Home Habari za michezo TATIZO WABONGO TUNADHARAU SOKA LETU…SIMBA NA YANGA NI TISHIO KUBWA CAF

TATIZO WABONGO TUNADHARAU SOKA LETU…SIMBA NA YANGA NI TISHIO KUBWA CAF

Habari za Yanga SC

Bado mpira wetu una mapungufu mengi, wala tusiache kurekebisha. Bado mpira wetu una watu wengi tu wapigaji, wala tusikae kimya. Lakini kuna mahali tumepiga hatua. Kuna mahali tumesogea.

Tusijibeze sana. Katika kipindi cha miaka mitano ya hivi karibuni, Taifa Stars imefuzu na kushiriki michuano ya AFCON na CHAN. Sio jambo dogo hata kidogo. Katika kipindi hicho pia, timu ya Wanawake U-17 imecheza Fainali za Kombe la Dunia. Sio jambo dogo.

Tumewaona pia Tembo Warriors wakitinga Kombe la Dunia. Sio jambo dogo. Ni vizuri kuendelea kukosoa na kutoa suluhisho la maendeleo ya mpira wetu lakini tusibeze hatua hizi za maendeleo. Kuna mahali tumesogea. Kuna mahali tumepiga hatua. Sio jambo dogo.

Mapema mwaka huu ilitoka tafiti moja ikiitaja Ligi Kuu Bara kushika nafasi ya tano Afrika. Ni tafiti ambayo haikukubaliwa na wadau wengi wa soka nchini. Lakini kadiri msimu wetu unakoelekea, kuna vitu vinaonekana.
Kuna ubora unaanza kuonekana. Tuendelee kukosoa na kutoa suluhu lakini tusiibeze sana ligi yetu.

Haikuja kwa bahati mbaya Simba kuwafunga kwa Mkapa kila siku vigogo wa Afrika.

Watu wamejifunza. Watu wanawekeza. Haikuja kwa bahati mbaya Yanga kushinda mechi tatu za ugenini msimu. huu. Watu wamejifunza. Watu wamewekeza.

Kupata timu mbili kwa pamoja zilizofika Robo Fainali kwenye michuano ya CAF, sio bahati mbaya. Siku za nyuma, hii kitu haikuwa levo zetu. Mpira wetu unakuwa kwa kazi sana. Ligi yetu inakuwa kwa spidi ya 5G.

Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na wasaizidi wake wote kuna vitu hawafanyi sawa sawa kwenye mpira wetu. Fungia fungia ya viongozi wa soka, kwangu ina ukakasi mkubwa lakini suala la matokeo uwanjani na udhamini, Karia amefanya kazi kubwa sana. Anapaswa kupongezwa sana katika hili.

Kumekuwa na kasoro nyingi sana zilizogubika uchaguzi uliopita wa Klabu ya Simba.

Kumekuwa na sintofahamu nyingi sana pia juu ya Uwekezaji wa Mohammed Dewji ‘MO Dewji’, lakini tukitaka kuwa wa kweli, MO amefanya kazi kubwa sana pale Msimbazi.

Mpira wetu unakuwa wala tusijibeze sana. Kumekuwa na fukuto mara kwa mara pale Yanga juu ya mgongano wa kimaslahi kati ya Mdhamini wa Klabu hiyo, Ghalib Said Mohammed ‘GSM’ na Rais wa Klabu, Muhandisi, Hersi Said lakini Ufalme huu mpya wa Yanga ni pamoja na uwepo wa hawa watu pale Jangwani.

Azam FC ni kweli bado hawajafika pale ambapo Watanzania wengi wanatarajia kuwaona lakini, yapo maendeleo ya wazi kabisa waliyoanza kutapata. Leo hii pengine hakuna timu hata moja ya Ligi Kuu ambayo haina mchezaji aliyewahi kucheza Azam FC.

Bado wanateseka sana kupata matokeo mazuri uwanjani, lakini walau ndiyo timu yenye msingi mzuri na uwekezaji kwenye soka la vijana kuliko timu nyingine yoyote nchini. Unaruhusiwa kuibeza Azam FC lakini usipitilize. Kuna kitu kikubwa wamekiongeza kwenye mpira wetu.

Kwa ninachokiona Kimataifa kwa Simba na Yanga msimu huu, siku si nyingi tutakiona kwa Azam FC na Singida Big Stars. Ligi yetu inakuwa. Bado ina mapungufu mengi lakini inakuwa.

Hawa kina Fiston Mayele, Clatous Chota Chama, Aziz KI, hawako nchini kwa bahati mbaya. Wamekuja kuongeza thamani. Tusiache kuisema. Tusiache kukosea lakini, tusiibeze kupitiliza. Ukanda wa CECAFA hakuna nchi inayotufikia. Kuna kazi nzuri sana imefanyika.

Kazi ya kulinda Chapa (Brand) ni yetu sote. Sio jukumu la TFF na klabu peke yao. Siku hizi ni rahisi kuona wachezaji wa Afrika Magharibi tena wakiwa na umri mdogo kabisa wanakuja Tanzania. Sio jambo rahisi. Haiiji kwa bahati mbaya.

Siku za nyuma, wachezaji wengi kutoka Ghana, Nigeria, Mali na nchi za Magharibi walikuja kwetu wengi wakiwa ama na viwango vya kawaida au wakiwa Wamezeeka! Wachezaji kama Djigui Diarra, Pape Ousmane Sakho, Aziz Kl na Peter Banda usingewaona nchini. Bado hatujafika walipo Al Ahly, Mammelod Sundown au Wydad Casablanca lakini kuna mahali taratibu tumeanza kusogea.

Ni vizuri kukosoa na kutoa suluhisho lakini tusisahau kuona tulikotoka na tulipo. Kuwaona Simba na Yanga kwa pamoja wapo Robo Fainali kwenye michuano Afrika sio jambo dogo. Ni fahari kubwa kwa Taifa letu. Muda si mrefu Azam na Singida Big Stars watakuwa anga hizi.

Tuna kundi kubwa la wachezaji ambao siku hizi wanacheza soka Barani Ulaya. Ni jambo jema sana. Muda si mrefu kufuzu CHAN na AFCON litakuwa ni jambo la kawaida tu kwa Taifa letu. Mpira wetu pamoja na mapungufu yetu yote, naona kila siku tunapiga hatua mbele.

Tukirekebisha mapungufu ya soka letu kwenye uongozi, upendeleo, waamuzi na miundombinu ndani ya miaka 10 ijayo, tutakuwa mbali sana.

SOMA NA HII  MUDATHIR AWEKA SIRI ZA GAMONDI HADHARANI