Home Habari za michezo KUELEKEA MECHI NA AL AHLY….MASTAA SIMBA WANG’ATWA SIKIO MBINU ZA KUMALIZA KAZI...

KUELEKEA MECHI NA AL AHLY….MASTAA SIMBA WANG’ATWA SIKIO MBINU ZA KUMALIZA KAZI MAPEMA…

Habari za Simba

WAKATI macho na masikio ya mashabiki wa soka nchini yakitamani kuona mechi ya African Football League (AFL) ambapo Simba na Al Ahly zinakutana, mastaa wanataka kocha asuke kikosi vizuri ili timu yake ifanye vizuri.

Michuano hiyo itakayozinduliwa Oktoba 20, lakini mchezo unaosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka nchini ni kati ya Simba na Al Ahly ya Misri. Mara ya mwisho Simba ilipokutana na timu hiyo iliibuka na ushindi wa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.

Nyota wa zamani waliowahi kuitumikia timu hiyo na kucheza na Waarabu hao katika michezo iliyopita, wametoa mbinu zitakazowavusha Simba katika mechi hiyo inayosubiriwa kwa shauku.

Amri Said, ambaye aliwahi kuwa beki wa kati wa timu hiyo na sasa ni kocha, alisema Simba sio timu mbaya ndio maana inacheza kimataifa na kwa sasa kazi kubwa ni kwa viongozi pamoja na benchi la ufundi kuhakikisha wanapata ushindi kwenye mchezo huo

“Mbinu za kocha ndizo zitakazowafanya wachezaji kushinda kwani Waarabu wanashambulia sana na wana nguvu, hivyo kocha ana kazi ya ziada na mabeki na washambuliaji ili kuhakikisha anazuia na kushambulia kwa umakini wa hali ya juu,” alisema Said.

“Kikosi kina wachezaji wapya ila kocha atakuwa anajua nani aanze na wapi, hivyo kwa Waarabu dakika zote 90 ni kukimbizana na hawaachi nafasi ndio maana Simba inatakiwa kuwa vizuri kote na lazima mabosi wawaunge mkono.”

Boniface Pawasa ambaye kwa sasa ni kocha wa soka la ufukweni, alisema Simba ina changamoto ya wachezaji wapya, lakini wana uwezo na akicheza Che Malone na Enock Inonga kama mabeki wa kati hakuna kinachoharibika pia Saido Ntibazonkiza na Moses Phiri wakiwa kama washambuliaji na nyuma yao akisimama Clatous Chama.

Alisema ukiachana na ufundi wachezaji wanatakiwa kujiamini kwani uwanja watakaocheza mchezo wa ugenini waliutumia walipokipiga na Zamalek miaka mingi iliyopita na Simba ikapata ushindi sio kwa sababu ilikuwa bora zaidi yao ila ilijua nini kilichoipeleka Misri.

“Uzalendo na uchungu walionao wachezaji wa Simba ndio utakaokwenda kuunda historia nyingine, hivyo nina hakika wachezaji wakipata utulivu na kocha akipanga mfumo wake vizuri yale ya Zamalek 2003,” yanajirudia.

“Hii mechi ni ya faida kwa wachezaji itaangaliwa na dunia nzima, hivyo ni nafasi yao kujiuza kimataifa. Lazima waonyeshe morali ya kupambana na kuhitaji matokeo mazuri na tusisahau Simba ina bahati ya kufanya vizuri mechi za kama hizi,” alisema Pawasa.

SOMA NA HII  SIMBA INAMTU HUYU MMOJA TU