Home Habari za michezo MASHABIKI WA SIMBA MZUKA UMEPANDA, UNAJUA KWANININI? ISHU IKO HIVI

MASHABIKI WA SIMBA MZUKA UMEPANDA, UNAJUA KWANININI? ISHU IKO HIVI

SIMBA SC YAFANYA KUFURU...WINGA MATATA WA KIMATAIFA...USAJILI WA KUTISHA MAPEMAA

MASHABIKI wa Simba mzuka umepanda. Unajua kwa nini? Wamepata taarifa kwamba katika kambi ya timu hiyo iliyopo Uturuki, ametua kipa kutoka Brazili, Jefferson Luis Szerban de Oliveira aliyetambulishwa kwa wachezaji wenzake akiwa amepewa miaka miwili, lakini jana saa 7 mchana, Luis Miquissone naye alitambulishwa kuhitimisha kile tulichokiandika.

Baada ya muda mrefu ikimfukizia kumrejesha kikosini, hatimaye jana Simba imemtambulisha rasmi, Luis akipewa mkataba wa miaka mitatu akiwa mchezaji huru, huku mitandaoni kukilipuka kwa mashabiki wa klabu hiyo kusema; ‘Ligi Kuu na ianze tu’.

Mashabiki mbalimbali walichimba mkwara huo kwa kuamini chama la Msimbazi safari hii limekamilika kutokana na vyuma vilivyosajiliwa, hivyo kuamini wanarejesha heshima iliyopotea kwa misimu miwili iliyopita mbele ya watani wao, Yanga.

Luis aliyeuzwa na Simba misimu miwili iliyopita kwa Al Ahly ya Misri, alitambulishwa ikiwa ni wiki chache tangu Mwanaspoti lilipofichua dili hilo la nyota huyo kutoka Msumbiji kurejea kikosini ili kuendeleza ule moto uliotikisa soka la Tanzania.

Nyota huyo amerejea Msimbazi kama mchezaji huru baada ya kuvunja mkataba na Al Ahly na anakuwa mchezaji wa tisa kusajiliwa hadi sasa ndani ya Simba akiungana na Willy Onana, Aubin Kramo, Che Fondoh Malone na Fabrice Ngoma pamoja na wazawa, David Kameta ‘Duchu’, Hussein Kazi, Shaaban Idd Chilunda na Hamis Abdallah.

Kuingia kwa Luis kunamfungulia milango Peter Banda kusepa kikosini, huku mashabiki wakisubiri utambulisho wa Jefferson aliyepewa miaka miwili atakayechukua nafasi ya Pape Ousmane Sakho anayetarajiwa kuuzwa nchini Ufaransa.

Tofauti na ilivyoripotiwa jana kwamba Simba imemsainisha kipa Mcameroon Simon Omossola anayetokea Saint Eloi Lupopo ya DR Congo, ukweli ni kwamba Wekundu hao wamemvuta Mbrazili Jefferson Oliveira mwenye miaka 29 aliyetambulishwa jana kambini Uturuki.

Kipa huyo amesajiliwa kutoka Resende iliyopo Serie D nchini Brazili na baada ya Simba kumpiga chini Mcameroon, ambaye awali alipewa nafasi kubwa baada ya kutemwa Mbrazili mwingine Caique Luis Santos, kisha ikampeleka kambini na kumtambulisha kwa wachezaji wenzake.

Kipa huyo alikuwa akiichezea Resende kwa mkopo kutoka Itabirito FC aliyojiunga nayo mwaka jana na anatua Msimbazi kumsaidia Aishi Manula aliye majeruhi na Ally Salim aliyekuwa ndiye tegemeo kwa mechi za mwisho za msimu uliopita.
Kanuni za Ligi kwa wachezaji wa kigeni, zinaruhusu wachezaji 12 na ujio wa Luis na kipa huyo Mbrazili unaifanya Simba iwe na wachezaji 14 kwa sasa, hivyo mabosi wa klabu hiyo kulazimika kuwafyeka wawili huku majina ya Banda na Sakho yakihusishwa baada ya mazungumzo ya ndani.

Habari kutoka ndani ya Simba ni kwamba Luis amerudishiwa jezi namba 11 aliyokuwa akiitumia kabla ya kuondoka ambayo ilivaliwa na Banda na tangu kuwekwa kwa ‘tiza’ ya utambulisho wa nyota huyo mashabiki na wapenzi wa Simba walikichafua mtandaoni wakieleza namna chama lilivyotimia.
Wengi walikuwa wakisema ligi na ianze sasa ili wamalizane mapema na watani wao waliowanyang’anya mataji yote kwa misimu miwili iliyopita wakati Luis akitaabika kule Al Ahly.

Simba iliweka rekodi ya kubeba mataji ya Ligi Kuu Bara kwa misimu minne mfululizo sambamba na Kombe la ASFC, Ngao ya Jamii kabla ya Luis kuuzwa pamoja na Clatous Chama aliyeenda RS Berkane ya Morocco kisha kurejeshwa msimu mmoja na nusu uliopita. Luis aliondoka Simba akiwa amefunga mabao 9 na asisti 15 kwa msimu wa 2020-2021.

Simba ilimsajili Luis misimu mitatu iliyopita akitokea UD Songo ya Msumbiji baada ya kufunga bao lililowang’oa Wekundu katika mechi ya raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa msimu wa 2019-20 baada ya sare ya 1-1 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa

SOMA NA HII  SIRI YA GAMONDI KUTUA YANGA YAFUCHUKA, NABI AHUSISHWA