Home Habari za michezo VITA HII MPYA YAIBUKA YANGA…BACCA AMPASUA KICHWA JOB…ISHU NZIMA IKO HIVI

VITA HII MPYA YAIBUKA YANGA…BACCA AMPASUA KICHWA JOB…ISHU NZIMA IKO HIVI

Habari za Yanga SC

YANGA inaendelea kupasua anga lakini wakati mashabiki wao wakichekelea mafanikio ya ukuta wao ulioruhusu mabao machache pekee kuna vita mpya imeanzishwa kwenye ukuta wao wa mabeki watatu wa kati.

Vita hiyo imeibuka baada ya kuibuka kwa beki wao Ibrahim Abdulla ‘Bacca’ aliyeingia kibabe ndani ya kikosi cha kwanza cha timu hiyo kisha kujimilikisha eneo.

Badaa ya benchi la ufundi la Yanga kumpa nafasi ya kwanza Bacca katika mchezo wake wa ligi Kuu Bara dhidi ya Geita nyumbani wakishinda kwa mabao 3-1, beki huyo akaamsha vita akipangua ukuta huo mpaka kwenye mechi za Kimataifa.

Tayari Bacca ameshaanza kwenye mechi tatu huku mbili kati ya hizo ni zile za Kimataifa za Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya US Monastir Yanga ikishinda kwa mabao 2-0 kisha ile ya TP Mazembe ugenini wakishinda tena kwa bao 1-0.

Jana beki huyo alikuwa tena uwanjani wakati Yanga ikicheza dhidi la Azam Shirikisho (ASFC) dhidi ya Geita lakini sasa itawapasua kichwa makocha wa timu hiyo.

Bacca ana mudu kutumia miguu yote vizuri tangu aingie kwenye kikosi cha kwanza amelazimisha kuupangua ukuta wa muda mrefu wa mabeki wenzake wawili Dickson Job na nahodha wake mkuu Bakari Mwamnyeto.

Mchezo mmoja tu ambao mabeki hao watatu wamecheza pamoja ule dhidi ya TP Mazembe akiwalazimisha makocha wa timu hiyo kumpeleka kulia Job huku yeye akibaki kucheza kati na Mwamnyeto mechi ambayo beki wao wa kulia Djuma Shaban alipumzishwa kufuatia kuwa na kadi mbili za njano wakihofia kama angecheza angeweza kupata kadi na kumkosesha mechi za hatua ya robo fainali.

Faida kubwa ya Bacca imekuwa katika mipira ya juu ambapo katika mchezo dhidi yas Monastir katika mipira ya juu 12 aliruka mara 11 na kufanikiwa kuanza kucheza yeye mpira akiiweka Yanga salama baada ya kuonyesha udhaifu wa mipira ya namna hiyo na kupoteza kwa mabao 2-0 baina ya timu hiyo kwenye mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi ugenini ambao hakucheza.

Mtego wa makocha wa Yanga ni kuamua nani atakuwa katika ukuta wa Yanga katika mechi zinazofuata hasa ile ya Simba na Yanga endapo Djuma atakuwa sawa na mabeki hao watatu wa kati Mwamnyeto, Job na Bacca.

Kocha wa Yanga Nasreddine Nabi amechekelea ujio wa Bacca akisema wala hawana presha yoyote ambapo sasa watakuwa na wigo mpana wa kuchagua nani yuko sawa kulingana na mpinzani wanayekwenda kukutana naye.

Nabi alisema Bacca ameonyesha uimara mkubwa tangu aanze kupewa nafasi ambapo amemtaka sasa kubaki katika muendelezo wa kiwango chake huku akiwataka wenzake nao kuendelea kujipanga sawasawa.

“Sidhani kama kuna changamoto, kazi yetu kama makocha ni kuchagua nani anafaa kuanza katika kikosi cha kwanza tukijiridhisha juu ya uimara wa mchezaji kulingana na mpinzani tunayekwenda kukutana naye, huu ushindani ndio tunaoutaka,”alisema Nabi.

“Unaona sasa tuna wigo mpana wa kuchagua nani wa kuanza pale kwa mabeki wa kati lakini kwangu mimi Bacca amekuja vizuri ameonyesha uwajibikaji mkubwa katika mechi ambazo tumempa nafasi kitu ambacho anatakiwa kukifanya sasa ni kuwa na muendelezo wa kucheza kwa ubora lakini pia hata wengine wenzake nao kubaki katika mstari huo.”

SOMA NA HII  MWANA FA AWEKA WAZI WALICHOCHANGIA SIMBA