Home Habari za michezo JUMA MGUNDA KITI CHA MOTO SIMBA……UONGOZI WATIA NENO

JUMA MGUNDA KITI CHA MOTO SIMBA……UONGOZI WATIA NENO

Kocha Msaidizi Simba SC

Wakati msafara wa Simba ukiondoka juzi kuelekea Uturuki ambako utaweka kambi ya siku 20 kujiandaa na msimu mpya, hatima ya kocha msaidizi Juma Mgunda iko kwenye mabano baada ya kushindwa kusafiri na timu hiyo.

Juma Mgunda hakuonekana katika msafara ulipokuwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, huku kocha mkuu Robert Oliveira ‘Robertinho’, akiondoka na kocha msaidizi namba moja, Ouanane Sellami, meneja mpya wa timu hiyo Mikael Igendia, kocha mpya wa viungo Corneille Hategekimana na kocha wa makipa Daniel Cadena.

Kabla ya msafara huo kupaa, mratibu wa mratbu wa klabu hiyo Abbas Ally aliwatoa wasiwasi mashabiki wa Simba akidai kundi lingine litaungana na kikosi, siku tatu baadaye huko Uturuki.

“Huu ni masafara wa kwanza lakini wapo wachezaji wengine ambao wataungana na kikosi huko huko Uturuki na wengine watatokea hapa, usajili bado unaendelea,”alisema Abbas ambaye ameongozana na timu hiyo.

Hata hivyo licha ya uongozi wa Simba pamoja na Mgunda mwenyewe kutokuwa tayari kuzungumzia kukosekana kwake habari kutoka kwa chanzo cha uhakika ndani ya timu hiyo zimefichua kuwa ipo katika hatua za mwisho za kuachana na kocha huyo wa zamani wa Coastal Union.

“Kuna uwezekano mdogo wa kuendelea kusalia na kocha Juma Mgunda. Kwa sasa uongozi upo katika mazungumzo ya kukamilisha baadhi ya mambo kabla haujamuaga rasmi. Ameitumikia vizuri timu yetu hivyuo hatutaki kuachana naye vibaya,” kilifichua chanzo hicho.

Juhudi za kuutafuta uongozi wa Simba pamoja na Mgunda ziligonga mwamba kutokana na simu zao kuita bila kupokelewa ingawa kabla timu hiyo haijakwea pipa jana, kocha Robertinho alisema kuwa anaenda Uturuki na benchi la ufundi lililokamilika.

“Tunaenda kambini na benchi la ufundi lililokamilika na jambo la kufurahisha wote wana leseni ya ukocha daraja A. Wana uzeofu wa soka la Afrika na ni makocha wakubwa. Nadhani ni jambo chanya. Malengo yetu ni kucheza vizuri, kushinda mechi na kwa nini isiwekane tukawa mabingwa?

“Tunakwenda kupata kambi yenye utulivu ambayo tutaitumia kutengeneza muunganiko wa kikosi kamili kwa hawa wachezaji wapya waliokuja na wale wa zamani ambao tuliobaki nao, tunahitaji kwenda kujiandaa vizuri ili tuwe na ubora wa kuja kushindana kwa ubora wa jina la Simba na baadaye tupate mataji, hili linawezekana,”alisema Robertinho

Ukiondoa Mgunda, nyota wapya wawili watatu wa kigeni wa timu hiyo, Willy Onana, Che Fondoh Malone na Aubin Kramo walishindwa kusafiri na msafara huo kwa kile kinachotajwa kuwa ni kuchelewa kupata viza ya kuingilia Uturuki kama ilivyo kwa Jean Baleke, Pape Osmane Sakho ambaye bado hajarejea nchini kutokea Senegal alikoenda mapumzikoni.

Wachezaji waliondoka jana ni makipa Ally Salim na Feruzi Teru, mabeki wakiwa Shomari Kapombe, David Kameta ‘Duchu’, Israel Mwenda, Mohamed Hussein ‘Tshabalala, Kennedy Juma,Henock Inonga, viungo wakiwa Sadio Kanoute, Jimson Mwanuke, Said Ntibazonkiza, Kibu Denis, Peter Banda huku washambuliaji wakiwa Mosses Phiri, John Bocco na Mohamed Mussa.

Mgunda alijiunga na Simba, Septemba mwaka jana kukaimu kwa muda nafasi ya kocha mkuu baada ya timu hiyo kuachana na Zoran Maki kabla ya baadaye kubadilishiwa majukumu na kupewa nafasi ya kocha msaidizi baada ya kutua kwa Robertinho.

Katika kipindi alichoiongoza Simba akikaimu nafasi ya ukocha mkuu, timu hiyo ilicheza mechi 21, ikipata ushindi katika mechi 16, ikapata sare nne na kupoteza mchezo mmoja.

SOMA NA HII  AZIZI KI NDO BASI TENA YANGA, MWAMBA HUYU HAPA KACHUKUA NAMBA YAKE, KOCHA AWEKA WAZI