Home Habari za michezo PAMOJA NA KUPEWA ‘THANK YOU’…MKUDE KAACHA MSALA HUU SIMBA…WAKONGWE WAONYA…

PAMOJA NA KUPEWA ‘THANK YOU’…MKUDE KAACHA MSALA HUU SIMBA…WAKONGWE WAONYA…

Tetesi za Usajili Yanga

JUZI uongozi wa Simba kupitia Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano, Ahmed Ally, ulitangaza kuiweka kando jezi namba 20 iliyokuwa ikivaliwa na kiungo wao Jonas Mkude ambaye wameachana naye.

Wiki iliyopita Simba waliachana na Mkude baada ya kukaa kwenye timu hiyo kwa miaka 13 mfululizo akiwa anatokea timu ya vijana.

Hata hivyo, taarifa zimekuwa zikisema kuwa mchezaji huyo anaweza kujiunga na Yanga kwenye dirisha hili la usajili.

Ahmed alisema jezi hiyo inawekwa kando hadi hapo atakapopatikana mchezaji mwingine kutoka timu yao ya vijana kama ilivyokuwa kwa Mkude aliyetoka kwenye timu hiyo na kudumu ndani ya Simba kwa kipindi kirefu.

Alisema kuwa jezi hiyo itatumika na mchezaji wa nafasi yoyote ilimradi awe ametoka timu ya vijana.

Baada ya kutangaza hivyo, wakongwe wa timu hiyo wameibuka na kuelezea kuwa walichokifanya viongozi wa Simba si sahihi kwani jezi hiyo inapaswa kuendelea kutumika na mchezaji mwingine kwasasa.

Beki wa zamani wa timu hiyo, George Masatu, alisema kuwa; “Sioni sababu ya kuipumzisha jezi eti hadi apatikane mchezaji mwingine kutoka timu ya vijana, asipopatikana mwenye ubora kama Mkude ina maana haitatumika milele, jezi zinazowekwa kando kikawaida ni zile za wachezaji waliofariki kama Patrick Mafisango ili mashabiki wasikumbuke machungu.

“Nawashauri tu viongozi wa Simba watulie kwenye maamuzi yao kwa sasa, waache wachezaji kwa sababu za msingi na wasajili ambao kweli watakuwa na msaada na timu yao,” alisema Masatu.

Naye mshambuliaji mkongwe wa timu hiyo Emmanuel Gabriel alisema kuwa; “Wanaiweka kando jezi ili iweje?, Hakuna sababu ila naona ni siasa zinaendelea ndani ya Simba, namna walivyomuacha wamekosea hivyo wanatafuta namna ya kujisafisha, waache jezi itumike na mchezaji mwingine.

“Binafsi naona Mkude atafanya vizuri huko atakapowenda na sidhani hayo mambo yao ya kumuaga kama yatafanikiwa endapo atasaini Yanga kweli, Yanga hawawezi kumruhusu kwenda kuagwa na hakuna sababu kwasasa, Simba hawajamheshimu Mkude,” alisema Gabriel.

Jezi ya Mkude ndani ya Simba ilianza kuvaliwa na kiungo mkongwe Primius Kasonso ambaye aliichezea timu hiyo kuanzia mwaka 2003 hadi 2007, alisema hajapendezwa na kilichoamuliwa na viongozi hao.

“Mkude siyo mwanzilishi wa hiyo jezi, nilianza kuivaa na sikutokea U20 na hakuna uhakika wa kumpata bora kama Mkude, ningependa jezi apewe mchezaji mwingine ndani ya Simba maana ni namba ambayo hutumika pia na timu nyingi.

“Niliichukua namba hiyo kwasababu miaka hiyo hakuna mchezaji wa Simba aliyekuwa akiitumia, zilikuwepo mbili 20 na 25 aliyokuwa anaitumia Marehemu Christopher Alex,” alisema Kasonso

Baada ya Kasonso jezi hiyo ilivaliwa na Sadick Muhimbo kutoka Congo na George Owino raia wa Kenya.

Alipoulizwa Mkude alisema kuwa; “Mimi jezi yao nimewaachia maana ni mali yao, hivyo lolote watakaloamua ni wao.”

SOMA NA HII  BAADA YA YANGA KUTEMA KOMBE LA MAPINDUZI ..KAZE AFUNIKA USO CHINI..ATAJA WACHEZAJI WALIOMFELISHA...