Home Habari za michezo SIMBA YAANDAMWA NA NJAA KALI…KOCHA MKUU ATHIBITISHA…AMEZUNGUMZA HAYA

SIMBA YAANDAMWA NA NJAA KALI…KOCHA MKUU ATHIBITISHA…AMEZUNGUMZA HAYA

Habari za Simba SC

JANA tulianza sehemu ya kwanza ya mahojiano yetu na Kocha Mkuu wa Simba, Robert Oliviera ‘Robertinho akifafanua mambo mbalimbali ndani ya ajira yake akiwa na wekundu hao na hapa anaendelea kueleza presha aliyokumbana nayo wakati anaanza kazi.

“Presha haiwezi kukosekana katika aina hii ya kazi zetu, unajua mwanzoni nilitegemea kukumbana na hali ya watu kuelewa kile ambacho nataka nikitambulishe Simba kuanzia kwa wachezaji mpaka mashabiki, mimi ni kocha ambaye napenda presha kwa kuwa inanijenga, tulitaka kuweka mbinu mpya na sasa kila mmoja anafurahia kazi tuliyoanza nayo.

“Huwezi kukwepa presha kwenye soka, unachotakiwa ni kuibeba na kujua msimamo wako kama kocha ni upi, tulitaka kuibadilisha Simba icheze soka la kisasa zaidi nadhani sasa watu wanaona matunda ya kile tulichokazana nacho mwanzoni, ukiogopa presha ni bora ukakae nyumbani tu huwezi kufanikiwa katika soka.

TUTAJUANA HUKOHUKO ROBO FAINALI

“Kila mechi ina mpango wake kwasasa akili zetu ni kucheza vizuri dhidi ya Raja kule kwao baada ya hapo tutasubiri kujua tutakutana na timu ipi, hii sio Simba ambayo itawaogopa wapinzani nadhani mliona tulipocheza na Horoya, tuliwasoma vizuri walijua tutacheza kama tulivyocheza mchezo wa kwanza kwao, hapana tuliwabadilishia mambo mengi na ushindi mkubwa ukaja.

“Imani yangu kubwa ni kutokana na mabadiliko mazuri ya wachezaji wangu, wameonyesha ukomavu mkubwa wa kubadilika kwa haraka na sasa tunacheza kama Simba yenye njaa na ushindi hii ndio njia sahihi ambayo tunakwenda nayo sasa na tutamuangalia mpinzani wetu anayekuja baada ya mechi ya mwisho tutajipanga kufikia malengo yetu.

NIKWELI ALIKUWA HAMTAKI CHAMA

“Hakuna kocha anayeweza kumchukia mchezaji wake bora, nadhani kama kuna watu wanaliongelea hili kwa mrengo huo wanakosea, nina furaha sana kufanya kazi na Chama hapa Simba ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa nadhani tunachotaka kifanyike sasa Simba.

Chama pia anakitekeleza vizuri, unamkataaje mchezaji kama huyo, nilikwambia kabla kwamba mimi ni kocha ambaye napenda kukaa chini na mchezaji wangu na kumwelekeza kile ambacho anatakiwa kukifanya na alielewa kwa kuwa ni mchezaji mkubwa lakini kikubwa tulitaka awe na msaada kwa wenzake ndani ya uwanja, nadhani sasa mnamuona Chama bora na hatari zaidi.

“Nina maelewano mazuri sana na uongozi wa juu hasa mwenyekiti wa bodi na mwenyekiti wa klabu, napata ushirikiano wao mkubwa sana mapema tulipokutana Dubai nilifanya nao kikao nikawambia katika majukumu yao wafikirie zaidi watafanya makubwa zaidi na mimi huo ndio mtindo ninaokwenda nao huku kwenye timu, sikuja hapa kuwa mtalii nimekuja hapa kubadilisha mambo mengi mazuri kwa Simba ipate mafanikio.

MAISHA NA WASAIDIZI

“Jukumu langu kama kocha mkuu ni kuhakikisha kwanza najenga umoja katika watu wangu tunaounda benchi la ufundi, nilipokuja hapa nilimkuta Mgunda (Juma) nilipopata wasifu wake nikasema huyu nitaendeloea naye, ni kocha mzuri na tunasaidiana vizuri majukumu ya hapa Simba. “Nikamleta msaidizi wangu Sellami (Ouanane) huyu nilifanya naye kazi Tunisia kwa miaka mitatu pia ni kocha wa mazoezi ya viungo naye anafanya kazi bora sana kuna kocha wa makipa Zakaria (Chlouha) angalia kazi yake bora.

“Tuna meneja wa timu Patrick( Rweyemamu) ni mtu bora sana, kwanza anajua mpira lakini pia anaipenda sana Simba, anatusaidia mambo mengi kutokana na uzoefu wake hapa Tanzania wapo pia wengine lakini kitu bora kwangu ni kulijenga hili benchi na kuishi kama familia moja na hapa tunawafanya pia wachezaji kuiga maisha yetu.

“Mimi sio kocha ambaye najua kila kitu kuna wakati hawa wasaidizi wangu wananishauri juu ya maandalizi yetu kisha napima na nikiona kuna kitu bora nachukua na kubadilisha, sikuja hapa kuwatenganisha watu.

TSHABALALA, KAPOMBE STARS

“Nilishtuka kama ambavyo Watanzania wengi walishtushwa lakini niliwaambia wachezaji wangu watulie waendelee kucheza kwa ubora ,sikufahamu sababu ipi ya msingi kwa kuwa niliamini ubora wao wangeitwa lakini tuheshimu maamuzi ya makocha wenzetu.

“Unajua wachezaji wengi wameongezeka ubora sana hapa Simba, angalia Baleke (Jean) anafunga mabao matatu akitumia krosi za Kapombe, hawa ni mabeki wawili wa pembeni ambao wamejitahidi kuwa na muendelezo mzuri wa uchezaji wao, nilipenda nidhamu yao baada ya kutoitwa walitulia na niliona kocha wa Tanzania aliongea nao nadhani amewaonyesha thamani nzuri.

ITAENDELEA KESHO…….

SOMA NA HII  PAMOJA NA TIMU KUPATA MATOKEO...MGUNDA AVUNJA UKIMYA SIMBA...AANIKA ANACHOKITAKA ILI AFANYE KAZI VIZURI...