Home Habari za michezo LUIS MIQUISSONE AZUA GUMZO KIKOSINI SIMBA

LUIS MIQUISSONE AZUA GUMZO KIKOSINI SIMBA

Tetesi za usajili Simba

Kikosi cha Simba SC kinaendelea kujifua kambini Ankara, Uturuki huku kikipokea nyota wapya waliosajiliwa hivi karibuni wakiwamo wazawa, Shaaban Idd Chilunda, Hussein Kazi na Hamis Abdallah, lakini unaambiwa usajili wa Luis Miquissone aliyerejeshwa klabuni umegeuka gumzo kila kona.

Licha ya Simba kusajili na kutambulisha mastaa wapya hadi sasa, usajili wa Luis umeonekana kukonga nyoyo za wanasimba na baadhi ya wadau wa soka ndani na nje ya nchi wakiueleza una maana gani kwa msimu ujao wa kikosi hicho.

Nyota huyo aliuzwa misimu miwili iliyopita na Simba kwenda Al Ahly ya Misri, lakini alikosa nafasi katika kikosi cha kwanza kiasi cha kutolewa kwa mkopo kwa timu ya Abha kabla ya hivi karibuni Ahly kuvunja naye mkataba na kuibukia Msimbazi iliyokuwa ikimwinda kwa muda mrefu.

Usajili huo umeonekana kama muarubaini kwa timu hiyo iluiyopoteza mataji yote iliyokuwa nayo kwa misimu miwili mfululizo mbele ya Young Africans na kufanya wadau kumjadili tangu alipotambulishwa juzi Jumamosi (Julai 22) mchana.

Mmoja wa wanachama wa Simba wanaoishi Afrika Kusini, Abdullah Mabange amesema kuwa, kurejea kwa fundi huyo ni moja ya sajili zilizokuwa zikililiwa kwa muda mrefu na wanasimba na kwamba kilichobaki ni kuona mziki wa Msimbazi ukiwafunika wapinzani.

“Nawapongeza sana viongozi wa klabu yetu kwa kutupa amani ya moyo, huyu fundi bwana karudi atakutana na mafundi wenzake maana ujio wake kuna watu hawakulala,” amesema Mabange aliyeongeza hata nyota wengine waliosajiliwa na kubakizwa kikosini ni wazuri na ndio maana wamesajiliwa kuitumikia time ya yenye mafanikio makubwa ndani na nje.

Kwa upande wa kocha na mchambuzi wa soka, Kennedy Mwaisabula amesema usajili wa Luis umekuja wakati muafaka ambao Simba inapambana kurejesha furaha kwa mashabiki wao.

“Miquissone( Luis) ni mchezaji ambaye upenda wa pili hawataki wala hawahitaji kumsikia, ni usajili mzuri na mkubwa sana nawapongeza Simba katika kutimiza kiu ya wapenzi wa klabu yao,” amesema Mwaisabula.

Kocha huyo amesema wale wanaohoji alifanya nini alipokuwa Al Ahly au Abha wanapaswa kutulia kwani anaamini atafanya vizuri hapa kutokana na mahitaji yake na ubora aliokuwa nao.

Luis ataungana na nyota wapya waliotimba kambini juzi akiwamo kipa Jefferson Luis kutoka Brazili aliyetambulishwa jana Jumapili (Julai 23) kama tulivyowahabarisha, Chilunda, Kazi na Hamis.

Pia kuna vifaa vipya vilivyotangazwa mapema kama Fabrice Ngoma, Aubin Kramo, Willy Onana, David Kameta ‘Duchu’ na beki Mcameroon, Che Fondoh Malone, waliochukua nafasi ya nyota 10 waliotemwa katika kikosi kilichopita kilichomaliza nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu Bara.

SOMA NA HII  KAGERE WA SIMBA RUKSA KWENDA KUKIPIGA YANGA