Home Habari za michezo SIMBA, YANGA WAWEKA WAZI MALENGO YA USAJILI WAO DIRISHA KUBWA LA USAJILI

SIMBA, YANGA WAWEKA WAZI MALENGO YA USAJILI WAO DIRISHA KUBWA LA USAJILI

Dirisha la usajili kwa klabu za ligi kuu ya NBC (NBCPL), ligi daraja la kwanza (Championship) na ligi kuu wanawake (SLWPL) limefunguliwa kuanzia Julai mosi hadi Agosti 31 kwa ajili ya timu kufanya usajili na uhamisho wa wachezaji ambapo timu mbalimbali hutumia wakati huu kufanya maboresho ya vikosi vyao kulingana na mahitaji yaliyotokana na mapungufu kwenye msimu ulioisha.

Ifuatayo ni ripoti fupi maalumu ya kiufundi (Technical Report) inayoangazia mahitaji ya muhimu kwa timu mbili za Kariakoo ambazo zimeongoza msimamo wa ligi ya NBC 2022/23 na kikanuni zitawakilisha nchi kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao, Yanga Sc na Simba Sc.

Kwenye ripoti hii fupi nitazingatia maeneo muhimu kama upana wa vikosi kuanzia kwa wataalamu wa benchi la ufundi hadi kwa wachezaji nikisindikiza hoja zangu kwa takwimu na mahitaji ya kimbinu

YANGA SC

Hawa ndiyo mabingwa wa ligi kuu ya NBC (NBCPL), kombe la FA (ASFC) na washindi wa ngao ya jamii kwa misimu miwili mtawalia, hali inayoakisi kuwa ndio timu iliyokua bora zaidi msimu uliopita.

Ubora

Yanga Sc walikua bora zaidi ya Simba Sc kwenye maeneo mengi msimu uliopita kama;

1. Upana wa kikosi

Ni wazi kuwa Yanga walikuwa na kikosi chenye wachezaji wengi wenye viwango vinavyokaribiana kiufundi (individual technical ability), utimamu wa kimwili (physical ability) na uelewa wa mbinu za walimu wao kiasi kwamba hakukuwa na utofauti mkubwa wa uwasilishaji wao wa mbinu uwanjani.

Karibia nafasi zote za Yanga zilikuwa na wachezaji zaidi ya wawili wenye viwango vinavyokaribiana ndiyo maana staili ya uchezaji na mifumo yao ilikuwa haibadiliki sana hata wakifanya mabadiliko ya kikosi kwa kiasi kikubwa kasoro eneo la beki wa pembeni kushoto ambalo licha ya kuwa lilikuwa na wachezaji wenye viwango vinavyokaribiana kama Joyce Lomalisa na Bryson David lakini mara nyingi na muhimu Nabi alimpanga Kibwana Shomari kwa sababu ya uwezo wake bora wa kulinda kuliko David na Lomalisa.

2. Benchi la ufundi bora

Hakuna shaka kuwa Yanga Sc ndio timu iliyokuwa na benchi la ufundi lililokuwa bora zaidi kuliko timu zingine kutokana na mambo mbalimbali yaliyoakisiwa na benchi hilo kuanzia mbinu za mkuu wao Nasredine Nabi, usaidizi wa wasaidizi kama Cedric Kaze anayekuwa na Nabi kwenye benchi na mtathmini wa viwango Halil Bin Yusuph anayekaa jukwaani.

Hawa ni washauri wakuu ambao ushauri wao nimeuakisi kwenye nyakati muhimu kama wakati wa timu kutafuta mbinu mbadala hasa kwenye mechi ambazo timu ilibadili mbao za matokeo kipindi cha pili, hii ikiwa na maana kuwa mchango wa mawazo wa kimbinu kutoka kwa wasaidizi hawa wa Nabi uliongeza nguvu.

Lakini pia kocha wa makipa Milton Nionev ambaye ufundishaji wake wa makipa ulishabihiana na mahitaji ya Nabi hasa timu inapokuwa na mpira kipa kuwa mchezeshaji.

Mahitaji ya Nabi kwa golikipa hayakuwa wakati wa kuzuia tu, bali hata wakati wa kushambulia Nabi alihitaji kipa mwenye uwezo wa kusaidia timu kujenga mashambulizi kuanzia kwenye theluthi yao ya kwanza (build up phase) ambapo mfumo wao mama wa 4-2-3-1 ulinyumbulishwa kuwa kwenye muundo wa 3-3-4-1, Diara akiwa ameongeza idadi kwa wale watatu wa nyuma ambapo wakijenga shambulizi husimama sambamba na mabeki wa kati hasa wanapocheza dhidi ya timu inayopenda kuanza kuzuia kuanzia theluthi ya kwanza ya wapinzani (highline pressing).

Bila kumsahau kocha wa viungo Helmy Gueldich ambaye alisaidia kuwaweka wachezaji kuwa kwenye utimamu bora kusindikiza mbinu za Nabi hasa kwenye mechi zilizohitajika kumalizwa dakika za jioni, bado wachezaji walionekana kuwa timamu kuwasilisha vyema mbinu za waalimu wao.

Mapungufu

Licha ya Yanga Sc kuwa bora lakini pia ilikuwa na mapungufu yake;

1. Takwimu zisizoridhisha za viungo washambuliaji

Kazi kubwa ya viungo washambuliaji ni kutengeneza nafasi za upatikanaji wa mabao, kwa Yanga muda mwingi walikuwa wakitumia mshambuliaji mmoja kwenye mfumo wao wa 4-2-3-1, walitumia zaidi mshambuliaji mmoja wa kati nyuma yake wakicheza viungo watatu washambuliaji, wa pembeni wawili na kiungo mshambuliaji mmoja

Yanga licha ya upana wa kikosi chake lakini takwimu za uchangiaji wa mabao za washambuliaji wao wa pembeni, hazikuwa na uwiano na mahitaji sahihi ya timu yao, upungufu wa watengenezaji hawa pengine ndio uliwafanya Yanga kutoka na idadi kubwa ya mabao zaidi ya Simba licha ya kuwa mabingwa, Yanga ni timu ya pili kufunga mabao mengi (61) baada ya Simba Sc (75) lakini takwimu za uchangiaji za mabao kutoka kwa viungo wao washambuliaji hasa wa pembeni zilikuwa hafifu zaidi, kuanzia utengenezaji na umaliziaji.

Takwimu za wachezaji waliochangia zaidi magoli (magoli + asisti) zinaonyesha kuwa hakuna kiungo mshambuliaji wa Yanga Sc aliyechangia mabao mengi kiasi cha kuweza kuingia hata kwenye 5 bora kuungana na mshambuliaji wao Fiston Mayele aliyechangia mabao 20, tofauti na Simba ambayo imeingiza wachezaji watatu, Saidi Ntibanzokiza (27), Clatous Chama (19) na Moses Phiri (13).

2. Mabeki wa pembeni

Kweli Yanga imekuwa na mabeki bora zaidi wa pembeni, lakini kuanzia katikati ya msimu kuja mwishoni tuliona Nabi akiwatumia zaidi Kibwana na Job Kwenye nafasi ambazo kiuhalisia zilikuwa na watu waliokuwa bora, Djuma Shaban na Joyce Lomalisa na David Bryson kushoto, hii inatoa tafsri ya kuwa eneo hilo linahitaji zaidi maboresho.

Mahitaji

Ili kuweza kupunguza mapungufu Yanga inahitaji;

1. Viungo washambuliaji bora ambao ni hatari zaidi kiufundi, kimbinu na kitakwimu na siyo machachari pekee, kwenye hili tayari hatua ya kwanza ya kuachana na viungo wengi wa pembeni imefanyika kama Tuisila Kisinda, Bernard Morisson, Dickson Ambundo na bado wengine huku wakiendelea kuwaacha au kuwatoa kwa mkopo ili kusajili wengine.

2. Kuwatoa kwa mkopo wachezaji walioshindwa kuonyesha makali yao ambao mikataba yao haujaisha na kusajili wengine ambao wanaweza kuongeza changamoto na kuongeza ushindani wa namba kwenye uwanja wa mazoezi ili kuongeza upana wa kikosi.

3. Kufukia mashimo ya watu muhimu na bora walioondoka kwenye timu kuanzia kwenye benchi la ufundi na wachezaji mfano makocha (kocha mkuu ameshaletwa), kiungo mshambuliaji mwenye ubora kama au unaokaribiana na wa Feisal Salum aliyeuzwa Azam Fc.

SIMBA SC

Simba ni timu yenye takwimu bora za wachezaji na nyingi za timu zaidi kwenye ligi kuu ya NBC (NBCPL)

wa benchi la ufundi

Ni wazi kuwa Simba kutoshinda mechi nyingi pia kumetokana na udhaifu wa benchi la ufundi, aidha mabadiliko ya kubadili makocha wakati msimu unaendelea au Ubora wa wataalamu wanaoajiriwa kwenye benchi la ufundi.

Mabadiliko ya mara kwa mara ya wakufunzi kwenye benchi la ufundi hubadilisha na kuharibu mtiririko sahihi ya mafunzo wanayopewa wachezaji, mfano kubadili kocha mkuu katikati ya msimu kuondoka kwa Kocha mkuu Zoran Maki na kuacha timu ikikaimiwa na Suleiman Matola ambaye alimpa kijiti Juma Mgunda hadi baadae alipokuja Roberto Oliveira, kunakua na utofauti wa mbinu wanazofundishwa wachezaji kutoka kwa kocha mmoja kwenda kwa kocha mwingine kila mwalimu ana staili yake ya uchezaji, mifumo na hata uchaguzi wa wachezaji wanaoshabihiana na mbinu zake.

Lakini kubadiliwa kwa wataalamu wengine kwenye benchi la ufundi kama kocha wa makipa, madaktari na mtaalamu wa viungo kunaweza kuwa kulichangia mabadiliko Kwenye hali za wachezaji kuanzia utimamu wa mwili na hata aina ya mazoezi wanayopewa kutoshabihiana na mbinu za waalimu tofauti.

Hivyo kubadilika kwa wakufunzi kulisababisha wachezaji kulishwa mbinu tofauti ndani ya msimu mmoja, mabadiliko ya utimamu wa mwili kiasi kwamba wengine walifikia hatua ya kupata majeraha ya mara kwa mara na hata kuathiri viwango vya wachezaji na mwisho huathiri mwendelezo wa matokeo ya timu.

3. Udhaifu kwenye dirisha lililopita la usajili

Ni wazi kuwa maingizo mengi ya wachezaji kwenye madirisha mawili ya msimu jana (dirisha kubwa la mwezi Juni 2022 na disemba 2022) yalikua na mapungufu mengi ndio maana asilimia kubwa ya wachezaji waliosajiliwa Kwenye dirisha lile walishindwa kufaulu ndani ya Simba kama Nelson Okwa, Victor Akpan, Augustine Okrah, Mohamed Outara, Ismael Sawadogo.

Hapa kuna mapungufu ya aina mbili, aidha wachezaji waliosajiliwa hawakuendana na mahitaji ya kiufundi ya Simba au waliosajiliwa walikua na matatizo ya kiafya wakaandamwa na majeraha ya mara kwa mara.

Mahitaji

1. Kuongeza idadi kubwa ya wachezaji wenye ubora mkubwa ili kuongeza upana wa kikosi chao, hii ikiwa sambamba na kujaza nafasi zilizoachwa na wachezaji walioachwa hasa wa kigeni.

2. Kuimarisha benchi la ufundi kwa kuajiri kocha bora wa makipa, kocha bora wa viungo, mtaalamu bora wa kuchua misuli ambao watasaidiana na Rorbeto Oliviera ili kujaza nafasi za wale walioachwa.

3. Kuimarisha idara ya usajili na Kazi zake, kuanzia aina ya wachezaji wanaowasajili kwa kuzingatia mahitaji muhimu ya kiufundi, vipimo vya afya kuepuka kusajili wachezaji wenye hatari la kuwa na wimbi la majeraha.

4. Kuepuka kubadilika hovyo kwa wataalamu wa benchi la ufundi.

SOMA NA HII  MWAMBA HUYU HAPA KUTOKA CHIPOLOPOLO AIUNGA MKONO POWER DYNAMO DHIDI YA SIMBA