Home Habari za michezo BEKI MPYA WA SIMBA AFUNGUKA MAZITO

BEKI MPYA WA SIMBA AFUNGUKA MAZITO

Tetesi za Usajili Simba SC

SIMBA imekwea jana kwenda Uturuki kuweka kambi ya mazoezi ya siku kadhaa. Watakuwa kwenye ardhi ya nchi moja na Hull City ya England. Lakini yenyewe tayari imeshafika huko.

Lakini sasa beki mpya wa Simba, Che Malone Fondoh (24), kutokea Coton Sport ya Cameroon amewaambia mashabiki wakae mkao wa kunenepa. Mambo mazuri yanakuja kuanzia mwezi ujao.

Staa huyo aliyepewa mkataba wa miaka miwili akitabiriwa kusimama na Henock Inonga pale nyuma, ameliambia Mwanaspoti kuwa yupo Simba kwaajili ya kuwapa furaha, makombe na heshima mashabiki na wapenzi wa timu hiyo.

Malone aliyekuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Cameroon kwa msimu uliopita ni miongoni mwa wachezaji wapya walioikamua mkwaja mrefu Simba kwani ililazimika kuvunja mkataba ili kumpata kutokana na umahiri wake.

Akipiga stori na Mwanaspoti ameeleza furaha yake kujiunga na Simba huku akiweka wazi ana deni la kuwapa mafanikio wanachama na mashabiki wa Simba.

“Nafurahi kujiunga na Simba, ni timu kubwa inayofanya vizuri kwenye michuano ya Afrika. Ninapaswa kujituma na kufanya vizuri zaidi ili nisiwaangushe bali kuwaheshimisha,” alisema Malone akipania zaidi kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika inayoanza Agosti 18.

Beki huyo alisema anaamini umoja, kujituma na ubora wa kikosi kizima ndio utaifanya Simba kuwa tishio zaidi kwa msimu ujao na tayari ameshafuatilia asilimia kubwa ya wachezaji wa kikosi cha sasa anaelewa nini cha kufanya Msimbazi kwavile mpira wa Afrika hautofautiani.

“Simba ina wachezaji wengi bora na wazuri, kwa kushirikiana nao tunaweza kufanya vizuri zaidi na kufikia malengo, naamini umoja, kujituma na kupambana zaidi itatufanya tufike juu zaidi,” alisema Malone aliyewahi pia kuzichezea timu za taifa za vijana za Cameroon.

Sambamba na Malone hadi Sasa Simba imetambulisha wachezaji wengine wapya wa kigeni, Mshambuliaji Mcameroon Willy Onana aliyeibuka mfungaji bora na mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Rwanda akiichezea Rayon Sports na Winga Muivory Coast Aubin Kramo kutokea Asec Mimosac.

Kwa upande wa kocha mkuu wa kikosi hicho, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ alisema Malone na wachezaji wengine waliosajiliwa wataongeza ubora kwenye kikosi chake.

“Usajili tulioufanya ni katika maeneo ambayo tulihitaji watu wa kazi, naamini ujio wa wachezaji hawa utakuja kuongeza ushindani na ubora kikosini na hilo litatufanya kufikia malengo,” alisema Robertinho.

Simba imesafiri kwenda nchini Uturuki kwaajili ya maandalizi ya msimu mpya ‘Pre Season’ ambapo itajichimbia huko kwa karibu wiki tatu ikijifua kabla ya kurejea mwanzoni mwa mwenzi ujao kuanza mikiki mikiki ya mashindano.

Tayari Hull City iko Instanbul ikijinoa na timu nyingine kibao za Ulaya za madaraja mbalimbali hupendelea kuweka kambi Uturuki kutokana na miundombinu rafiki ambayo mingi iko hapohapo kwenye eneo la hoteli.

SOMA NA HII  REKODI ZA GOMES NDANI YA LIGI KUU BARA HIZI HAPA