Home Habari za michezo HII HAPA NDIO MITEGO MIWILI YA YANGA

HII HAPA NDIO MITEGO MIWILI YA YANGA

Habari za Yanga

Yanga haijaruhusu bao lolote mpaka sasa kwenye ligi na inachofanya ni kuendelea kushusha vipigo vyenye ujazo tofauti lakini mitego miwili inayowapa shida wapinzani imejulikana.

Ikiwa imecheza mechi tatu mpaka sasa Yanga haijapoteza mchezo wowote kama zilivyo klabu nyingine tatu pale juu chini yao za Simba, Azam na huku Mashujaa nao wakitamba baada ya kutofungwa hadi sasa.

Ilichojitofautisha Yanga na hizo timu tatu nyingine ni kwamba wao hawajaruhusu wavu wao kutikiswa ndani ya mechi hizo kama Mashujaa huku mfumo wa kocha wao Miguel Gamondi ukionyesha kuwabeba.

Gamondi amekuwa akitumia mfumo sawa na ule wa mtangulizi wake Nasreddine Nabi lakini Muargentina huyo akaufanyia maboresho kimtindo ambayo ndio yameiweka timu hiyo kwenye ubabe wanapokutana na timu pinzani.

Yanga inatumia mfumo wa 4-2-3-1 lakini ile nidhamu yao ya kukabia juu kuanzia washambuliaji wa mbele ndio kitu ambacho kinawasumbua wapinzani.

Mtego wa kwanza

Timu pinzani zinazokutana na Yanga zimekuwa katika mazingira magumu zinapoamua kupanga mashambulizi kuanzia golini kwao ambapo wakijaribu hilo tu washambuliaji wa mbele wa Yanga na viungo wao watatu wa nyuma ya mshambuliaji huanza kazi haraka ya kuusaka mpira.

Wachezaji hao wanne wamekuwa wakizilazimisha timu pinzani kupoteza mpira kwa haraka au kuamua kuutupa kwa kupiga mbele jambo ambalo ni faida kwa Yanga ambao haraka wataufanya mpira kuwa kwenye miliki yao.

Mtego wa pili

Hata unapokutana na timu itakayopaki basi kisha kuamua kucheza soka la mashambulizi ya haraka (kaunta) bado mfumo huo umekuwa mwiba kwa wapinzani ambapo haraka viungo wakabaji wawili na mabeki wao wanne wamekuwa tayari kukabili mashambulizi hayo kirahisi.

Ugumu kwa timu pinzani ni kwamba mashambulizi hayo yanahitaji idadi kubwa ya wachezaji kuweza kulikamilisha kitu ambacho huwa ni vigumu kuweza kuipangua ngome ya timu hiyo.

Ukuta kazi rahisi

Ukuta wa Yanga kwenye mechi zao 8 za mashindano tofauti waliyocheza wamekuwa wakikutana na kazi rahisi kuzima mashambulizi ya timu pinzani kwa kujikuta wanakabiliwa na mashambulizi rahisi kutoka kwa wapinzani.

Mashambulizi hayo yamekuwa yakizimwa kirahisi na mabeki hao au wakati mwingine kipa bora wa msimu wa pili mfululizo Djigui Diarra ambaye amekuwa imara kutoka na kwenda kuwa sehemu ya ulinzi akitumia ubora wake wa kujua kumilikia mpira na kucheza kwa miguu.

Msikie SMG

Kocha Said Maulid ‘SMG’ alisema Gamondi amefanikiwa kuijenga timu yenye ubora huo wa kisasa akimsifia pia kocha wa mazoezi ya viungo kuifanya kazi ya kocha huyo kuwa rahisi.

“Nadhani Gamondi amefanikiwa tena kwa nafasi kubwa, hatua ya kwanza unapoitazama Yanga utaona ni timu ambayo inataka wakati wote mpira uwe kwenye umiliki wao ndio maana unaona kama sio kuanza kukabia kule mbele basi timu pinzani hazitakuwa na muda mrefu wa kuuchezea mpira,” alisema SMG ambaye ni winga wa zamani wa timu hiyo.

“Yanga wanakaba sana tena wanapokonya mpira ndani ya sekunde chache, nafikiri kitu kikubwa ambacho alifanikiwa kwenye falsafa hii ni kuwa na kocha mzuri wa mazoezi, Yanga wachezaji wao wana pumzi ya kutosha na wako fiti hili limesaidia kuendana na mfumo ambao kocha anataka uchezwe, timu ambazo zimekutana na Yanga mpaka sasa zimeshindwa kuhimili hayo yote kwa pamoja.”

SOMA NA HII  HUU HAPA MUZIKI KAMILI WA YANGA DHIDI YA RIVERS UNITED KIMATAIFA