Home Habari za michezo KWA PIRA HILI LA GAMONDI HATARI

KWA PIRA HILI LA GAMONDI HATARI

Habari za Yanga leo

Wakati Nabi alipotangaza kuondoka Yanga na kisha benchi lake zima la ufundi likamfuata katika mlango wa kutokea pamoja na straIka kinara Fiston Mayele, wengi walitaka kujua warithi wao watafanya nini cha kuweka alama – lakini kama kuna chochote basi hili pira nyonya damu la Miguel Gamondi linatisha!

Nabi alifahamika kwa soka la pasi, sub zake zenye matokeo chanya na makombe, wakati Mayele alifahamika kwa mabao yake na jihad uwanjani, hivyo haikushangaza mashabiki kujiuliza ni kipi warithi wao watafanya cha kuwafurahisha Wananchi.

Lakini kama hiki ambacho Yanga wameonyesha katika mechi tano kubwa za michuano yote (ikiwamo moja ya kirafiki dhidi ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini) ni kivuli cha picha halisi ya kile ambacho Wananchi watarajie kutoka kwa mastaa wao, basi mwaka huu moto utawaka.

Yanga imecheza mechi tano bila ya kuruhusu bao, ikifunga jumla ya mabao 10-0 huku pia ikiwanyima wapinzani hata nafasi ya kupiga mashuti langoni mwao. Hii inatisha.

Licha ya kutema taji moja la Ngao ya Jamii ambalo ililishikilia katika misimu miwili ya Nabi na Mayele, lakini Yanga haikufungwa bao lolote katika mechi za Ngao ya Jamii ambazo kwa mara ya kwanza msimu huu zimefanyika kwa mtindo wa mtoano ikishirikisha timu nne zilizomaliza juu katika Ligi Kuu Bara msimu uliopita.

Mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara walitema Ngao kwa penalti 3-1 dhidi ya mahasimu wao Simba, ambao bahati, ushujaa wa kipa Ally Salim, upigaji mbovu wa penalti wa Yanga na makosa ya waamuzi viliwabeba Wekundu wa Msimbazi pale Mkwakwani, Tanga.

Yanga ilitawala mechi ile dhidi ya Simba na iliutumbukiza mpira wavuni mara mbili (zote zikakataliwa kwa kuotea) huku Wananchi wakipiga mashuti 11, matano yaliyolenga lango na sita yaliyoenda nje, wakati Simba ilipiga shuti moja tu lililolenga lango katika dakika zote 90 na jingine moja tu lililoenda nje ya lango la Yanga katika mechi ya fainali ambayo Wekundu wa Msimbazi walibanwa kwelikweli.

Kiujumla, wachezaji wa Simba walinyimwa kukaa na mpira, kuufurahia na hata kuweka mipango yao kwani Yanga walikuwa wepesi kuunyang’anya haraka ulipoondoka katika himaya yao.

Ungeweza kusema Yanga walichofanya ni kama vile walijiona ni wao tu ndio waliokuwa na haki ya kukaa na mpira – ukiuchukua wanakuvamia haraka na kuurudisha katika himaya yao.

Na haikushangaza kocha Robertinho alipolazimika kumtoa supastaa na mpishi mkuu wa mabao ya Simba, Clatous Chama pamoja na kipenzi wa Wanamsimbazi Luis Miquissone ambao walipotezwa na beki Yao Kouassi. Hata mashabiki wa Simba walionekana kutofurahishwa na hali ile ya kuwaona “Yanga wanakuja tu” kulishambulia lango lao.

Kwenye Ngao ya Jamii, Yanga ilianza na Azam. Wananchi walichowafanya Azam kila mtu aliona. Wanalambalamba walikula 2-0 na mpira waliusaka. Kumbe ile ilikuwa trela tu na wengi walisubiri kuona Yanga itachezaje dhidi ya Simba.

Lakini baada ya kurudia kile ilichokifanya dhidi ya Azam kwa kuwanyima Wekundu wa Msimbazi kufurahia mpira kwa kuwanyang’anya haraka, Yanga ya Gamondi imeanza kupata utambulisho wake – pira nyonya damu.

Na pira nyonya damu lilionekana dhidi ya Asas ya Djibouti katika mechi yao ya hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo Yanga ilishinda 2-0 Jumapili iliyopita kisha KMC juzi walionja ladha mbaya zaidi ya pira nyonya damu kwasababu mabao yalikuwa yakimiminika nyavuni wakala mabao 5-0 huku timu hiyo ya Manispaa ya Kinondoni ikipiga shuti moja tu lililolenga lango.

Simba ilipiga shuti moja lililolenga lango, Asas shuti 0, KMC shuti moja na Azam ilikiona cha moto. Kama hiki tulichokishuhudia katika mechi tano ikiwamo ya kirafiki dhidi ya Kaizer Chiefs iliyolala 1-0 katika kilele cha Wiki ya Mwananchi, kama ndio staili mpya Yanga, msimu huu nyasi zitawaka moto. Kama hili pira nyonya damu ndio staili halisi ya Gamondi, basi wapinzani wajipange.

MAGOLI YAMEGAWANYWA

Kwa misimu miwili iliyopita, Yanga ilitegemea magoli ya Mayele zaidi, lakini katika mechi hizi chache za msimu huu magoli yanaonekana kugawanywa kwa wachezaji, japo Aziz Ki anaonekana kufunga mara kwa mara.

Inaweza kuwa ni mapema sana kusema chochote, lakini dalili za mvua ni mawingu. Msimu huu katika mabao hayo 10-0 ni Aziz Ki na Musonda ndio wenye mengi (3&2) mtawalia, wakati dhidi ya KMC mabao yalifungwa na watu watano tofauti.

Licha ya kwamba mabao 10 ambayo Yanga imefunga katika mechi tano ni wastani wa mabao mawili tu kwa kila mechi, lakini staili yao ya uchezaji ya kumnyonya damu mpizani, kutoruhusu mabao, kutoruhusu mashuti yapigwe langoni mwao na kutengeneza nafasi nyingi za hatari, ni vitu ambavyo vinapaswa kuwashtua zaidi wapinzani.

Yanga kwa muda mrefu imekuwa ikikosolewa kwa kushindwa kuwashindilia mabao mengi wapinzani wao hata pale inapotokea imewashika kisawasawa tofauti na mahasimu wao Simba ambao ukijichanganya ukaingia kwenye “mfumo” wanakudhalilisha kwa mvua ya mabao.

Lakini kama kipigo cha juzi ni ishara ya zama mpya za kutumia vyema nafasi zinazotengenezwa na mafundi wengi waliojaa katika eneo la kiungo la Yanga, basi wapinzani watapaswa kujichunga zaidi.

PACOME, YAO & MAXI

Viwango vya nyota wapya katika mechi hizi chache vimewavutia wengi na kutabiriwa makubwa kama wataendelea hivi.

Aziz Ki alikuwa na kiwango cha kupanda na kushuka, lakini msimu huu anaonekana kuanza vyema akicheza tofauti ikiwamo kurudi nyuma kusaidia ulinzi.

Pacome Zouzoua, MVP wa Ligi Kuu ya Ivory Coast msimu uliopita, alichelewa kujiunga na Yanga na juzi alipoanzishwa kwa mara yake ya kwanza aliiteka shoo kwa pasi zake, kuhaha karibu uwanja mzima, udambwidambwi mwingi na bao tamu la kiufundi baada ya kumchekecha beki mmoja kabla ya kuuchopu mpira juu ya kipa akimalizia asisti ya Maxi Nzengeli.

Na huyu Maxi kabla ya kumpa asisti Pacome, alipiga ‘turn’ moja la hatari sana kumtambuka mchezaji wa KMC na kuendeleza kile ambacho amekuwa akifanya katika mechi zote tangu ametua nchini na kuwavutia wapenda soka.

Yote hayo yamekuwa yakipata sapoti ya beki wa kulia mwenye mapafu ya mbwa, Yao Kouassi ambaye kazi yake imewafanya watu kumuita jeshi.

Kama hiki kilichofanyika katika mechi tano zilizopita, kikiendelezwa, moto utawaka!

SOMA NA HII  MUONEKANO WA UKURASA WA MBELE GAZETI LA CHAMPIONI JUMATANO