Home Azam FC NGAO YA JAMII SAFARI HII HATARI, SIO SIMBA SIO YANGA MAMBO YAPO...

NGAO YA JAMII SAFARI HII HATARI, SIO SIMBA SIO YANGA MAMBO YAPO HIVI

KABLA ya kuanza kwa Ligi Kuu msimu ujao mwezi Agosti huwa kunakuwa na mechi ya uzinduzi ya Ngao ya Jamii.

Mechi hiyo awali ilikuwa ikihusisha bingwa wa Ligi Kuu na yule wa Kombe la Shirikisho la Azam (FA). Kukatokea mabadiliko ikawa inahusisha bingwa wa ligi Kuu dhidi ya mshindi
wa pili wa ligi.

Lakini msimu ujao wa 2023/2024 timu nne zitacheza kisha wale waliofanya vizuri wataingia fainali ili kupata bingwa mmoja ambazo ni Simba, Yanga, Azam FC na Singida Big Stars ambao kwa sasa wanajulikana kama Singida Fountain Gate.

Michuano hiyo ilizoeleka kuchezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa lakini awamu hii itachezwa kwenye uwnaja wa Mkwakwani mkoani Tanga ambako pia kulifanyika fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (FA).

Sio mbaya kikubwa mashabiki wa Tanga ni wenye bahati kushuhudia kwa mara ya kwanza Ngao ya Jamii yenye timu nne.

Ratiba inaonesha Agosti 9 bingwa mtetezi Yanga itavaana na Azam wakati Simba itaumana na Singida Fountain Gate Agosti 10. Mshindi wa pili, tatu, nne na bingwa mpya wa michuano hiyo atapatikana Agosti 13.

MSISIMKO

Timu hizi nne ndizo ambazo zimetoka kufanya vizuri kwenye ligi msimu wa 2022/2023 na zinatarajia kuwakilisha nchi kwenye michuano ya kimataifa. Mashabiki wa Tanga watashuhudia sasa timu zote kubwa kuchezwa kwao, Simba ikimenyana na Azam FC na Yanga dhidi ya Singida Fountain Gate.

Wamekuwa wakiona kwenye televisheni namna Simba ikicheza na Azam FC kwa ushindani mkubwa lakini sasa wataona kwa macho yao burudani kutoka kwa timu hizo.

Na pengine mwanzoni baada ya kutangazwa fainali ya FA ichezwe Tanga, walitamani ingezikutanisha Simba na Yanga ila mambo yalikuwa tofauti baada ya Azam kuwafunga wekundu Msimbazi katika mchezo nusu fainali uliochezwa mkoani Mtwara kwa mabao 2-1.

Kufungwa kwa Simba kulipoteza matumaini kwa mashabiki wekundu hao walioko Tanga kushuhudia fainali dhidi ya timu hizo.

Lakini kupitia Ngao ya Jamii huenda zikakutana kutegemea na matokeo ya mechi zao za awali za Ngao Jamii zitakavyokuwa na ndilo ambalo wataomba litokee ili kuwashuhudia watani zao wakicheza mkoani humo sio kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kama ambavyo ilizoeleka.

KUWAONA WAPYA
Watazishuhudia timu hizo zikiwa na mastaa wengine wapya. Kwa sasa timu zinakuwa zimesajili wachezaji wa kigeni kuweka nguvu kwa maandalizi ya msimu hivyo, wakishawatambulisha kwenye matamasha yao wanakutana kwenye ngao ya jamii kisha
wanakuwa tayari kujitathmini kuanza Ligi Kuu.

Na hapo Yanga imekuwa siku ya mwananchi ambayo huwatambulisha nyota wake na kucheza mechi za kirafiki na kadhalika, Simba inakuwa na tamasha lake ambalo pia, hutumika kutambulisha wachezaji wapya na kucheza mchezo wa kimataifa wa kirafiki.

Mashabiki wao wanatumia fursa ya kuona nyota wapya wakionesha ushindani na baada ya hapo ushindani mwingine wa kweli unahamia kwenye ngao ya jamii. Azam FC pia huwa ina
tamasha lake na wanafanya kama Simba na Yanga wanavyofanya.

Hakika baada ya matamasha, mashabiki wa mkoani Tanga ndio watakaofaidi ushindani wa kweli wa wachezaji wapya kupitia michuano hiyo midogo ya mtoano na kujua nani amesajili
vizuri na tayari kuanza msimu mpya.

UTOFAUTI
Timu watakazoenda kuziona sio zile ambazo waliona msimu uliopita ambao Yanga ilichukua taji, wanaweza kuona mambo mengine tofauti na ushindani mwingine tofauti na uliozoeleka.

Kwa mfano Yanga kwa sasa itakuwa chini ya kocha mwingine mpya ambaye hajawahi kuziona timu hizo zikicheza labda kama atapata nafasi ya kufuatilia video zao. Lakini tayari
kuna vikosi vingine tofauti pengine mfumo wa makocha ukabadilika.

Yanga itakuwa chini ya Miguel Gamondi kocha mpya aliyetangazwa hivi karibuni raia wa Argentina.

Azam FC itakuwa chini ya kocha mpya kutoka Senegal, Youssouph Dabo huku
Simba pekee ndiyo itakayokuwa na faida ikibaki na kocha wake, Roberto Olveira ingawa anaweza kupata wakati mgumu wa kupanga kikosi chake kulingana na usajili mpya.

Pia, Singida ilitajwa huenda ikaachana na kocha wake Hans Pluijm bado taarifa za uhakika hazijatolewa ni tetesi hivyo kama itakuwa hivyo watakuwa chini ya kocha mpya. Lakini haya yatajulikana baadaye.

Na timu ikishakuwa na kocha mpya huja na mfumo wake, mbinu zake ambazo ni tofauti pengine na zile zilizozoeleka kwa wachezaji lakini pia hupanga wachezaji wake aliowazoea wanaoendana na mfumo wake.

Kwa hiyo inategemewa ushindani wa aina yake ambao kila timu itataka kuonesha ubora namna gani wamejiandaa kitaifa na kimataifa. Kwa maana kwamba Simba na Yanga zinatarajiwa kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kwa upande wa Simba wana michuano mingine ya Afrika Super Cup. Kwa timu za Azam FC na Singida wao watawakilisha Kombe la Shirikisho la Azam.

FAIDA
Tanga ni karibu hivyo wategemee mashabiki kutoka mikoa jirani kama Dar es Salaam, Morogoro, Kilimanjaro na kwingine.

Wanaweza kupata wageni wengi kwa maana ya mashabiki wa timu hizo kwa hiyo ni faida kwa wafanyabiashara wa vyakula, jezi lakini pia hoteli na nyumba za kulala wageni zijiandae kupata wageni na kuongeza mapato.

Faida nyingine, Chama cha soka mkoani humo kitafaidika japo kidogo kwa mapato ya uwanjani kwani hakika watapata mashabiki wengi wa kujaza uwanja huo.

HASARA
Uwanja sio mkubwa sana watu wanaweza kuzidi kutegemea na mechi. Kwa mfano kama itatokea Simba na Yanga kukutana ni lazima watajaa sana kuleta msisimko, shangwe na furaha kwa timu zao.

Hata kama itakuwa Yanga au Simba dhidi ya Azam bado ni hivyo, kwa kuwa timu hizo zina mashabiki wengi.

SOMA NA HII  KUHUSU AZIZI KI KUCHEKA SANA NA NYAVU.........ISHU IKO HIVI MWENYEWE AFUNGUKA KILA KITU