Home Habari za michezo SIRI YA GAMONDI KUTUA YANGA YAFUCHUKA, NABI AHUSISHWA

SIRI YA GAMONDI KUTUA YANGA YAFUCHUKA, NABI AHUSISHWA

Habari za Yanga SC

Dar es Salaam. Kocha wa Yanga, Migel Gamondi amesema mafanikio makubwa iliyopata Yanga msimu uliopita ndiyo sababu kubwa iliyomvuta Jangwani, kwani yeye ni muumini wa mafanikio.

Gamondi alikiri kuwa kazi kubwa ya kufanya aliyonayo mbele yake kuvuka mafanikio ya mtangulizi wake, Nasreddine Nabi.

Nabi, ambaye alikaa na Yanga kwa misimu miwili na nusu alifanikiwa kutwaa mataji mawili ya Ligi Kuu Tanzania Bara, mawili ya Kombe la FA (ASFC) na mawili ya Ngao ya Jamii, huku akiifikisha miamba hiyo katika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Gamondi, ambaye aliwasiri nchini usiku wa Julai 7, amepewa kibarua cha kuwafundisha mabingwa watetezi wa soka nchini akiaminika kuwa mtu sahihi kwa ajili ya kuongeza mafanikio Jangwani.

Akizungumza na Mwananchi jana, Gamondi alisema anatambua kuwa ana kibarua kigumu cha kuvuka mafanikio aliyoyakuta, lakini kitu pekee kilichomfanya awahi nchini ni kupata muda wa kuwasoma wachezaji pamoja na mazingira ya Tanzania.

“Si rahisi, lakini inawezekana, nilikuwa na ofa nyingi lakini nimechagua Tanzania kwa sababu nimepata ofa kutoka kwenye timu ambayo imepata mafanikio makubwa na mimi ni muumini wa mafanikio.

“Natarajia kuwa na timu nzuri na bora na napenda kuwa na wachezaji ambao ni waumini wa kucheza mpira, natamani kuona timu yangu inacheza soka safi kuanzia nyuma hadi mbele,” alisema Gamondi.

Kocha huyo raia wa Argentina alisema anafahamu kuwa anatazamwa na kila mwanasoka kuona atafanya nini Yanga, hivyo ana kila sababu ya kukaa na wachezaji wake mapema ili kutambua wapi palipo na shida na wapi wanatakiwa kurekebisha kabla ya msimu kuanza.

Alisema ameuomba uongozi kuwarudisha wachezaji kambini mapema ili aweze kupata muda wa kuanza kuwazoea mmoja mmoja, namna wanavyocheza kabla ya msimu mpya haujaanza ajue ni namna gani anaweza kuanza msimu vizuri.

“Bado sijapata nafasi ya kukaa na wachezaji, lakini nimeomba nafasi hiyo ili kuanza kambi mapema, mimi ni mgeni kikosini, nahitaji kuona ubora wa kila mchezaji ili nifahamu nafanya kazi na watu wa aina gani,” aliongeza Gamondi.

Alisema anafurahi kutua Tanzania anaendelea kuyasoma mazingira kadri siku zinavyozidi kwenda, anaamini ni nchi nzuri na ina ushindani wa kutosha yupo tayari kukabiliana na ushindani.

Gamondi ana kazi kubwa ya kuendeleza mafanikio ya Nabi, ambaye aliiacha Yanga ikiwa na kila taji la mashindano iliyocheza Tanzania Bara kwa misimu miwili mfululizo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here