Home Habari za michezo ROBERTINHO ATAMBA KUHUSU KIKOSI CHA SIMBA

ROBERTINHO ATAMBA KUHUSU KIKOSI CHA SIMBA

Kocha Mkuu wa Simba SC Robertinho Oliveira Gonçalves do Carmo amekiri kuridhishwa na uwezo wa kikosi chake baada ya kucheza mchezo wa kwanza wa Kimataifa wa Kirafiki jana Jumatatu (Julai 24), nchini Uturuki.

Simba SC iliyoweka kambi mjini Ankara, ilicheza mchezo huo dhidi ya Zira FC iliyomaliza nafasi ya tano katika msimamo wa Ligi Kuu ya Soka nchini Azerbaijan, msimu uliopita 2022/23.

Robertinho amesema kikosi chake kilionesha uwezo mzuri na mkubwa, na imemsaidia kutambua wapi anapotakiwa kukazia maandalizi yake kabla ya kuelekea katika mchezo wa Pili wa Kimataifa ambao utatangazwa baadae.

“Nimefurahishwa na uwezo wa kikosi changu katika mchezo huu wetu wa kwanza wa Kirafiki, ni sehemu ya maandalizi yetu hapa Uturuki, kwa hakika yamenipa mtazamo chanya.”

“Lengo langu kubwa ni kuhakikisha wachezaji wanakuwa kitu kimoja na tunakuwa na kikosi imara, ninatarajia kuwa na michezo mingine miwili ama mitatu tukiwa hapa, kwa ahiyo ninatarajia kuona mazuri kutoka kwa wachezaji wangu.”

“Tumecheza na timu nzuri ambayo imetupa upinzani wa kutosha, na hilo ndilo limenisaidia mimi kuona wapi tulipokosea na wapi tulikuwa wazuri, kiukweli nimefurahi sana kwa uwezo wa kila mchezaji niliyempa nafasi ya kucheza.” Amesema Robertinho

Simba SC ilitangulia kupata bao la kuongoza kupitia kwa Kiungo Mshambuliaji Kibu Denis katika dakika ya 33, huku bao la Zira FC likifungwa na Rostan katika daiika ya 63.

SOMA NA HII  PAMOJA NA KUMFUNGIA AMROUCHE..., CAF WASHUSHA RUNGU LA PILI KWA TANZANIA....