Home Habari za michezo MANULA AFUNGUKA MAPYA YA MOYONI…ADAI HAKUTAKA KUDAKA KABISA……ILA..!!

MANULA AFUNGUKA MAPYA YA MOYONI…ADAI HAKUTAKA KUDAKA KABISA……ILA..!!

Habari za Simba leo

Kipa namba moja wa Klabu ya Simba na Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Aishi Manula amesema kuwa hakuwahi kupenda kuwa kipa badala yake alijikuta akilazimika kufanya hivyo baada ya kukosa namba kwenye nafasi za ndani ya uwanja.

Manula amesema hayo wakati akifanyiwa mahojiano maalum na Millard Ayo akizungumzia historia ya maisha yake ya soka.

“Mpira nilianza kucheza nikiwa darasa la sita baada ya kuanzisha academy yetu pale nyumbani Kilombelo. Mwanzilishi alikuwa mzee mmoja aliitwa Michael Mandevu, tulikuwa uwanjani tukicheza akaja na mipira miwili, akatuita na kutupa tukaanza kucheza.

“Baada ya hapo akatukalisha akasema tunataka tuanzishe timu, tukakubali, akauliza tuipe jina gani tukachagua Serengeti Boys, basi tukaanzia pale. Tuliweka program tukawa tunafanya mazoezi saa nane mchana mpaka saa 10 jioni, wakubwa wakija tunawaachia uwanja, niliendelea hivyo mpaka sekondari.

“Nilianzia kucheza beki namba mbili (beki wa kulia), mtaani kwetu tulikuwa na watoto wengi wanaojua mpira sana, na tulikuwa vijana kama watatu wenye viwango vizuri, tukiwa mtaani kila mmoja alikuwa na timu yake, kwa hiyo kuna nyakati tulikuwa tunaamua kudaka sababu ya uwezo wetu, lakini kama timu yetu ni moja tunaenda kushindana na timu za nje, kuna kaka yetu alikuwa anadaka sisi tunacheza ndani.

“Lakini kuna mwenzetu mmoja alikuwa ananizidi kidogo kwenye kiwango, akawa anapangwa namba mbili mimi nakwenda namba tatu, baadaye kipa wetu alipata changamoto, kocha akauliza mwenye idea ya kudaka nikajitokeza nikijua ni mechi moja tu, akawa ananipanga nikawa nafanya vizuri japo sikupenda. Tukawa tunabishana sitaki kudaka yeye ananilazimisha.

“Hata wale timu ya wakubwa wakataka niwadakie, nakataa, wakasema kama hudaki basi hautakuwa unacheza mimi nikakubali, nikawa nikimaliza mazoezi yangu nakaa nje wao wanacheza, baadaye nikaona acha niendelee kudaka tu taratibu mwisho wa siku nikawa kipa.

“Nilianza kung’aa kwenye mashindano nikiwa kidato cha pili mwaka 2010, tulianza UMISETA ngazi ya shule tukacheza mpaka wilayani, wakati ule ule yakaanza mashindano ya Copa Coca Cola, mwalimu wangu akaniuliza nachagua kwenda wapi, nikajibu Copa Cioca Cola, hivyo nikaondolewa jina langu UMISETA kwenda Mkoani pale Morogoro.

“Nikawa miongoni mwa watu waliochaguliwa Copa Coca Cola ambapo tulikuja Kibaha, japo kwa mwaka wa kwanza tulitoka robo fainali, nikarudi Kilombelo.

“Mwaka 2011 nilichaguliwa tena, tukafika mpaka fainali na timu yetu ya Copa Coca Cola Kilombelo lakini bahati mbaya tulifungwa na mkoa wa Kigoma ndipo nilipochaguliwa kujiunga na Academy ya Azam FC na tayari nilikuwa nimechaguliwa Timu ya Taifa na Kocha Kim Paulsen.

“Kujiunga na Azam FC ilikuwa ni jambo kubwa sana kwangu wala sio pesa nitakayopata, nilimwambia mama na alifurahi sana kwamba ule mzigo wa kusomesha umepungua kwa sababu baba alikuwa ameshafariki na tulikuwa na maisha magumu kijijini,” amesema Aidhi Manula.

SOMA NA HII  SIMBA DAY YA MSIMU HUU USIPIMEEH...MABINGWA WA AFRIKA KUTUA NCHINI KUKIPIGA SIKU HIO