Home Habari za michezo SIMBA WATAMBA KUHUSU USAJILI WAO MPYA, CHAMA, NGOMA WAHUSISHWA

SIMBA WATAMBA KUHUSU USAJILI WAO MPYA, CHAMA, NGOMA WAHUSISHWA

WAKATI Clatous Chama na Fabrice Ngoma wakiinogesha kambi ya mazoezi ya Simba iliyopo Uturuki baada ya mastaa hao kutimba juzi wakitokea Dar es Salaam, nyota wapya wazawa, kiungo Abdallah Hamisi na Hussein Kazi wameanza tambo wakisema miguu yao itaongea uwanjani.

Chama na Ngoma ni kati ya wachezaji waliochelewa kuondoka kwenda Uturuki kwa sababu tofauti, lakini juzi mara baada ya kumalizana na ishu zao walikwea pipa na kutimba kambini na kuifanya inoge zaidi, wakiungana na wenzao waliotangulia tayari kujiandaa na msimu mpya.

Wachezaji hao sambamba na wengine waliopo kambini humo pamoja na benchi la ufundi juzi walipata nafasi ya kumtembelea Balozi wa Tanzania nchini Uturuki, Luteni Jenerali Mstaafu, Yakubu Hassan Mohammed aliyepata wasaa wa kuzungumza nao.

Ngoma aliyesajiliwa kutoka Al Hilal ya Sudan, alipokelewa kwa staili ya aina yake ya kuwekewa mistari miwili na wachezaji wenzake pamoja na watu wa benchi la ufundi kisha kupita katikati yao kwa kupigwa makofi mepesi mgongoni ikiwa ni ishara ya kukaribishwa rasmi Simba.

Lakini mambo yakiwa hivyo, nyota wawili kati ya watatu wazawa waliosajiliwa na kutambulishwa rasmi, wamefunguka juu ya namna walivyijipanga kuwapa raha mashabiki wa Msimbazi, licha ya kuwa ni mara ya kwanza kuchezea timu kubwa na zenye presha kama Simba.

Hamis aliyepewa mkataba wa miaka miwili, alisema kwa uzoefu alionao na kwa kushirikiana na wachezaji wenzake wanaweza kufanya makubwa msimu ujao.

Kiungo huyo ni Mtanzania aliyecheza soka la kulipwa nje ya nchi kwa miaka mingi, ataungana na Sadio Kanoute, Mzamiru Yassin, Nassor Kapama na Fabrice Ngoma kwenye eneo la kiungo mkabaji.

“Siku zote nimekuwa nikipenda changamoto, najua ukubwa wa Simba na daraja la wachezaji waliopo, nitatumia uzoefu wangu ili kuisaidia timu kufikia malengo, asanteni nyote ambao mmenitumia jumbe za pongezi kwangu hii ni hatua nyingine,” alisema Hamis aliyewahi kuzitumikia timu za Muhoroni Youth, Sony Sugar, Bandari za Kenya pamoja na Orapa United ya Botswana.

Kwa upande wa Kazi alitambulishwa siku moja na Hamis, alisema kurejea Simba ina maana kubwa sana kwake kwa sababu ni timu ambayo alianza kutafuta mafanikio yake kwenye soka.

“Nilianza kucheza Simba timu ya vijana kabla ya kwenda nje kupambana, nipo tayari kwa changamoto mpya,” alisema beki huyo wa kati.

Kazi ni beki wa kati atakuwa na kibarua cha kupigania namba mbele ya wazoefu Henock Inonga, Kennedy Juma na Che Fondoh Malone.

Hussein amecheza soka la kulipwa Shelisheli katika timu ya Forester FC kabla ya kujiunga na Mbeya Kwanza, Polisi Tanzania na Geita Gold.

SOMA NA HII  ROBERTINHO AFUNGUKA HALI YA WACHEZAJI WA SIMBA HUKO UTURUKI SIO POA.......ISHU IKO HIVI