Home Habari za michezo KOCHA WA SIMBA AUNGANA NA WACHEZAJI WAKE KAMBINI UTURUKI, AJA NA JAMBO...

KOCHA WA SIMBA AUNGANA NA WACHEZAJI WAKE KAMBINI UTURUKI, AJA NA JAMBO HILI, ONANA ATAJWA

Habari za Simba SC

KOCHA Mkuu wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ tayari amerejea kambini kwa chama hilo nchini Uturuki akitokea kwenye kozi fupi iliyofanyika Brazil huku akitua na faili la mastaa wapya akiwemo Luis Miquissone na Willy Onana.

Robertinho hakuwa kambini kwa siku saba zilizopita kutokana na kuwa moja ya wakufunzi wa kozi maalumu iliyoandaliwa na chama cha soka Brazil lakini kwa Simba hakuna kilichoharibika kwani programu zote alimuachia kocha msaidizi Mtunisia Sellami Ouannane aliyesimamia timu katika kipindi chote hicho.

Akizungumza na Mwanaspoti baada ya kutua kambini, Robertinho alisema kazi ya kwanza atakayoifanya katika kipindi kilichobaki cha maandalizi ya msimu mpya ni kutengeneza muunganiko wa timu kwa kuwa ana wachezaji wengi wageni.

Mbrazil huyo alisema anataka kuhakikisha mastaa wapya wote walioingia kwenye dirisha hili la usajili wanaingia kwenye mifumo na kutengeneza timu yenye uwiano sawa kati ya wale watakaoanza kwenye kikosi cha kwanza na wale watakaoanzia benchi.

“Nataka kila mchezaji wakiwemo Miquissone na Onana wajitume kwa asilimia zote ili kupata nafasi. Tumesajili wachezaji wazuri sasa kinachofuata ni kutengeneza timu yenye muunganiko imara kwa ajili ya michuano mbalimbali ambayo tunayo msimu huu,” alisema Robertinho na kuongeza;

“Naamini muda tulionao tutalifanikisha hilo kwa umoja na msimu ujao utakuwa bora zaidi kwetu.”

Simba tayari imefunga usajili kwa kushusha jumla ya majembe 10 mapya ambapo kati yao wazawa ni wanne mabeki, David Kameta ‘Duchu’ na Hussein Bakari ‘Kazi’, kiungo mkabaji Abdallah Hamis na mshambuliaji Shaaban Chilunda.

Wachezaji wa kigeni waliotua Simba katika dirisha kubwa hili ni sita, Kipa Mbrazil Jefferson Luis, beki Mcameroon Che Malone Fondoh, kiungo Mkongomani, Fabrice Ngoma na washambuliaji, Mcameroon Onana, Muivory Coast, Kramo Aubin na Miquissone raia wa Msumbiji aliyerejea Simba baada ya kuuzwa Al Ahly miaka miwili nyuma.

Idadi hiyo ya wachezaji imefanya Simba kutimiza wachezaji 12 wa kigeni katika kikosi chao kama inavyotakiwa na kanuni na taratibu za ligi, kwani tayari imemuuza Msenegal Pape Sakho kwenda Quevilly Rouen Metropole ya Ufaransa na kuachana na Mmalawi, Peter Banda.

KUTEST MITAMBO

Moja ya vitu alivyoanza navyo Robertinho alivyorejea kambini jana ni kutesti mitambo yake ambapo Simba ilikuwa uwanjani ikicheza mechi ya kirafiki na Zira FC ya Ligi Kuu nchini Azerbaijan iliyomalizika kwa kufungana bao bao 1-1, timu hiyo iliyomaliza nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi hiyo, msimu uliopita.

Hata hivyo, haitaishia hapo, kwa mujibu wa Robertinho, Simba itacheza mechi nyingine za kirafiki zisizopungua tatu kabla ya kurejea nchini tayari kwa mikikimikiki ya tamasha lao la ‘Simba Day’, mechi za Ngao ya Jamii na baadaye ligi.

“Tutacheza mechi za kirafiki ili kuangalia muunganiko wa wachezaji na uwezo wao wa kufuata maelekezo tunayowapa na baada ya hapo tukuwa tayari kwa kuanza msimu mpya,” alisema Robertinho.

Simba inatarajia kurejea nchini Agosti 1 na baada ya hapo Agosti 6, itakuwa kwenye kilele cha tamasha lao la Simba Day kisha itasafiri hadi Tanga kucheza mechi za Ngao ya Jamii dhidi ya Singida Foutain Gate Agosti 9, mwaka huu Uwanja wa Mkwakwani.

SOMA NA HII  HERSI ASHINDWA KUFAFANUA JAMBO HILI LA UBINGWA WA YANGA