SIMBA iko nchini uturuki ilikokita kambi maalumu ya kujifua kwaajili ya msimu ujao iliopanga kufanya mapinduzi na kurejesha ufalme wake uliotwaliwa na watani zao wa jadi Yanga kwa misimu miwili iliyopita.
Wakati ikiendelea kujifua kule uturuki, ndani ya kikosi cha Simba kuna sura mpya za makocha na wachezaji lakini pia yupo kijana David Kameta ‘Duchu’ aliyerudi msimbazi baada ya kukaa nje ya kikosi hicho kwa misimu miwili.
Duchu alisajiliwa na Simba kwa mara ya kwanza msimu wa 2020/2021 akitokea Lipuli, lakini alidumu kikosini hapo kwa msimu mmoja kabla ya kupelekwa kwa mkopo Biashara United kisha Geita Gold na baadae Mtibwa Sugar.
Baada ya misimu miwili mbali na jezi ya Simba, sasa amerejea kwa wakali hao wa Msimbazi tena na amepewa kandarasi ya miaka mitatu huku wenye Simba yao wakiamini ameiva sasa tayari kwa kuwatumikia kwa asilimia 100.
Kupitia Makala haya, hizi ni sababu tano ambazo zimemfanya Duchu kurejea Simba kwaajili ya msimu ujao na endelevu.
MAHITAJI
Simba katika nafasi anayocheza Duchu (Beki wa kulia) kuna mabeki wawili asilia, Shomari Kapombe na Israel Mwenda lakini pia Jimmyson Mwanuke mara kadhaa amekuwa akicheza eneo hilo kama kiraka.
Hata hivyo, Kapombe ndiye anaonekana kujitengenezeaq utawala katika eneo hilo kulingana na Mwanuke na Mwenda kushindwa kuonyesha ushindani mkubwa kwake.
Hivyo Simba ilihitaji beki atakayetoa ushindani kwa Kapombe ambapo kwa wazawa, Duchu ni miongoni mwa wachezaji waliokuwa bora katika misimu miwili iliyopita na wanaweza kutoa ushindani kwa Kapombe na hata kuwa mbadala bora katika eneo hilo.
UBORA
Jambo lingine lililochagiza Duchu kurejea Simba ni ubora aliounyesha tangu ametolewa kwa mkopo hadi msimu uliopita akiwa Mtibwa.
Kumekuwa na uchache wa mabeki wa kulia nchini wenye muendelezo wa ubora wao kwenye ligi hususani vijana.
Wengi wamekuwa wachezaji wa msimu mmoja na misimu mingine wanazingua lakini Duchu ubora wake umekuwa na muendelezo na kila uchwao anaonekana kuimarika zaidi jambo lililowashawishi Simba kumrejesha kundini na kuachana na dili nyingine.