Home Habari za michezo MASTAA YANGA KULAMBA POSHO ZA KIMADRID WAKIBEBA UBINGWA WA CAF…KAZI INAANZA KESHO…

MASTAA YANGA KULAMBA POSHO ZA KIMADRID WAKIBEBA UBINGWA WA CAF…KAZI INAANZA KESHO…

Habari za Yanga SC

Mastaa Yanga huenda wakageuka mamilionea kama watatwaa kombe la Shirikisho Afrika msimu huu kwani uongozi wa timu hiyo unampango wa kuwapa asilimia 40 za pesa ya ubingwa huo ambayo ni karibu sh 2 bilioni za Kitanzania ambapo ukigawa kwa wachezaji 30 kila mmoja atachota milioni 60.

Yanga imefuzu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza msimu huu baada ya kuitoa Marumo Gallants ya Afrika Kusini kwa jumla ya mabao 4-1, na katika fainali itakutana na USM Alger kutoka Algeria katika mechi mbili za nyumbani na ugenini na mshindi wa jumla atakuwa bingwa na kukabidhiwa Kombe pamoja na kitita cha pesa sh 4.7, bilioni za Kitanzania.

Moja ya viongozi wa timu hiyo, (jina tunalo) alilithibitishia kuwa uongozi pamoja na mfadhili wa timu hiyo, Gharib Said tayari wameanza kuzipigia hesabu pesa za ubingwa huo ambazo ni sh 4.7 bilioni, na moja ya maeneo waliyoweka kwenye mpango wao ni kuwapa bonasi isiyozidi asilimia 40 za pesa hiyo wachezaji kama zawadi ya kutwaa ubingwa huo na kuweka historia ya kuwa klabu ya kwanza Tanzania kubeba ubingwa wa Afrika.

“Mwanzo tulikuwa na malengo ya kufika robo fainali lakini kwa ubora wa kikosi chetu tumefika fainali. Ni jambo la kuwapongeza zaidi wachezaji wetu kwa kujitoa na kupambana hadi tulipo sasa.

“Huwezi kuamini kwa sasa tumepanga kubeba ubingwa huu na kila mmoja wetu anajua hilo kwani tutaweka historia na heshima kwetu na taifa kwa ujumla na kubwa zaidi tutapata fedha ambazo tutazitumia katika matumizi ya kawaida ya klabu ila kubwa zaidi tutawapa wachezaji kiasi kisichozidi asilimia 40 kama bonasi kwa kazi kubwa waliyofanya,” kilieleza chanzo chetu.

Kwa hesabu za kawaida, asilimia 40 ya sh 4.7 Bilioni ni takribani sh 1.9 bilioni hadi sh 2 bilioni hivyo huo ndio mkwanja watakaoupata mastaa wa Yanga kama watatwaa ubingwa huo.

Kwa ujumla wa wachezaji wa Yanga, wanaocheza na hata wale wasiocheza lakini wamesajiliwa kwenye makabrasha yaliyoko katika ofisi za shirikisho la Soka Tanzania (TFF), wapo 30.

Hivyo ukichukua sh 1.9 bilioni ambayo ni asilimia 40 ya sh 4.7 bilioni ambazo huenda wakapata kama watatwaa ubingwa ni wastani wa kila mchezaji kukunja zaidi ya milioni 63.

Lakini mkwanja huo kama ilivyo kawaida kwa Yanga kugawa bonasi kutokana na ushiriki wa wachezaji kwa kuzingatia waliocheza mechi nyingi, walioisaidia zaidi timu na mambo mengine basi huenda kukawa na ambao watapata zaidi ya sh 63 milioni na wengine watakuwa pungufu ya hapo.

Hapo bado haujaweka bonasi nyingine zikiwemo zile za kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu, bonasi kutoka kwa wadhamini wa timu hiyo na kama kama itabeba kombe la TFF (ASFC), ambalo imeingia fainali na Azam FC.

Yanga imeendelea kupiga tizi kwa usiri zaidi katika kambi yake iliyoko Avic Town Kigamboni ikijiandaa na mechi ya kwanza ya fainali dhidi ya USM Alger itakayopigwa keshokutwa Jumapili kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Kocha Mkuu wa timu hiyo, Nasreddine Nabi anaamini utakuwa ni mchezo mgumu lakini wanaendelea kujipanga ili kushinda nyumbani kabla ya marudiano ugenini, Juni 3, mwaka huu.

“Haitakuwa mechi rahisi lakini tunajipanga kushinda, tunaendelea na maandalizi na tunaamini tutafanya vizuri,” alisema Nabi.

SOMA NA HII  KUMBE PACOME ALIMLILIA GAMONDI KABLA YA DABI...BOSS YANGA AFUNGUKA ISHU NZIMA A-Z