Home Habari za michezo KUHUSU USAJILI SIMBA….MBRAZILI KAANZA NA HAWA KWANZA….’KIBERENGE’ CHA GEITA GOLD NDANI…

KUHUSU USAJILI SIMBA….MBRAZILI KAANZA NA HAWA KWANZA….’KIBERENGE’ CHA GEITA GOLD NDANI…

Tetesi za Usajili Simba

Klabu ya Simba imeanza harakati za kuimarisha kikosi chake na miongoni mwa nyota wanaotajwa kuwa katika mpango wa kuwanasa ni winga wa Geita Gold, Edmund John.

Habari za uhakika kutoka ndani ya Klabu hiyo zinasema tayari winga huyo mwenye umri wa miaka 20 ameanza mazungumzo na Uongozi wa Simba SC kwa ajili ya kujiunga nao msimu ujao.

Nyota huyo wa zamani wa Serengeti Boys, anamudu kucheza nafasi za winga zote mbili kulia na kushoto pia ana uwezo wa kucheza nafasi ya nyuma ya mshambuliaji.

Harakati za kumsajili Edmund zimeanza kutokana na mapendekezo ya Kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’ ambaye katika ripoti yake ameutaka uongozi kusajili mawinga wawili wazawa wanaomudu kucheza kila upande.

“Mazungumzo yanaendelea baina ya Simba SC na mchezaji na yanakaribia kufikia pazuri. Tunafahamu ana mkataba na Geita Gold hadi Januari mwakani lakini tunaweza kuzungumza nao na tukafikia mwafaka wala hakuna shida katika hilo.”

“Kocha amependekeza tusajili mawinga wawili wazawa ambao wataleta ushindani kwa wageni na huyu Edmund ni miongoni mwa wachezaji wa nafasi hiyo walioonyesha kiwango kizuri msimu huu,” amesema mmoja wa vigogo wa Simba SC

Licha ya kucheza nafasi ya winga, Edmund ni miongoni mwa wachezaji wa nafasi hiyo walioonyesha uwezo wa kufumania nyavu msimu huu ambapo hadi sasa ameifungia timu yake mabao manne dhidi ya Tanzania Prisons, Dodoma Jiji, Polisi Tanzania na Coastal 3 Union.

Wakati ikiwa katika mpango wa kumnasa winga huyo, Simba SC pia iko katika mpango wa kumwongezea mkataba winga wake kiraka Jimmyson Mwanuke ambaye mkataba wake wa miaka mitatu utafikia tamati mwishoni mwa msimu ujao.

Uwezo mkubwa wa Mwanuke kucheza nafasi tofauti uwanjani pamoja na nidhamu anayoonyesha vinatajwa kama sababu iliyomshawishi Robertinho kufanya maamuzi ya kuendelea kubaki na nyota huyo aliyesajiliwa kutokea Gwambina FC msimu uliopita 2021/22.

Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amesema timu yake haijafanya mchakato wa usajili wa Edmund na suala la Mwanuke kama lipo au halipo litatolewa ufafanuzi.

“Taarifa kuhusu Simba SC kumhitaji Edmund sisi wenyewe tunaziona tu kwenye mitandao ya kijamii na vyombo habari, kuhusu Mwanuke kama kuna chochote klabu itatoa taarifa,” amesema Ahmed Ally

SOMA NA HII  ANALIPWA BIL 2 KWA TANGAZO MOJA