakika za mwisho msimu uliopita.

WYDAD ATHLETIC

Simba pia inaweza kukutana na watetezi wa taji la michuano hiyo kwa sasa, na moja kwa moja italazimika kurudi tena uwanja uleule wa Mohamed V, jijini Casablanca Morocco kuvaana na wababe hao waliowahi kukutana nao mara moja mwaka 2011 na kupasuliwa mabao 3-0.

Wydad kwa msimu huu ilianza kwa kusuasua ikimtimua hadi kocha, lakini sasa imeshika kasi na kumaliza kinara wa Kundi A na kabatini kwao historia inaonyesha wana mataji matatu ya CAF ikiwamo la mwaka 1992, 1975 na 2022, huku ikimaliza ya pili katika miaka ya 2011 na 2019.

Kundini msimu huu ilimaliza kama kinara kwa kukusanya pointi 13, ikipoteza mechi moja tu ikicheza ugenini dhidi ya JS Kabylie yua Algeria, ikishinda nne na kutoka sare moja.

Kupoteza ugenini inaweza kuwa habari njema kwa Simba kama itaamua kukomaa na ule msemo wa Kwa Mkapa hatoki mtu kupata ushindi kabla ya kwenda Casablanca.

Hata hivyo, Wydad ina rekodi ya kushindwa ugenini ikiwamo kuifumua Petro de Luanda ya Angola kwa mabao 2-0 na nyumbani imeshinda mechi zote kuonyesha walivyo wazuri. Kinara wa mabao wa timu hiyo ni mshambuliaji raia wa Senegal, Bouly Sambou mwenye mawili, huku beki wa kati Mkongomani Arsène Zola, Yahya Jabran na winga wao wa kushoto Zouhair El Moutaraji wote hawa wakifunga mara moja.

ESPERANCE DE TUNIS

Kuna Esperance de Tunis ya Tunisia nao inaweza kukutana na Simba ikiwa na rekodi ya kuchukua taji hilo mara nyingi zaidi kuliko timu zote tatu zinazoweza kukutana kwenye robo robo fainali, ikibeba mara nne miaka ya 1994, 2011, 2018 na 2019, huku ikimaliza ya pili miaka ya 1999, 2000, 2010, 2012.

Kwenye makundi Esperance imekusanya pointi 11, ikiwa ndio timu iliyovuna pointi chache msimu huu na kuongoza kundi ikiwa Kundi D, ikishinda mechi tatu, ikitoka sare mbili na kupoteza moja.

Kwa hawa jamaa Simba lazima ijipange kweli kweli na kuhakikisha inashinda nyumbani, kwani Watunisia waliopoteza mabao 3-1 dhidi ya Zamalek ugenini, kisha mechi mbili za ugenini ilitoka sare na nyumbani imeshinda mbili na kutoka sare na majirani zao wa CR Belouizdad ya Algeria.

Nyota wanaopaswa kuchungwa na Simba kama watapangwa pamoja ni; mshambuliaji Mohamed Ben Hammouda mwenye mabao mawili, huku wengine wakiwa ni beki wa kati Mohammed Tougai, winga wa kushoto, Hamdou Elhouni na mshambuliaji Riad Benayad wenye bao moja moja kila mmoja.

MSIKIE KOCHA

Kocha wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ akizungumzia droo hiyo alisema timu yake haiwezi kuhofia timu yoyote na wachezaji wake wameendelea kuwa na mabadiliko makubwa ya kucheza mechi za nyumbani na ugenini.

Robertinho alisema licha ya kupoteza kwao dhidi ya Raja ugenini kuna makosa machache yaliyosababisha matokeo hayo lakini ameridhishwa na nidhamu ya mchezo kijumla kutoka kwa wachezaji wake huku akitamba anajua ni mfumo gani atatumia kuwakamata wapinzani wake.

“Simba haimuogopi yeyote hili narudia kusema, tuna mabadiliko makubwa ya ubora wa kucheza mechi hizi kubwa, tunaziheshimu zote ambazo tunaweza kukutana nazo lakini kwangu mimi na wenzangu tunasubiri kujua tutakutana na nani na baada ya hapo tutawatafuta kujua ubora wao na udhaifu wao kisha tutajipanga,” alisema Robertinho ambaye ameendelea kuibadilisha Simba taratibu.

SOMA NA HII  SOPU AZIGONGANISHA SIMBA NA YANGA....MMOJA AANZA MAZUNGUMZO NAYE...MWINGINE AMPANDIA DAU JUU KWA JUU....