Home Habari za michezo SALIM NA CHAMA WAPEWA KAZI MAALUM LEO….MBRAZILI AKESHA NA ONYANGO…

SALIM NA CHAMA WAPEWA KAZI MAALUM LEO….MBRAZILI AKESHA NA ONYANGO…

Habari za Simba SC

KIKOSI cha Simba SC kina dakika 90 za kuhakikisha inazitumia vizuri katika mchezo wa kwanza wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Wydad Casablanca utakaopigwa leo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kabla ya kurudiana Aprili 28 ugenini.

Kocha Mkuu wa Simba SC, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ amekaa na nyota wa timu hiyo, beki wa kati, Joash Onyango na kiungo Clatous Chama ambao amewakabidhi mechi kwa kuwapa funguo za ushindi.

Iko hivi, kutokana na mchango wa Chama kwenye kufunga na kutengeneza nafasi, Robertinho amemtaka kuendeleza kiwango bora huku kwa Onyango akimtaka kuepuka na makosa aliyofanya katika hatua ya makundi.

“Kila mmoja wetu anajua jinsi gani tunahitaji matokeo mazuri, tunapaswa kuongeza umakini mkubwa wakati wa kuzuia na kushambulia kwa kuhakikisha nafasi zetu tunaweza kuzitumia vizuri,”alisema Robertino ambaye beki wake Henock Inonga aliliambia Mwanaspoti jana kwamba; “Mashabiki waje, sisi tutafanya kazi.”

Kocha huyo wa zamani wa Vipers ya Uganda, aliendelea kuwa; “Ilikuwa ni lazima nizungumze na Chama pamoja na kwamba anajua nini cha kufanya, huyu ni mchezaji muhimu kwetu kama walivyo wachezaji wengine kwenye timu.” “Onyango nimezungumza naye ili kumrudisha kwenye hali ya kujiamini huyu ni mchezaji mkubwa kwenye timu hii, siyo hao tu hata wengine nimezungumza nao kwa nyakti tofauti,”aliongeza.

Kuonyesha ubora wa Chama ambaye ni Mzambia, ni kwamba anashika nafasi ya pili kwenye ufungaji bora kwenye Ligi ya Mabingwa ambapo amefunga mabao manne akizidiwa na Hamza Khabba wa Raja Casablanca mwenye matano.

Kwenye mastaa waliohusika katika kufunga na kutoa pasi za mabao, Chama anashika nafasi ya pili akihusika na mabao matano nyuma pia ya Hamza Khabba wa Raja Casablanca ambaye amehusika na sita.

Katika utengenezaji wa nafasi kubwa za kufunga Chama anashika pia nafasi ya pili akiwa amefanya hivyo mara nne nyuma ya staa wa Petro Atletico, Jaredi Lopes Teixeira ambaye ametengeneza tano.

Kiujumla katika utengenezaji wa nafasi Chama anashika nafasi ya tatu akitengeneza mara 15 nyuma ya Jaredi Lopes wa Petro Atletico mwenye 16 huku kinara ni Ahmed Sayed ‘Zizo’ wa Zamalek mwenye 19.

Kwa upande wa Onyango ni kutokana na kuongoza kwa kusababisha penalti nyingi zaidi katika hatua ya makundi akisababisha tatu akifuatiwa na Abdoulaye Camara na Mohamed Kamara wa (Horoya) wenye moja.

Mara ya kwanza kwa timu hizi kukutana ilikuwa ni Mei 28, 2011 katika mchezo wa mchujo kuwania nafasi ya kufuzu hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika ambapo Simba ilifungwa mabao 3-0.

Katika mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Petro Sport uliopo huko jijini Cairo, Simba ilipata nafasi hiyo baada ya kushinda rufaa yake kwa TP Mazembe iliyomtumia kimakosa mchezaji, Besala Bokungu.

SOMA NA HII  MDOGO MDOGO...HIVI NDIVYO AYOUB LAKRED ANAVYOFUTA UFALME WA MANULA MSIMBAZI...