Home Habari za michezo GAMONDI AFANYA MAAMUZI MAGUMU KWENYE KIKOSI CHA YANGA, MAYELE ATAJWA

GAMONDI AFANYA MAAMUZI MAGUMU KWENYE KIKOSI CHA YANGA, MAYELE ATAJWA

Habari za Yanga SC

KOCHA mpya wa Yanga, Miguel Angel Gamondi, kwa sasa yupo AVIC Town, Kigamboni, Dar, akikisuka kikosi cha timu hiyo, huku taarifa zikibainisha kwamba, Muargentina huyo anatengeneza kikosi ambacho kitafanya vizuri bila kumtegema mshambuliaji mmoja kama ilivyokuwa msimu uliopita.

Ikumbukwe kuwa, wakati Yanga ikifanya vizuri msimu uliopita 2022/23 kwa kushinda mataji yote ya ndani na kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika chini ya Kocha Nasreddine Nabi, ilikuwa ikimtegemea zaidi Fiston Mayele kufunga mabao.

Kuelekea msimu ujao 2023/24, Yanga inaanza maisha mapya bila ya Nabi wala Mayele ambaye amejiunga na Pyramids ya Misri.

Taarifa kutoka katika Kambi ya Yanga iliyopo AVIC Town, zinasema kwamba, Kocha Gamondi ameanza kuisuka timu hiyo kucheza bila ya kumtegemea mshambuliaji wa kati kufunga mabao na badala yake watu wote wanaocheza eneo la ushambuliaji kufunga mabao ya kutosha.

“Kocha Gamondi anaisuka Yanga imara sana kwa ajili ya msimu ujao, ambacho anakifanya kwa sasa ni kuhakikisha anaifanya timu ya msimu ujao inakuwa tishio zaidi hasa kwa kuwafanya wale wachezaji wote wanaocheza eneo la mbele wawe na uwezo mkubwa wa kufunga mabao.

“Kocha hataki timu iwe inategemea mchezaji moja tu kufunga mabao kwani anafahamu kwamba inaweza kutokea siku akabanwa na wapinzani, wakashindwa kupata matokeo mazuri.

“Kutokana na hilo, kina Maxi Mpia, Pacome Zouzoa, Aziz KI na Jesus Moloko wamekuwa wakipewa mbinu na mazoezi maalumu ili wawe na uwezo mkubwa wa kufunga mabao,” kilisema chanzo hicho.

Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe, amesema: “Watu wasiwe na mashaka na Yanga ya msimu ujao kwani tunaamini tutaendelea pale ambapo tumemaliza msimu uliopita na kikubwa watu wanatakiwa kumuachia mwali yeye ndiye anaiandaa Yanga bora zaidi na zaidi.”

SOMA NA HII  KISA KUHOJI HOJI SANA KUHUSU BIL 20 ZA MO DEWJI...SIMBA WAMSHUKIA JUMLA JUMLA DK KIGWANGALLA...