Home Habari za michezo YANGA SC WAANZA KUKICHAFUA NIGERIA….MORRISON NA WENZAKE WATOA MSIMAMO…

YANGA SC WAANZA KUKICHAFUA NIGERIA….MORRISON NA WENZAKE WATOA MSIMAMO…

Habari za Yanga SC

YANGA SC imetua na kuanza mazoezi Nigeria kwenye mji wa Uyo ambako mchezo wao utachezwa Jumapili mchana dhidi ya Rivers, lakini mastaa wa Jangwani wametoa msimamo mzito kwamba ushindi ni muhimu na Fiston Mayele amesema yupo fiti.

Yanga SC itachezea kwenye uwanja wa Godwill Akpabio, ambao wenyeji wao Rivers wanaona kama ni faida kwa wapinzani kutokana na ubora wake wa eneo la kuchezea kuelekea mechi hiyo itakayopigwa Jumapili ukiwa ni mchezo wa kwanza wa hatua ya Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Timu hiyo ilitua ardhi ya Nigeria kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Murtala Muhammed jijini Lagos jana saa 6:30 mchana ikitokea Ethiopia ilikounganishia ndege ambapo kikosi hicho kilipumzika mjini hapo kwa usiku mmoja.

Jana jioni, Yanga SC ilifanya mazoezi yake ya kwanza ya kukunjua mwili baada ya safari ndefu ya kutoka jijini Dar es Salaam hapohapo Lagos na kujipanga na hesabu zingine kabla ya leo kuanza safari nyingine fupi itakayotumia saa 1:30, kuelekea mji wa Uyo ambako utachezwa mchezo huo.

Beki wa kulia wa Yanga, Djuma Shaban ‘Soja ya Bemba’, ameliambia Mwanaspoti kuwa kama kuna maumivu makubwa katika mioyo yao ni juu ya matokeo ya kupoteza dhidi ya watani wao Simba lakini wanakwenda kubadilisha upepo kupitia mchezo na Rivers ambao tayari Kocha Nabi Mohammed ameshawasoma.

Djuma ambaye anahusishwa na TP Mazembe, ameongeza kuwa wanajua kila kitu juu ya ubora wa wenyeji wao wakikutana nao mara ya pili ingawa wanafahamu kwamba wana kikosi kipya lakini kwasasa tayari wanawajua juu ya udhaifu wao na ubora wao.

“Tuliwaumiza mashabiki wetu na sisi imetuuma sana kufungwa na Simba lakini hayo yamepita sasa umebaki ujumbe wa kutukumbusha kwamba tunatakiwa kwenda Nigeria kubadilisha yale matokeo ili tuwarudishie furaha watu wetu,”alisema Djuma ambaye ni staa wa zamani wa AS Vita.

“Tumeangalia mechi zao tunajua sasa wapi tupatumie kutengeneza ushindi lakini pia tutaongeza umakini kuhakikisha tunawazuia washambuliaji wao ambao wana ubora ili wasiharibu hesabu zetu.”

Wakati Djuma akiyasema hayo mshambuliaji wa timu hiyo Fiston Mayele aliongeza kuwa wanaiheshimu Rivers, lakini wanatua Nigeria wakiwa na malengo makubwa ya kuuhitaji ushindi kwa vitendo na sio maneno.

“Afya yangu imeimarika baada ya kupata maumivu nitafanya mazoezi kamili na wenzangu, sisi kama wachezaji tumesahau matokeo yaliyopita, tunakwenda kuhakikisha tunashinda huku ugenini, tunajua haitakuwa rahisi lakini hesabu zetu ndio zitakazotupa ushindi,”alisema Mayele ambaye ana mabao mawili hatua ya makundi.

Yanga imeondoka na mziki kamili wa wachezaji 23 tayari kwa mchezo huo wakiwemo makipa watatu Djigui Diarra, Metacha Mnata, Erick Johora wakati mabeki wakiwa Ibrahim Abdulla ‘Bacca’, nahodha mkuu Bakari Mwamnyeto, Dickson Job, Kibwana Shomari, Lomalisa Mutambala, Mamadou Doumbia na Djuma.

Wamo viungo, Zawadi Mauya, Yannick Bangala, Jesus Moloko, Khalid Aucho, Farid Mussa, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Tuisila Kisinda, Stephane Aziz KI, Mudathir Yahya huku washambuliaji wakiwa Mayele, Kennedy Musonda, Bernard Morrison na Clement Mzize.

SOMA NA HII  PROFESA JAY ATEMBELEWA NA KIONGOZI WA SIMBA