Home Uncategorized MANULA BOMU KWETU, HUKU WENYE MPIRA WAO WANAMUONA YUKO VIZURI

MANULA BOMU KWETU, HUKU WENYE MPIRA WAO WANAMUONA YUKO VIZURI


Na Saleh Ally, Cairo
KUNA kikundi cha wataalamu wa kutafuta wachezaji kwa ajili ya timu mbalimbali za ligi za Ulaya hasa kutokea katika nchi za Kaskazini mwa Ulaya, wako hapa nchini Misri kwa kazi maalum.

Nchi za Sweden, Denmark, Norway na nyinginezo zikiwemo maalum kama Ubelgiji, Ufaransa na kadhalika wako hapa kufuatilia baadhi ya wachezaji wakichukua takwimu zao.

Huu ni utaratibu wa kawaida wa klabu zilizo katika nchi hizo kwa kuwa wanajua michuano ya Afcon inakutanisha ‘cream’ ya Afrika. Yaani wachezaji bora katika kila nchi wanaunda timu zao za taifa kuja kupambana kuonyesha ubora hadi bingwa anapatikana.

Wataalamu hawa si mawakala, ni wataalamu wa kazi hiyo wakiwa wana elimu kubwa ya ukocha lakini wanajua namna gani mchezaji bora anakuwa.

Kumjua mchezaji bora pia ni elimu, ndio maana unaona kuna wachezaji wanachukuliwa na kupikwa. Watu hawa wanaona mbele ya mchezaji kuna nini na ndio maana ananunuliwa kwa bei ya kawaida wakijua baadaye atakuwa bora na kuwa biashara kubwa.

Kwa kuwa nilikaa eneo la watu maalum VIP wakati wa mechi kati ya Tanzania, wako walitaka msaada wangu kuhusiana na wachezaji wa Tanzania. Wakanitajia baadhi ya majina yao, kati ya hao hawakuwa wamemuorodhesha Aishi Manula, kipa namba moja aliyekuwa langoni.

Kufikia dakika ya 67 ya mchezo, wakaanza kuniuliza maswali mengi kuhusiana na Manula ikiwemo akademi anayocheza lakini hata kipa anayemfundisha katika klabu ya Simba anatokea wapi, ni nani na pia wakataka kujua kuhusiana na kocha anayemfundisha timu ya taifa.

Wao ndio walikuwa wa kwanza kuhoji vipi Manula anacheza akiwa ameumia. Waliamini alitakiwa kutolewa mapema na kusisitiza, tatizo kubwa la Afrika, wachezaji wengi hawachezi muda mrefu kwa kuwa hucheza dakika nyingi za mechi walizocheza wakiwa na maumivu ambayo yasingekuwepo kama wangekuwa wakipumzishwa kwa wakati.

Walinieleza ubora wa Manula na ubora wake wakisisitiza alikuwa bora kuliko kipa wa Kenya siku hiyo. Wakanieleza makosa ya mabeki yaliyokuwa yakimuathiri na yeye pia alionekana kutoyang’amua.

Wakasisitiza kuhusiana na uzoefu na kusisitiza anaweza kuwa bora zaidi kama atapata kocha bora hasa au kutoka nje ya Tanzania kwa kuwa wanamuona bado ni mdogo na ana nafasi ya kukua.

Mazungumzo yao na mimi yalinifanya nitafakari. Wakati naondoka nilikutana na watalaamu hao wanaotokea Ufaransa ambao pia walitaka kujua zaidi kuhusiana na Simba, kama mechi zote za Ligi ya Mabingwa Afrika alicheza yeye au la.

Sitaki kusema katika mechi dhidi ya Kenya Manula hakukosea, lakini nataka nikukumbushe kwamba Watanzania ndio tumeongoza kwa kumbeza Manula baada ya Stars kufungwa mabao 3-2 ikiwa imetangulia.

Kosa moja la kudondosha mpira na Michael Olunga akapiga tik tak. Hili ni kosa lake ndio, lakini nani alilirekebisha katika msitu wa wachezaji wa Tanzania? Hivyo ni kosa la pamoja.

Ukiangalia mechi hiyo, Manula ameokoa mara nyingi zaidi ya kipa wa Kenya kutokana na kwamba mashambulizi mengi yalipenya kwenye ngome ya Stars.

Angalia mashuti matatu akiwa uso kwa uso na mshambulizi amedaka kabisa. Lakini Watanzania ndio wamemshambulia huku Wakenya wakijifisia na kumsifia kuwa ameiokoa sana nchi yake.

Takwimu za Caf na runinga ya BeinSport zimefanana kabisa, sijajua kama wanachukua sehemu moja nazo, zikanithibitishia kile walichokiona wale wasaka wachezaji kutoka klabu mbalimbali walichokiona kilikuwa sahihi.

Takwimu zinaonyesha ubora wa Manula ulikuwa juu kuliko Patrick Matasi wa Kenya ambaye timu yake ilishinda. Wastani wa Manula kuokoa mashuti ulikuwa ni asilimia 73.7 wakati Matasi ni 55.6%, sisi hatuoni.

Manula aliokoa michomo hatari saba langoni mwake, Matasi akaokoa mitano. Lakini bado tunambeza na huenda tunapaswa kujifunza kwamba, suala la kubeza pia limekuwa ni anguko letu katika soka kwa miaka 39.

Miaka 39 bila kucheza Afcon, si jambo dogo na haliwezi kuwa na sababu moja pekee. Angalia leo ndio tumerejea lakini tunatamani kuwa Misri, Cameroon au Senegal katika mashindano ya kwanza.

Lawama ni msingi wa maisha ya wapenda mpira kwa kuwa sote tunaamini tunajua sana. Hatutoi nafasi ya pongezi kwa kuwa tunaamini kukosoa ni kuonyesha tunajua sana, jambo ambalo ni bovu sana.

Anayejitahidi kwa uwezo wake wote, anapolaumiwa ‘hufa’ mapema kabisa. Maana anakuwa haoni kitu sahihi cha kufanya kama kila anachofanya kinaonekana hakina faida.

Manula anaonekana hadi na Wakenya kwamba alifanya vema licha ya ukweli wanaona hakuna uzoefu na hilo lina ukweli. Lakini Watanzania tunaamini yeye ndiye alikuwa tatizo.

Ukiangalia wachezaji wetu wamejitahidi sana “kunyenyemea” kutokana na uwezo wao. Mfano katika takwimu walizotoa Caf na BeinSPorts za mechi hiyo, zinaonyesha Himid Mao alicheza vizuri zaidi katika baadhi ya vitengo zaidi ya Victor Wanyama.

Hawa hawapendelei na ni watalaamu hasa. Ukiangalia takwimu si kila sehemu Himid amezidiwa na Wanyama. Lakini hili kwa Watanzania unaweza kuwa ubishi wa mwaka mzima bila ya “half time”.

Takwimu zinasema hivyo kwamba hata ubora wa basi, Himid alikuwa bora zaidi ya Wanyama. Lakini utaona pasi muhimu za Wanyama zilikuwa na ubora zaidi. 

Himid kazuia wenyewe wanasema blocks mashuti mengi zaidi kuliko Wanyama kwa maana ya wastani na huye ni holding midfield bora wa siku.

Leo Saimon Msuva na Mbwana Samatta wako kwenye wafungaji waliofunga mabao angalau moja moja. Lakini wako washambulizi kibao na nyota ambao hawajafunga hata bao moja.
Tanzania ni kati ya nchi chache zilizofikisha mabao mawili kabla ya mechi za jana. Lakini hakuna Mtanzania anayeweza kuona hilo kwamba kuna sehemu ya mwanzo na sasa tunaweza kusonga.

Tunaweza kujifunza mambo mengi baada ya kuanza kujifunza. Yote hata tunasema kwa kuwa tumekuja Afcon. Isingekuwa hivyo, kusingekuwa na mjadala, basi itakuwa vizuri tukijenga huku tukionyesha thamani kwa wale wanaotupigania.

TAKWIMU
Manula:
Mechi alizocheza: 2
Dakika alizocheza: 180
Mabao ya kufungwa: 5
Kuokoa kwa wastani wa dakika: 7
Mashuti aliyookoa langoni: 7
Mashuti aliyookoa kwa wastani: 73.7%


Matasi:
Mechi alizocheza: 2
Dakika alizocheza: 180
Mabao ya kufungwa: 4
Kuokoa kwa wastani wa dakika: 2.5
Mashuti aliyookoa langoni: 5
Mashuti aliyookoa kwa wastani: 55.6%


Wanyama:
Mechi alizocheza: 2
Dakika alizocheza: 180
Pasi alizopiga: 100
Uhakika wa pasi: 78%
Kuvuruga mipango: 1
Tackles alizofanikiwa: 4


Himid: 
Mechi alizocheza: 2
Dakika alizocheza: 128
Pasi alizopiga: 52
Uhakika wa pasi: 78.8%
Kuvuruga mipango: 4
Tackles alizofanikiwa: 5


Olunga:
Mechi alizocheza: 2
Dakika alizocheza: 180
Nafasi alizotengeneza: 2
Krosi alizopiga: 2
Uhakika wa mashuti: 75%
Faulo alizocheza: 1

Samatta:
Mechi alizocheza: 2
Dakika alizocheza: 180
Nafasi alizotengeneza: 1
Krosi alizopiga: 0
Uhakika wa mashuti: 80%
Faulo alizocheza: 6:

WAFUNGAJI:
Mickaël Poté  (Benin)   2
Michael Olunga (Kenya) 2
Emmanuel Okwi (Uganda) 2
Andre Ayew (Ghana) 1
Mbwana Samatta (Tanzania)  1
Jordan Ayew (Ghana) 1
Yaya Banana (Cameroon) 1
Saimon Msuva (Tanzania) 1
Djalma (Angola) 1
Stephane Bahoken (Cameroon) 1

TIMU NA MABAO YA KUFUNGA:
MABAO MATATU:
Mali, Algeria, Misri, Kenya, Madagascar na Uganda.

MABAO MAWILI: 
Benin, Cameroon, Tanzania, Senegal, Nigeria, Guinea, Ghana na Tunisia.

BAO MOJA:

Angola, Zimbabwe, Afrika Kusini, Ivory Coast na Mauritania.
SOMA NA HII  HIVI NDIVYO AZAM FC ILIVYONYOOSHWA NA SIMBA DAKIKA 450