Home Habari za michezo KUELEKEA USAJILI MPYA…MBRAZILI SIMBA ANOA PANGA…AWAPA MABOSI MSIMAMO WAKE…

KUELEKEA USAJILI MPYA…MBRAZILI SIMBA ANOA PANGA…AWAPA MABOSI MSIMAMO WAKE…

Habari za Simba SC

Wakati Uongozi wa Simba SC ukijizatiti kuwa na kikosi bora kwa msimu ujao wa 2023/24, Kocha Mkuu wa klabu hiyo ya Msimbazi Roberto Oliviera ‘Robertinho’ amesema atafanya mapinduzi makubwa katika mchakato wa usajili kwa ajili ya kuboresha kikosi chake.

Robertinho amesema wanajua walipokosea na wanafanya tathmini ya kila idara ili warekebishe makosa na kujenga kikosi imara kitakachowapa mafanikio.

Robertinho amesema kwa msimu huu kila mmoja ndani ya Simba SC ametimiza wajibu wake kwa kiasi kikubwa, kilichotokea ni matokeo ya mpira.

“Ni mapema kusema nani na nani tutasajili lakini nimepanga kufanya mabadiliko makubwa. Nafanya kazi kwa misingi ya taaluma yangu, kama unavyojua soka ni mchezo wa wazi, nitaendelea kuwa na kundi la wachezaji ambao wanajituma na kufanya kazi kwa moyo mmoja,” amesema Robertinho

Ameongeza tayari mapendekezo ya awali ameshayapeleka kwa mabosi wa klabu hiyo na anaimani yatafanyiwa kazi kwa wakati kwa sababu wanataka kuingia msimu mpya wakiwa bora zaidi.

Wakati huo huo Kocha huyo kutoka nchini Brazil ameanza maandalizi ya mchezo wa Mzunguuko wa 29 wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Polisi Tanzania utakaopigwa mwishoni mwa juma hili jijini Dar es salaam.

Simba SC ambayo tayari imeshajihakikishia kukosa taji msimu huu 2022/23, baada ya watani zao Young Africans kutwaa Ubingwa wa Tanzania Bara mwishoni mwa juma lililopita, imeanza maandalizi ya mchezo dhidi ya Polisi Tanzania tangu jana Jumatano (Mei 17), katika Uwanja wa Mo Simba Arena uliopo Bunju, Dar es salaam.

SOMA NA HII  KIUNGO MPYA SIMBA AMALIZA LIGI YA GHANA KWA MKOSI...SIKU YA KUTAMBULISHWA MSIMBAZI YATAJWA...