Home Habari za michezo SIMBA, YANGA KABLA YA LIGI KUANZA KIMESHAUMANA MAPEMAAA

SIMBA, YANGA KABLA YA LIGI KUANZA KIMESHAUMANA MAPEMAAA

LIGI imeanza mapema. Ndio, huko mtaani na kwenye mitandao ya kijamii ile ligi ya mashabiki na wapenzi wa klabu za Simba na Yanga imeanza. Hii imechangiwa zaidi na shusha nishushe inayoendelea baina ya klabu hizo. Simba ikishusha chuma kipya. Yanga nao wanashusha jembe lao na kuwapa burudani mashabiki na wapenzi wa klabu hizo.

Simba ilianza kumtambulisha Willy Onana kuitoka Rayon Sports ya Rwanda. Yanga ikajibua mapigo kwa kumsajili Nickson Kibabage kutoka Singida Fountain Gate. Kelele zikawa nyingi, wale wa Msimbazi wakiamini wamefunika mbaya mbele ya watani wao.

Simba ikamshusha tena Aubin Kramo kutoka Asec Mimosas ya Ivory Coast. Yanga haikujibu. Simba ikaendeleza moto kwa kumtoa hadharani Che Fondoh Malome wa CotonSport ya Cameroon. Hapo Yanga ikashtuka na kumleta beki kutoka SC Villa ya Uganda, Gift Fred.

Simba inamtambulisha David Kameta ‘Duchu’, Yanga ikajibu mapigo kwa Jonas Mkude, kiungo mwandamizi aliyeichezea Simba kwa misimu 13 mfululizo.

Kama haitoshi, ikamleta winga mwingine teleza maarufu kama Mbappe wa DR Congo, Maxi Mpia Nzengeli kutoka AS Maniema Union ya DR Congo. Msimbazi nao hawakupoa wakamtoa hadharani Fabrice Ngoma aliyekuwa Al Hilal ya Sudan. Yanga nao wakajibu kwa kumteremsha beki wa kumwaga maji kutoka Asec Mimosas ya Ivory Coast, Kouassi Yao Attahoula. Kimahesabu kwa nyota waliotambulishwa na timu hizo hadi sasa ni watano kwa watano, lakini sio kama kazi imeisha.

Unaambiwa Simba inajiandaa kumtambulisha winga Luis Miquissone kutoka Al Ahly ya Misri, huku Yanga inadaiwa inamalizana na straika mmoja mkali kutoka nje ya nchi ili aje kuchukua nafasi ya Fiston Mayele aliyepata dili jipya Arabuni kwa sasa.

Bahati nzuri ni kwamba dirisha la usajili lipo wazi hadi Agosti 31, hivyo bado kuna muda mrefu wa klabu hizo na nyingine kuongeza majembe mapya wakiwamo wachezaji wa kizawa ili kuchukua nafasi za waliopewa ‘thank you’, kwani mabosi wa klabu hizo wametamba kwamba hawajamaliza.

Lakini wakati mabosi wa Simba na Yanga wakitamba kuwa ‘hawajamaliza’ kushusha mashine mpya, huku mtaani na mtandaoni mashabiki na wapenzi wa timu hizo wanapigana mkwara wakiambiana kwa ‘mziki huu, mtakuja uwanjani kweli’, huku wengine wakidai kama vipi, waombe hata mechi ya kirafiki watesti mitandao kwa sasa ili wamalize ubishi mapema kabla ya mechi za Ngao ya Jamii.

Mechi za Ngao ya Jamii zinatarajiwa kupigwa kuanzia Agosti 9 kwa watetezi, Yanga kucheza na Azam FC kisha siku inayofuata itakuwa zamu ya Simba dhidi ya Singida Fountain Gate michezo yote ikipangwa kupigwa Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga na washindi wa mechi hizo kutinga fainali itakayopigwa Agosti 13 ikitanguliwa na mechi ya kusaka mshindi wa tatu.

Siku mbili baada ya kupigwa kwa mechi ya fainali na ile ya kusaka mshindi wa tatu wa Ngao ya Jamii baada ya Shirikisho la Soka nchini (TFF) kufanya mabadiliko ikiiga mfumo unaotumiwa kule Hispania, Ligi Kuu Bara itaanza rasmi kulingana na kalenda iliyotolewa na Bodi ya Ligi (TPLB).

Siku tatu baada ya kuanza kwa msimu mpya wa Ligi Kuu Bara, timu hizo nne zitakuwa kwenye majukumu mengi ya michuano ya kimataifa, Yanga na Simba zikicheza Ligi ya Mabingwa, wakati Azam na Singida zenyewe zitakuwa kwenye Kombe la Shirikisho Afrika zinazoanza Agosti 18.

Kwa namna timu hizo zilizofanya usajili hadi sasa kwa kuboresha baadhi ya maeneo ni wazi msimu ujao unaweza kuwa moto kuliko ilivyokuwa misimu miwili iliyopita ambapo Yanga, Simba na Azam zilikomalia nafasi tatu za juu na kwa ile ya nne ikiachwa kugombewa na timu nyingine.

katika msimu uliopita katika mechi ya Ngao ya Jamii, Simba iliicharazwa na Yanga kwa mabao 2-1, kisha kwenye mchezo wa duru la kwanza la Kariakoo Derby zilishindwa kutambiana kwa sare ya 1-1 na mchezo wa pili wa marudiano, Yanga ilicharazwa mabao 2-0 na kuwapa Msimbazi Kicheko.
Ingizo la Onana aliyemaliza kama kinara wa mabao wa Ligi Kuu ya Rwanda akifunga mabao 16 na asisti tano, huku akitangazwa kuwa Mchezaji Bora wa ligi hiyo, sambamba na Aubin Kramo aliyeng’ara kwenye Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita akifunga mabao manne, huku beki Malone akitua akiwa Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ya Cameroon kumeongeza mzuka mwingi Simba.

Kwa upande wa Yanga kuingia kwa Kibabage anayemudu kucheza kama beki wa kushoto na winga wa upande huo, pamoja na Yao anayemudu beki zote za pembeni, huku kukiwa na ongezeko la kiungo wa kati, Mkude na beki Fred pamoja na winga Maxi anayesifika kwa kasi na chenga, Yanga inaona kama inaenda tena kufanya mambo makubwa kuliko misimu miwili iliyopita.

Yanga inajua haitakuwa na Mayele aliyekubaliana na uongozi wa Yanga kuondoka, lakini uwepo wa asilimia kubwa ya nyota wa kikosi cha kwanza kilichotumika msimu uliopita na kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, umewapa jeuri na kuwatambia watani wao wa Simba.
Mashabiki wa Yanga wanaamini langoni kocha mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi hatakuwa na kazi ngumu kupanga kikosi cha kwanza kutokana na kuwepo kwa kuwepo Diarra Djigui, huku kulia anaweza kumpangaa Yao na kushoto atakuwapo ‘Waziri wa Maji’, Joyce Lomalisa.

Katika beki ya kati kuna uwezekana wa Gamondi kuwatumia Fred au Abdallah Bacca na Bakar Mwamnyeto kama sio Dickon Job, huku kiungo mkabaji atakuwa Mkude au Khalid Aucho na kiungo cha juu atasimama kati ya Mudathir Yahya au Salum Abubakar ‘Sure Boy’.

Winga wa kulia wanaamini ataanza kucheza kiberenge, Maxi na mshambuliaji wa kati atakuwa mashine mpya inayosakwa sasa, wakati mshambuliaji wa pili anatarajiwa kusimama Kennedy Musonda au Stephane Aziz KI, huku winga ya kushoto ataliamsha Kibabage kama sio Aziz Ki.
Kwenye benchi kutakuwa na watu wa nguvu kama Metacha Mnata na Abutwalib Mshery kumsaidia Diarra, wakati Kibwana Shomary, Farid Mussa, Dickson Job, Clement Mzize, Jesus Moloko watasubiri kuwapokea wenzao.
Kwa upande wa Simba jeuri imekuwa kubwa zaidi licha ya kutema wachezaji wengi kulinganisha na watani wao wa Yanga, kwani Simba imepiga chini mashine tisa hadi sasa ilihali Yanga imeacha saba tu, hii ni kutokana na kila idara kwa sasa Msimbazi kuwa na watu wa nguvu.

Aishi Manula wakati anajiuguza langoni inatarajiwa kuwepo kipa mwingine mpya anaendelea kusakwa, huku upande wa kulia kukiwa na Shomary Kapombe wakati Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ akiendelea kusimama kushoto na beki ya kati itakuwa chini ya Malone na Henock Inonga, wakati Sadio Kanoute atasimama kiungo mkabaji, huku winga ya kulia ikiwa chini ya Onana na ile ya kushoto akiachiwa Luis Miquissone, wakati Mzamiru Yassin au Fabrice Ngoma kama sio Clatous Chama watakaoshika kiungo cha juu, huku Jean Baleke kama kawaida atasimama kama mshambuliaji wa kati. Saido Ntibazonkiza au Kramo kama sio Chama atacheza kama mshambuliaji msaidizi.

Huko benchi kutakuwa na vifaa vya maana akiwamo Duchu, Israel Mwenda, Ally Salim, Kennedy Juma, Moses Phiri, Kibu Denis, Jimmyson Mwanuke na John Bocco watasubiri kuona Roberto Oliveira ‘Robertinho’ watawaingiza kuchukua nafasi ya nani ili kuendeleza moto wa Msimbazi.

WASIKIE WADAU
Baadhi ya wadau wa soka nchini wamekoshwa na usajili unaondelea hadi sasa kwa kila timu huku Yanga na Simba zitakazoiwakilisha nchi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika zikiteka zaidi hisia za wengi.

Akizungumza na Mwanaspoti kocha wa zamani wa Ruvu Shooting na Yanga, Boniface Mkwasa ‘Master’ alisema kila timu inaonekana imejipanga vizuri ingawa ni mapema sana kuwazungumzia wachezaji hao hadi pale watakapocheza.

“Kwa usajili wa Yanga mimi namkubali Nickson Kibabage, Jonas Mkude kwa sababu nimewaona na hata kwenye timu ya taifa niliwahi kumuita, wengine siwezi kusema ni wabaya au wazuri kutokana na kutowaona huko walikotoka.”

Mkwasa aliongeza licha ya usajili mzuri uliofanyika ila tathimini yake ataifanya pale watakapoanza tu kucheza.
“Simba imekuwa na maboresho makubwa na hii ni kutokana na malengo waliyojiwekea kwa msimu ujao, wachezaji wote wanaonekana ni wazuri kutokana na huko walikotoka hivyo tuwape muda kwanza ndipo tuanze kuwajadili.”

Kwa upande wa nyota wa zamani wa Simba, Boniface Pawasa amefurahishwa na usajili wa timu zote hadi sasa huku akitoa tahadhari kwa viongozi wa klabu hizo kusajili kwa matakwa ya benchi la ufundi na sio kwa mihemko tu.

“Ukiangalia profile (wasifu) wa wachezaji wote huko walikotoka unakupa matumaini wanaweza kuzifikisha hizi timu zetu nchi ya ahadi hivyo nasubiri kuona walichokifanya huko wakilete pia na huku kwa manufaa yetu.”

Kocha wa zamani wa Azam, Idd Nassor ‘Cheche’ anayeifundisha Pan Africans alisema usajili ni kamari hivyo hawezi kutoa sifa kubwa kwa kilichofanyika hadi nyota hao watakapocheza michezo mitano au sita.

SOMA NA HII  SIRI YA GAMONDI KUTUA YANGA YAFUCHUKA, NABI AHUSISHWA