Home Habari za michezo KOCHA WA YANGA AKUTANA NA MASTAA WA KLABU HIYO LEO KWA MARA...

KOCHA WA YANGA AKUTANA NA MASTAA WA KLABU HIYO LEO KWA MARA YA KWANZA

Tetesi za Usajili Yanga

Kocha Mkuu mpya wa Young Africans Miguel Gamondi, leo Jumatano (Julai 12) anakutana na wachezaji wake kwa mara ya kwanza, kuanza mazoezi ya ‘Gym’ kuweka miili sawa kabla ya kwenda uwanjani.

Gamondi raia wa Argentina, hivi karibuni alipewa mkataba wa miaka miwili kuinoa timu hiyo akichukua mikoba ya Nasreddine Nabi, aliyeondoka baada ya msimu wa 2022/23 kufikia tamati mwezi Juni.

Meneja wa Young Africans, Walter Harrison, amesema wanaanza mazoezi rasmi kujiandaa na msimu mpya wa mashindano yote ya msimu wa 2023/24.

Amesema katika programu ya kocha kuna ratiba mbili za mazoezi kwa siku, asubuhi watafanya mazoezi ya viungo katika gym za Gymkhana kabla ya jioni kufanya mazoezi ya uwanjani katika Uwanja wa Avic Town, Kigamboni, Dar es salaam.

“Ratiba ya msimu ujao inaanza leo Jumatano (Julai 12), wachezaji wote ambao wana mikataba na Yanga wapo Dar es salaam kwa kuanza mazoezi ya pamoja na kocha mpya, tunaamini kwa kuanza pamoja tutakuwa kitu kimoja,”amesema.

Harrison amesema ambao wanatarajiwa wachezaji kusajiliwa na wenzao kuitumikia Young Africans msimu ujao, watakuja kuungana watakapomalizana na uongozi.

Amesisitiza kuwa, wachezaji wa timu hiyo walianza kuripoti juzi katika kambi yao wakiwa tayari kwa maandalizi ya msimu huo mpya.

Meneja huyo amesema Gamondi tayari amepanga ratiba nzima ya maandalizi ya msimu mpya baada ya kufanya kikao na uongozi wa klabu hiyo na benchi la ufundi.

“Kocha anasema hakuna muda wa kuchelewa zaidi. Wachezaji wameshaanza kuripoti kambini na kazi kubwa iliyokuwa mbele yetu ni kutengeneza timu nzuri ya kwenda kushindana msimu ujao” amesema.

SOMA NA HII  AZAM WAIFANYIA JANJA TFF KUHUSU ISHU YA DABO