Home Habari za michezo UNAWAJUA WACHEZAJI WALIOANZA MSIMU VIBAYA, MAJANGA HAYA HAPA

UNAWAJUA WACHEZAJI WALIOANZA MSIMU VIBAYA, MAJANGA HAYA HAPA

Tetesi za usajili Simba

Miongoni mwa mambo ambayo yamekuwa yakitibua mipango ya makocha wengi kwenye soka ni pamoja na majeraha ya wachezaji muhimu ambao wamekuwa kwenye mipango yao, muda mwingine timu hubidi kuingia sokoni ili kupata mchezaji ambaye anaweza kuwa mabadala.

Unakumbuka msimu uliopita baada ya Abuutwalib Mshery ambaye alikuwa mabadala wa Djigui Diarra kupata majeraha? licha ya kuwa na Erick Johora iliwabidi kuingia sokoni wakati wa dirisha dogo na kumsajili kwa mkopo Metacha Mnata aliyekuwa Singida Big Stars.

Simba nao ndani ya msimu huo baada ya kuumia kwa mshambuliaji wao tishio Moses Phiri iliingia sokoni na kumsajili Jean Baleke ambaye alibeba vyema safu ya ushambuliaji ya wekundu huo wa Msimbazi.

Ishu ya majeraha kwa wachezaji huwaumiza sana kichwa makocha na kuwa na wakati mgumu mno kipindi ambacho dirisha la usajili linakuwa limefungwa, huwabidi kutafuta suluhu kulingana na wachezaji walipo hapo ndipo unakuja umuhimu wa kuwa na kikosi kipana.

Leo kwenye Spoti Mikiki tunakuletea wachezaji sita ambao wamekuwa na mwanzo mbaya wa msimu kutokana na kusumbuliwa kwao na majeraha mbalimbali, wapo ambao waliumia mwishoni mwa msimu uliopita na wengine wakati wa maandalizi lakini pia wapo ambao majanga yamewakumba kwenye michezo ya mwanzoni.

SKUDU MAKUDUBELA Siku chache zilizopita Yanga ilithibitisha kuwa winga wake Mahlatse Makudubela ‘Skudu’ ameondoka nchini na kurudi kwao Afrika Kusini kwa ajili ya kushughulikia zoezi la kupata hati mpya ya kusafiria.

Lakini kabla ya safari hiyo ikumbukwe kuwa winga huyo alikuwa anasumbuliwa na majeraha ambayo aliyapata kwenye mchezo wa ngao ya jamii dhidi ya Azam FC ambao Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-0.

“Skudu aliumia tulipokuwa Tanga, lakini tayari alishaanza mazoezi mepesi kurejea kwenye timu. Kocha akaona ampe ruhusa muda huu kwenda kushughulikia hati yake ya kusafiria ili kukwepa usumbufu wa safari baadae. “Hati yake ya kusafiria ya sasa hivi inaelekea kujaa hivyo kumpa nafasi ya kupumzika kupona vizuri amepewa na ruhusa ya kusafiri kulimaliza na jambo hili la hati ya kusafiria haraka,” anasema Meneja wa klabu hiyo Walter Harrison.

Skudu ni miongoni mwa wachezaji wapya ambao wamebeba matumaini ya mashabiki wa timu hiyo lakini ndio hivyo majeraha yamemfanya kukosa michezo ya mwanzoni mwa msimu ikiwemo wa Jumatano ambao Yanga ilicheza dhidi ya wakusanya mapato wa Kinondoni, KMC.

HENOCK INONGA Inonga amerudi kwao DR Congo baada ya kuumia bega katika mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Singida Fountain Gate hivyo Simba ilianza kukosa huduma yake tangu mechi ya fainali dhidi ya Yanga ambapo wekundu hao wa Msimbazi walitwaa taji hilo kwa penalti 3-1.

Baada ya fainali hiyo, Inonga ambaye atakuwa nje ya uwanja kwa wiki mbili aliondoka nchini na kurudi kwao kwa matibabu zaidi huku timu yake ikianza mikiki ya Ligi Kuu Bara kwa kucheza dhidi ya Mtibwa Sugar na Dodoma Jiji na kuvuna pointi zote sita.

Katika mechi mbili ambazo Simba imecheza nafasi yake amekuwa akicheza Kennedy Juma anayesimama na Che Malone.

“Mara nyingi wachezaji wanapopata majeraha na kama mapumziko ya kutibiwa yatachukuwa muda kidogo, basi huomba ruhusa ya kwenda kwao kwa matibabu zaidi. Hivyo atakuwa huko kwa muda wote aliopewa labda kuwepo na mabadiliko mengine,” anasema Ahmed Ally Mkuu wa kitengo cha Habari na Mawasiliano cha Simba.

AUBIN KRAMO Mashabiki wa Simba wanahamu ya kumuona Aubin Kramo akicheza kwenye kikosi chao lakini kupata kwake majeraha wakati wa maandalizi ya mechi dhidi ya Singida Fountain Gate kumemfanya asionekane kwenye michezo miwili ya Ligi Kuu Bara.

Msimu uliopita kwenye mechi za makundi ya Kombe la Shirikisho, Kramo aliupiga mwingi na kufunga mabao manne katika mechi tatu kati ya sita za hatua hiyo na timu hiyo kutolewa nusu fainali na USM Alger ya Algeria iliyobeba ndoo kwa faida ya bao la ugenini mbele ya Yanga.

VICENT ABOUBAKAR KMC inaweza kukosa huduma ya nyota huyu kwa zaidi ya wiki sita kutokana na kusumbuliwa na majeraha ya muda mrefu.

Ofisa habari mpya wa KMC, Khalid Chukuchuku amethibitisha hilo kwa kusema,”Tulikuwa na wachezaji wawili ambao walikosekana kwenye mchezo wetu uliopita dhidi ya Yanga ambao ni Andrew Vicent ambaye kwa sasa amerejea kikosini na Vicent Aboubakar ambaye ataendelea kuwa nje ya uwanja kutokana na aina ya majeraha aliyonayo.”

Aboubakar ambaye alivunjika na kuwekewa ‘ogo’ atakaporejea atakuwa na kibarua upya cha kupigania namba kutokana na kikosi hicho kuwa chini ya kocha mpya, Abdihamid Moalin.

AISHI MANULA Miezi mitatu iliyopita kipa namba moja wa Simba na Taifa Stars, Aishi Manula, alifanyiwa upasuaji Afrika Kusini alipoenda kwa ajili ya matibabu ya majeraha ya nyama za paja.

Manula aliondoka nchini Jumatatu (Mei 29) akiongozana na daktari wa klabu yake Edwin Kagabo kwa ajili ya kwenda kupata matibabu kutokana na jeraha lililomweka nje kwa muda mrefu.

Manula aliumia kwenye mchezo wa Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ walipocheza dhidi ya Ihefu kwenye Uwanja wa Azam Complex Aprili 7 mwaka huu, na tangu hapo alikuwa nje ya uwanja huku kipa aliyekuwa chaguo la tatu, Ally Salim akicheza kwenye michezo iliyofuata.

Kulingana na ushiriki wa Simba kwenye michuano ya kimataifa huku wakimpoteza Beno Kakolanya ambaye alitua Singida FG, iliwabidi kuingia sokoni ili kuzipa pengo hilo ndio maana wakasajiliwa Husseni Abeli na Ayoub Lakred. Manula ataendelea kukosekana kwenye kikosi hicho kwa zaidi ya wiki sita.

MALICKOU NDOYE Kipindi kama hiki mwaka jana, Azam FC ilifunga usajili wake kwa kumtambulisha beki wa kati, Malickou Ndoye aliyekuwa na umri wa miaka 22 kutoka Teungueth ya kwao, Senegal.

Ndoye ambaye anasumbuliwa na majeraha alifanya Azam kuwa na jumla ya wachezaji tisa wapya, akiwemo kipa Mcomoro mzaliwa wa Ufaransa, Ali Ahamada, Kipre Junior, Tape Edinho kutoka Ivory Coast.

Pamoja na kusumbuliwa kwake na majeraha Ndoye amekuwa na wakati mgumu kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo hata hivyo kwa sasa anaonekana kuwa na matumaini ya kupata nafasi chini ya kocha mpya, Youssouf Dabo.

WASIKIE WADAU Nahodha wa zamani wa Friend Rangers, Boniface Nyagawa anaamini Simba ndio wanaweza kuathiriwa na majeruhi ya Inonga kuliko Skudu kwa Yanga kutokana na ubora ambao amekuwa akiuonyesha beki huyo.

“Alikuwa ameanza kuwa na maelewano mazuri ya kiuchezaji na Che Malone sasa kocha atakuwa na kazi nyingine ya kufanya kuhakikisha wanatakuwa sawa. Yanga wapo na watu wenye ubora wa kucheza maeneo ya pembeni sioni kama kuna shida watakumbana nayo,” anasema.

Kwa upande wake, Jumanne Kibwana ambaye ni mwanachama wa Yanga, ameumizwa na kuumia kwa Skudu, akisema: “Kwa kile ambacho alikionyesha kwenye kilele cha wiki ya Mwananchi ni wazi kuwa ndiye nyota wetu mpya baada ya kuondoka Mayele, anavitu mguuni sisi Yanga tunataka ushindi na burudani.”

SOMA NA HII  BAADA YA KUFUNGWA MAGOLI YA KIZEMBE...'NDOA' YA SHIKHALO NA MTIBWA YAVUNJIKA RASMI...