Home Habari za michezo AHMED ALLY:- HATUKO TAYARI KUONA MASHABIKI WAKIZIDI KUTESEKA…LAZIMA TUTIBU TATIZO..

AHMED ALLY:- HATUKO TAYARI KUONA MASHABIKI WAKIZIDI KUTESEKA…LAZIMA TUTIBU TATIZO..

Mashabiki Simba

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba, Ahmed Ally amesema kuwa uongozi wa klabu hauko tayari kuona mashabiki wa timu hiyo wakiteseka na kulia kwa kukosa mataji badala yake wanakwenda kuyafanyia kazi mapungufu yao ili kurejea wakiwa bora zaidi msimu ujao.

Ahmed amesema hayo mara baada ya kumalizika kwa mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam dhidi ya Azam FC, mkoani Mtwara ambapo Azam waliibuka na ushindi wa bao 2-1 dhidi ya Simba na kufanikiwa kutinga hatua ya fainali ya michuano hiyo.

“Sisi kama simba tunakiri kuwa, msimu wa 2022/23 tumaumaliza rasmi hii leo, lakini lazima kazi ianze sasa, kila mtu kwenye idara yake ndani ya Simba aangalie tunakosea wapi ili msimu ujao tufanye vizuri.

“Tukisema twende hivi hivi tutakuwa tunafuga tatizo litakalotutesa msimu ujao. Lazima twende tukatibu hilo tatizo.

“Hatuwezi kila siku kuendelea kuwaliza na kuwaumiza mioyo mashabiki zetu, hatuwezi kuendelea na maisha hayo, lazima tufanye tathmini ya kina kuanzia wachezaji wote mpaka benchi la ufundi bila kuangalia jina huyu ni nani,” amesema Ahmed.

Mpaka sasa unaweza kusema Simba imekosa mataji yote msimu huu, kwani wametolewa Ligi ya Mabingwa Afrika kwenye hatua ya robo fainali, Kombe la Shirikisho la Azam wametolewa, ngao ya jamii wamekosa, Mapinduzi Cup wamekosa na hata ubingwa wa Ligi, Yanga ndiyo inaonongoza huku ikihitaji mchezo mmoja tu kutangaza ubingwa kati ya mitatu iliyosalia kutamatika kwa ligi.

SOMA NA HII  SAIDO ABAKIZA SIKU 40 KUENDELEA KUKIPIGA YANGA...UONGOZI WAMCHUNIA..SENZO AFUNGUKA HAYA...