Home Uncategorized KIPA KMC NA SIMBA KIMEELEWEKA….KOCHA KMC AANIKA KILA KITU

KIPA KMC NA SIMBA KIMEELEWEKA….KOCHA KMC AANIKA KILA KITU

LICHA ya Simba kuwa kimya katika harakati za usajili, tetesi zilipo ni kwamba tayari wamemalizana na kipa wa KMC, Jonathan Nahimana.

Nahimana alianza kuhusishwa na Simba hasa bada ya kuweka wazi kuwa anaipenda timu hiyo kuliko nyingine zilizopo Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kitendo cha nyota huyo ambaye pia anayefukuziwa na Azam FC, kutaja mambo yanayomvutia Simba, ikiwamo malipo ya mshahara kwa wakati, kiliibua gumzo ndani ya klabu yake.

Kipa huyo raia wa Burundi aliyedumu katika kikosi cha KMC kwa misimu miwili akionesha kiwango kikubwa hadi kuitwa timu ya Taifa ya nchini kwao, anamaliza mkataba wake KMC mwisho wa msimu huu.

Kwa mujibu wa taarifa ilizozipata gazeti la BINGWA jana, jeuri ya kipa huyo inatokana na kusaini mkataba wa awali na Wanamsimbazi hao wa miaka miwili.

“Nahimana anajiamini kutokana na kiwango chake na ndio sababu alisema vile, pia karibia timu kubwa zote hapa nchini zinamtaka, lakini naona Simba ndio wamefika pazuri kwa kusaini mkataba wa awali,” alisema mtoa habari huyo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.

Gazeti la BINGWA jana lilimtafuta Nahimana, lakini hakutaka kuzungumzia suala hilo na kusema bado yupo na KMC na kwamba iwapo kuna timu atakwenda, itajulikana baadaye.

Hata hivyo, Kocha wa KMC, Hererimana Haruna, alisema anasikia taarifa za mchezaji huyo kuondoka mwisho wa msimu, hivyo ameanza harakati za kutafuta mrithi wake.

“Nahimana aende pale anapohitaji, mechi za ligi zikianza nitaangalia kipa anayeweza kuchukua nafasi yake, hakuna kumzuia mchezaji, wachezaji wengi wanatamani timu kubwa,” alisema.

SOMA NA HII  NYOTA MPYA SIMBA AOMBA KUONDOKA BAADA YA MAMBO KUWA MAGUMU