Home Habari za michezo JINSI WAARABU WANAVYOLIHAMISHA SOKA KWAO….MESSI KAWACHOMOLEA NNJE MAPEMA TU..

JINSI WAARABU WANAVYOLIHAMISHA SOKA KWAO….MESSI KAWACHOMOLEA NNJE MAPEMA TU..

Habari za Michezo

“Kila mwanasoka au kila mtu ambaye anafanya kazi anataka kupata pesa kwa ajili ya kusaidia familia yake. Nimetoka katika familia maskini sana. Hatukuwa na chochote. Haya ni matunda ya kazi yangu na kama napata pesa hizi ni kwa sababu nimezitafuta. Kama nilivyokuja hapa basi ndivyo ninavyoweza kurudi Ulaya.”

Nyota wa Kibrazili aitwaye Oscar, alikuwa akizungumza hivi Januari 2017 wakati alipokamilisha uhamisho wake wa kushangaza kutoka Chelsea kwenda Shanghai Port ya China. Aliufungua moyo wake. kitu gani bora zaidi kuliko pesa?

Mbele ya waandishi wa habari pale Shanghai, China Oscar alijikuta akiongea maneno haya bila ya unafiki. Wanasoka wengine huwa wanajaribu kuficha, lakini Oscar aliamua kuufungua moyo wake. hakutaka kuwa mnafiki.

Oscar alikuwa na miaka 28 tu. Alikuwa wa moto kweli kweli. Hata hivyo pesa zilimteka na hakutaka kuficha. Wachina waliamua kumlipa kiasi cha Pauni 400,000 kwa wiki na ghafla Oscar akawa mmoja kati ya wachezaji wanaolipwa pesa nyingi zaidi duniani. Ilikuwa ghafla mno.

Wakati huo Wachina walikuwa katika ubora wao wa kumwaga noti. Nasikia mradi wao ulifeli. Sijui kwanini. Lakini sasa mradi kama huo umehamia kwa Waarabu. Wameanza kutusumbua katika mpira kwa kiasi kikubwa na sasa wanatia hofu.

Waarabu wana mambo mawili yanayotisha. Kwanza walianza kwa kununua timu Ulaya, lakini wanapeleka wachezaji wenye majina makubwa kwao. Hasa Waarabu hawa wa Saudi Arabia. Watatuua. Ofa wanazotoa kwa wachezaji zinawafanya wachezaji waingie katika mkumbo wa Oscar.

Hawatasema kama Oscar. Watakuwa wanafiki. Lakini mwisho wa siku hawalazimiki kusema kwa sababu kiasi cha pesa ambacho kinawapeleka Riyadh kinachanganya akili zetu. Ni kiasi ambacho hauwezi kukataa hasa kama umetimiza miaka 30 wakati ukicheza Ulaya.

Na sasa noti hizi zimemnasa rafiki yetu Karim Benzema. Bado alikuwa na miguu yenye nguvu kuweza kuendelea kutamba Ulaya, lakini ameamua kwenda zake Riyadh kwenda kuoga noti za Waarabu. Desemba mwaka huu atatimiza miaka 36.

Benzema atalipwa kiasi cha Pauni 173 Milioni kwa msimu mmoja katika mkataba wake wa miaka mitatu pale Saudia. Hili ni ongezeko mara 12 ya pesa alizokuwa analipwa Madrid. Alikuwa analipwa Pauni 14 milioni tu. Hazikuwa pesa haba lakini klabu ya Al-Ittihad imemtoa kutoka kuwa tajiri hadi kuwa tajiri aliyepitiliza.

Maisha yanataka nini zaidi kwa mtu aliyeshinda karibu kila taji ambalo alishiriki duniani. Angesubiri nini zaidi Santiago Bernabeu, wakati tayari alikuwa ameshinda mataji 25 klabuni hapo ikiwemo mataji mengi ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya.

Ilikuwa lazima afuate nyayo za rafiki yake Cristiano Ronaldo, ambaye naye aliamua kuchukua mkondo huu baada ya kushinda kila kitu pale Ulaya. Pesa ambazo Waarabu waliamua kumlipa ni kufuru na asingeweza kukubali kuendelea kudhalilisha barani Ulaya.

Mhanga mwingine wa noti hizi ni yule rafiki yetu mfupi N’Golo Kante wa pale Stamford Bridge. Wasaudia wanataka kumpeleka kwao na tayari ameshafuzu vipimo vya afya katika klabu ya Al-Attihad ambapo anakwenda kuungana na Benzema.

Waarabu wamemtengea Kane mshahara wa Pauni 100 milioni kwa mwaka. Maisha yanataka nini zaidi? Wote tunajua kwamba Kante ni kijana mpole, muungwana asiye na makuu, lakini linapokuja suala la pesa kama hizi wote tunamsamehe.

Ameshinda karibu kila taji alilowahi kujaribu kuwania katika soka. Ameshinda hadi kombe la dunia. Machi 29 mwakani atatimiza miaka 33. Kuna sababu gani za msingi ambazo zitasababisha asichukue pesa hizi za Waarabu kwa sasa.

Kama Oscar aliondoka akiwa na miaka 28 huku akiwa hajashinda mataji mengi Ulaya, vipi kuhusu Kante? Tunamdai nini hasa kiasi cha kumlaumu kwa kukimbilia pesa za Waarabu. Nadhani ni haki yake. ni wakati wa kumpigia makofi zaidi kuliko kumlaumu.

Mchezaji ambaye katika namna ya kushangaza alizikwepa noti hizi ni Lionel Messi. Klabu ya Al-Hilal walikuwa wanataka kufanya kufuru kwa kumlipa Messi kiasi cha Euro 500 Milioni kwa msimu mmoja wa soka. Kwa miaka mitatu wangemlipa kiasi cha Euro 1.5 Bilioni.

Hadi leo sielewi kwanini Messi ameamua kuzikwepa pesa hizi na kwenda zake Marekani katika klabu ya David Beckham. Inadaiwa kwamba kuna kampuni zitampa hisa zao wakati anacheza huko, lakini bado nashindwa kuelewa ukichaa uliompata akakimbia noti hizi.

Inadaiwa kuna sababu mbalimbali za Waarabu kumwaga noti hizi. Waarabu wa Saudia wanaamini kwamba mastaa hawa watawasaidia katika kampeni za kuandaa Kombe la Dunia mwaka 2030. Baada ya matusi ambayo tumeyaona Doha sasa hivi tunatazamia matusi mengine kutoka Saudia.

Ukweli ulio wazi ni kwamba pesa hizi wanazowapa kina Ronaldo na Benzema haziwezi kurudi kwa sababu za kibiashara. Hawana shida na pesa za viingilio wala mauzo ya jezi. Mchezaji kama Ronaldo kwa sasa anacheza katika uwanja ambao unachukua mashabiki 25,000 tu.

Lakini angalia mauzo ya jezi. Klabu yake ni maarufu duniani kiasi cha kuuza jezi nyingi za kurudisha mauzo ya jezi? Sio kweli. Jezi Ligi yao inaweza kuuza ving’amuzi vingi duniani? Sio kweli. Kwa mfano, katika timu ya Ronaldo mchezaji tunayemfahamu ni Ronaldo tu peke yake. kwanini tusumbuke kutazama kuitazama ligi yao? Sio sawa.

Hofu yangu kwa Waarabu kwa sasa ni kwamba wanaweza kurudi kwa wachezaji wenye umri mdogo kama kina Marcus Rashford, Martin Odegaard, Vinicius Junior, Bukayo Saka na wengineo. Usidhani kwamba na wao hawatamani pesa za kina Ronaldo.

Walau wenzetu waliozaliwa Ulaya kuna ndoto wanataka kuzitimiza kabla ya kuchukua noti hizi, lakini usiamini kwamba kila mmoja ana ndoto hizi. Wengine wanaweza kuwa na mawazo tofauti. Wapo wanaotaka kumiliki ndege zao binafsi mapema iwezekanavyo.

SOMA NA HII  AHMED ALLY AWACHARUKIA MASHABIKI WA YANGA WALIOWAPOKEA RS BERKANE JANA...ATOA POVU HILI...