Home Habari za michezo NGAO YA JAMII KUONYESHA MBIVU NA MBICHI, SIO SIMBA SIO YANGA…… ISHU...

NGAO YA JAMII KUONYESHA MBIVU NA MBICHI, SIO SIMBA SIO YANGA…… ISHU IKO HIVI

MECHI ya Ngao ya Jamii ni kiashiria cha kuanza kwa msimu mpya wa Ligi Kuu katika mataifa mengi huku Tanzania ikiwa ni miongoni mwao.

Msimu wa soka wa mwaka 2023 na 2024 kwa Tanzania Bara unatarajia kuanza Jumatano huku kukiwa na utofauti baada ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kubadili kanuni na badala ya kucheza timu mbili, sasa zitacheza timu nne.

Badala ya kuchezwa mechi moja kama ilivyoada, sasa kutakuwa na jumla ya mechi tatu, ambapo Yanga itacheza dhidi ya Azam FC Jumatano Agosti 9, huku Simba wakicheza dhidi ya Singida Fountain Gates siku inayofuata.

Washindi wa kila mchezo watakutana katika fainali ya Ngao ya Jamii na mshindi ndiye atakabidhiwa taji hilo.

KANUNI MPYA

Kanuni ya 19 kifungu cha kwanza inasema: Kutakuwa na shindano maalumu la ufunguzi wa ligi (Ngao ya Jamii) litakaloshirikisha timu tatu za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu na timu bingwa wa Kombe la Shikirisho.

Inaeleza kuwa endapo bingwa wa Kombe la Shirikisho atakuwa miongoni mwa timu tatu za juu, basi timu iliyoshika nafasi ya nne kwenye ligi ndio itaongezeka.

Na ndio maana zilichaguliwa Simba, Yanga, Azam FC ambao walikuwa wanaongoza tatu za juu na nafasi ya nne ilikuwa ni Singida Big Stars ambao kwa sasa wanajulikana kama Singida Fountain Gates.

Timu hizi zitacheza hatua ya mtoano, itaanza Yanga na Azam mmoja ataingia fainali akimsubiri mshindi kati ya Simba na Singida katika michezo itakayochezwa Jumatano na Alhamisi. Kutakuwa na mshindi wa kwanza, wa pili na tatu.

MATAMANIO

Mashabiki wa timu zote nne watakuwa wanaelekeza macho yao mkoani Tanga na wengine wataenda kuzishangilia.

Kwanini huko, kwa sababu zinakutana timu nne zilizofanya vizuri kwenye ligi, Kombe la Shirikisho la Azam (FA) msimu uliopita lakini pia, ndio wawakilishi wa nchi kwenye michuano ya kimataifa.

Kila mtu atachezesha kikosi chake cha kwanza kitakachompa matokeo kwa maana bado watakuwa wakijitathmini kuona kuwa je, vikosi vyao vitaweza kushindana kwa namna gani kwa sababu kila mmoja amesajili kujipanga na msimu mpya.

Watu watakuwa wanatamani kuona vikosi vyao, usajili mpya na makocha wao wamejipangaje. Kuona watakavyofanya vizuri kuelekea kwenye mashindano yaliyoko mbele yao.

Watu watataka kuona nani ni bora kuliko mwingine, namna walivyokuwa wanatambiana nani atakuwa amefaulu nani atakuwa amefeli.

HASIRA ZAO

Kuna timu hapa zina hasira na zinataka kuanza kuonesha makali yao. Kwa mfano katika mechi ya Yanga dhidi ya Azam FC, unaweza kuwa mchezo wa kisasi na mgumu kwa sababu wametoka kuonewa na Yanga msimu uliopita.

Mara ya mwisho timu hizo zilikutana kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga katika fainali ya FA na Yanga kuibuka na ushindi wa bao 1-0.

Pia, katika ligi msimu uliopita Yanga ikiwa katika ubora wake ilinyakua jumla ya pointi nne kwenye michezo miwili ya mkondo wa kwanza na wa pili. Timu hizo zinakutana zikiwa na maboresho ya vikosi vyao na makocha wakiwa wapya.

Yanga kuna Kocha Miguel Gamondi kutoka Argentina aliyechukua nafasi ya Nasreddine Nabi huku upande wa Azam FC kukiwa na Youssouph Dabo kutoka Senegal aliyechukua nafasi ya Kally Ongalla.

Ni makocha ambao pengine kila mmoja atakuja na mfumo wake utakaoweza kumpa matokeo mazuri.

Pia, kuna wachezaji wametoka Yanga wamesajiliwa Azam FC kama Yanick Bangala, Feisal Salum wanaungana na wengine wapya kwenye kikosi cha Azam FC kama Allassane Diao, Gibril Silla na Cheikh Sidibe.

Mashabiki wa klabu hiyo watataka kuona kama usajili huo mpya utalipa hasa baada ya timu hiyo kushindwa kuchukua mataji kwa muda mrefu.

Usajili mpya wa Yanga kuna Nickson Kibabage, Jonas Mkude, Maxi Nzengeli, Gift Fred, Yao Kouassi, Mahlatsi Makudubela, Pacome Zouzoua na Hafiz Konkoni.

Na mashabiki wa Yanga pia bado wana shauku ya kuiona timu yao kama itaweza kufanya vizuri kama misimu miwili iliyopita. Hasa baada ya kuondokewa na wachezaji muhimu kama Fiston Mayele, Bangala, Djuma Shaban na wengine wakiwa wamemaliza mikataba.

Simba itacheza na Singida Fountain Gate. Wanaopewa nafasi kubwa ni wekundu wa Msimbazi. Wanakutana makocha wote ni wale waliokuwepo msimu uliopita.

Isipokuwa vikosi vya timu zote mbili vimeboreshwa. Simba imesajili wachezaji karibu 10 ambao ni Essomba Onana, Aubin Kramo, Che Malone, David Kameta, Fabrice Ngoma, Idd Chilunda, Abdallah Hamis, Hussein Kazi, Luis Miquissone na kipa wa Brazil Jefferson Luis anayetajwa kutemwa.

Kwa upande wa Singida kuna wachezaji kama Abdul Mangalo, Dickson Ambundo, Duke Abuya, Malouf Tchakei, Thomas Ulimwengu, Gadiel Michael, Joash Onyango, Morice Chuku na wengine.

Asilimia kubwa ya kikosi chao kina wachezaji wapya. Wengine waliwahi kucheza Simba kama Onyango, Gadiel na Meddie Kagere.

Katika mara mbili Simba ilizokutana na Singida msimu uliopita imechukua pointi nne. Mchezo mmoja walitoka sare ya bao 1-1 mkoani Singida na mwingine ilishinda 3-1 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Timu zote zitakutana zikiwa imara ingawa Simba bado anaweza kupewa nafasi kutokana na usajili wake. Timu zote hizo kwenye mechi za kirafiki zilifanya vizuri. Mwenye hasira hapo ni Singida ambaye alionewa msimu uliopita. Je, ataweza kulipiza kisasi? Je, Simba atakuja na kasi gani.

NYOTA

Bila shaka mashindano hayo yanaweza kuwaibua nyota wapya watakaotamkwa midomoni mwa mashabiki na wachambuzi wa soka.

Kwa maana ya wale watakaofanya vizuri kwa kufunga, kudaka, kutoa pasi na wenye mbinu mbalimbali za kufurahisha uwanjani. Pengine inaweza kuwa kati ya wachezaji wageni waliosajiliwa kwa timu zote au wale waliozoeleka au waliopo kwa muda mrefu.

HISTORIA

Mchezo wa Ngao ya Jamii ulianzishwa kwa mara ya kwanza mwaka 2001 kabla ya kusitishwa kwa miaka kadhaa na kurejea tena kuanzia mwaka 2009.

Msimu uliopita Yanga ilichukua Ngao ya Jamii mbele ya Simba baada ya kuwafunga mabao 2-1 katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam. Ulikuwa ni ubingwa wa pili mfululizo baada ya msimu wa mwaka juzi kuchukua tena.

Takwimu zinaonesha Simba na Yanga zimeshachukua zaidi ya mara nne kombe hilo. Wengine waliowahi ni Mtibwa na Azam FC kila mmoja mara moja.

Je, nani ataweka rekodi mpya msimu wa 2023? Nani atakuwa nyota wa mchezo. Nani atakuwa bingwa? Shangwe lote linahamia Tanga kwa muda mfupi kabla ya kuanza kwa msimu wa Ligi Kuu.

SOMA NA HII  MABASI KUTOKA AFRIKA KUTUMIKA KWA AJILI YA KOMBE LA DUNIA QATAR...FAINAL ZIKISHA YATAGAWIWA BUREEE...