Home Habari za michezo HAWA HAPA ‘MAPRO’ WA SIMBA WALIOKIWASHA UHAKIKA MPAKA SASA….WENGINE MHH…

HAWA HAPA ‘MAPRO’ WA SIMBA WALIOKIWASHA UHAKIKA MPAKA SASA….WENGINE MHH…

Kikosi cha Simba Msimu huu 23/24

SIMBA ni kati ya timu za Ligi Kuu zenye wachezaji 12 wa kigeni kwenye vikosi vyao wakiwamo waliosajiliwa kwenye dirisha kubwa lililofungwa Agosti 31, mwaka huu na waliokuwapo tangu msimu uliopita lakini kiungo Mkongomani, Fabrice Ngoma na beki Mcameroon, Che Malone Fondoh wamewafunika wote.

Unajua wamefunikaje? Ngoma na Malone ndio wachezaji wa kigeni ndani ya Simba waliocheza mechi zote mbili za ligi kwa dakika 90 bila kufanyiwa mabadiliko.

Mastaa wa kigeni wa Simba waliosajiliwa sambamba na Ngoma kwenye dirisha lililopita ni Luis Miquissone, Willy Onana, kipa Mmorocco Ayoub Lakred, Aubin Kramo, huku waliokuwapo tangu msimu jana ni Clatous Chama, Said Ntibazonkiza, Sadio Kanoute, Henock Inonga, Jean Baleke na Moses Phiri.

Ngoma na Malone wameungana na wazawa watatu, mabeki Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ na Shomari Kapombe na kipa Ally Salim kuwa mastaa wa Wekundu wa Msimbazi waliocheza dakika 180 kila mmoja kwenye mechi mbili.

kupitia makala haya huu hapa uchambuzi wa mastaa wa kigeni wa Simba na dakika walizocheza kwenye ligi kwa msimu huu.

AYOUB LAKRED (Dk.0)

Ni usajili wa mwisho kwa upande wa Simba kutokana na kukamilisha idadi ya wachezaji wa kigeni na kuamua kupunguza mmoja kati ya 12 waliokuwa nao ili kuweza kumpisha kipa huyo ambaye amesajiliwa kwa lengo la kusaidiana na Aishi Manula ambaye yupo nje kwa muda akiuguza majeraha yake.

Lakred tangu amejiunga na Simba akitokea kutoka FAR Rabat ya Morocco hajacheza mechi hata moja sasa ni rasmi ataanza kutumika baada ya uongozi wa timu hiyo kufanya uamuzi wa kuachana na winga Peter Banda aliyetimkia Nyasa Big Bullet kwa mkataba wa miaka miwili.

FABRICE NGOMA (Dk.180)

Kiungo mkabaji mpya, raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Fabrice Ngoma, ameanza vizuri maisha yake ndani ya kikosi cha Simba.

Ngoma amekuwa mchezaji muhimu wa kutuliza timu inaposhambuliwa na kuanzisha mashambulizi pamoja na uwezo mkubwa wa kufunga.

Nyota huyo amecheza dakika zote 180 za Ligi Kuu Bara msimu huu akifunga bao moja kwa kichwa katika mchezo wa kwanza dhidi ya Mtibwa Sugar akimalizia pasi ya Jean Baleke.

Ujio wa Ngoma, unawafanya Sadio Kanoute na Mzamiru Yassin, mmoja kusubiri nje akimpa nafasi staa huyo ambaye amejiunga na Simba akitokea klabu ya Al Hilal ya Sudan.

CHE MALONE (Dk.180)

Ni panga pangua katika kikosi cha kwanza cha Simba tangu ametua ndani ya timu hiyo amekuwa akianzishwa. Ameziba vyema pengo la Joash Onyango aliyetimkia Singida Big Stars.

Malone amecheza na mabeki wote watatu wa kati waliopo ndani ya timu hiyo akianza na Henock Inonga mechi ya kirafiki Simba Day walipoilaza Power Dynamos 2-0 na kisha dhidi ya Singida Big Stars timu yake ikishinda kwa mikwaju ya penalti baada ya kucheza dakika zote 90 bila kuruhusu bao.

Pia amecheza mechi zote za ligi akianza na Mtibwa Sugar wakisaidiana na Kennedy Juma ambaye hakumaliza dakika zote 90 akimpisha Hussein Kazi, ambayo waliruhusu mabao mawili langoni mwao na alicheza tena dakika 90 zote dhidi ya Dodoma Jiji akianza na Kennedy.

LUIS MIQUISSONE (Dk.65)

Miquissone amesaini kurejea Simba baada ya miaka miwili tangu auzwe Al Ahly ya Misri na tayari amecheza mechi mbili za ligi lakini bado hajapata nafasi ya kufunga wala kutoa pasi ya mwisho ya bao.

Kiungo huyo mshambuliaji tayari amecheza dakika 65 hajafunga wala kutoa pasi iliyozaa bao. Alianza na Mtibwa Sugar akicheza dakika 27 kisha aliingia kuchukua nafasi ya Baleke aliyetolewa katika dakika ya 63 dhidi ya Dodoma Jiji, halafu aliingia katika dakika ya 38 akichukua nafasi ya Onana aliyecheza dakika 52.

WILLY ONANA (Dk.97)

Onana amejiunga na Simba akitokea Vipers ya Uganda ambako alimaliza ligi akiwa kinara wa upachikaji wa mabao. Tangu ametua Simba, kwenye Ligi Kuu ametupia bao moja na amecheza dakika 97 kati ya dk.180 ambazo Simba imecheza.

Alifunga bao hilo dhidi ya Mtibwa Sugar ugenini akichezeshwa kwa dakika 45 na kutolewa na nafasi yake ilichukuliwa na Saido. Katika mchezo dhidi ya Dodoma Jiji, Onana Sombasomba alicheza dakika 52 na hakufanikiwa kufunga wala kutoa asisti ya bao.

AUBIN KRAMO (Dk.0)

Kramo, raia wa Ivory Coast ana uwezo wa kucheza wingi zote mbili na kucheza namba 10. Ametua Simba akitokea Asec Mimosas kwa mkataba wa miaka miwili. Hadi sasa hajapata nafasi ya kucheza.

Kiungo mshambuliaji huyo alikuwa mchezaji wa pili wa kigeni kutambulishwa Simba SC baada ya uongozi wa klabu hiyo kukamilisha usajili wa Onana.

CLATOUS CHAMA (Dk.170)

Ni dakika 10 tu alizozidiwa na mastaa wapya waliosajiliwa katika dirisha kubwa la usajili lililofungwa mwishoni mwa mwezi uliopita. Chama ametumika kwa dakika 170 katika mechi mbili za Ligi Kuu Bara ambazo Simba imecheza hadi sasa.

Kwenye dakika hizo kiungo-mshambuliaji huyo alianza dhidi ya Mtibwa Sugar akifunga bao moja kwenye ushindi wa mabao 4-2 akicheza kwa dakika zote 90 na mechi dhidi ya Dodoma Jiji ambayo Simba iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 alicheza kwa dakika 80 na kumpisha Israel Mwenda.

SAIDO NTIBAZONKIZA (DK.118)

Kinara wa upachikaji wa mabao msimu uliopita alipofunga mabao (17), msimu huu amecheza dakika 118 na katika mechi hizo mbili alizocheza, aliingia kipindi cha pili katika dakika ya 45 akichukua nafasi ya Onana katika mechi dhidi ya Mtibwa Sugar na dhidi ya Dodoma Jiji FC alitoka katika dakika ya 73 na nafasi yake ilizibwa na Kibu Denis.

Saido kwenye michezo hiyo miwili hajafunga wala kutoa asisti hata moja akitumika zaidi ya dakika 100 tofauti na msimu uliopita.

SADIO KANOUTE (Dk.62)

Katika nafasi ya kiungo cha chini, kwa misimu miwili iliyopita alikuwa panga pangua katika kikosi cha kwanza cha Simba. Lakini msimu huu hali imekuwa tofauti kwani ameanza kwa kuchechemea akicheza kwa dakika chache zaidi kwenye mechi mbili.

Kanoute amecheza dakika 62 alianza mechi ya kwanza ya ligi dhidi ya Mtibwa Sugar waliyoshinda mabao 4-2 ambayo alitolewa katika dakika ya 45 nafasi yake ikichukuliwa na Mzamiru Yassin huku mchezo dhidi ya Dodoma Jiji timu yake ikiibuka na ushindi wa mabao 2-0 alicheza dakika 17.

HENOCK INONGA (Dk.0)

Ni beki kiongozi ndani ya kikosi cha Simba tangu amejiunga na timu hiyo lakini hajapata bahati ya kucheza mchezo hata mmoja wa Ligi msimu huu kutokana na kuwa nje ya uwanja akijiuguza majeraha aliyoyapata kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Singida Big Stars.

JEAN BALEKE (Dk.115)

Alijiunga na Simba katika dirisha dogo msimu uliopita ambao aliifungia timu yake mabao manane akimaliza msimu akiwa kwenye kiwango kikubwa na kuwa mchezaji pendwa wa mashabiki.

Msimu huu ameitumikia Simba kwa dakika 115 kwenye Ligi Kuu Bara na tayari ametupia mabao mawili akianza dhidi ya Mtibwa Sugar ugenini na alifunga bao moja kwenye dakika 63 alizocheza dhidi ya Dodoma Jiji nyumbani, mchezo ambao alitumika dakika 52.

MOSES PHIRI (Dk.50)

Ni mchezaji ambaye anaitumikia Simba katika msimu wake wa mwisho baada ya kusajiliwa kwa mkataba wa miaka miwili. Msimu wake wa kwanza 2022/23 aliifungia Simba mabao 10 kwenye Ligi Kuu akicheza mechi pungufu kutokana na kupata majeraha.

Msimu huu kweye dakika 50 alizocheza tayari ameshatupia bao moja kwenye mchezo dhidi ya Dodoma Jiji kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam na timu hiyo kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.

Phiri alianzia benchi kwenye mchezo wake wa kwanza dhidi ya Mtibwa Sugar, alicheza dakika 12 na mchezo wa nyumbani na Dodoma Jiji pia aliingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Baleke aliyetolewa katika dakika ya 52 na kumfanya mshambuliaji huyo acheze dakika 38 na kupachika bao.

SOMA NA HII  KISA SIMBA...TRY AGAIN AUWA NDEGE WAWILIKWA JIWE MOJA....APEWA SHAVU JIPYA FIFA...