Home Habari za michezo KUFA KUFAANA KUTOKA KMC MPAKA SIMBA

KUFA KUFAANA KUTOKA KMC MPAKA SIMBA

Habari za Simba

Katika maisha ya kutafuta kuna muda ili upate ulaji ni lazima aliyekuwa kwenye nafasi fulani atoke kisha ndio wewe upate na hiyo ndivyo jinsi ilivyo.

Jambo hilo limeenda kutokea kwa kipa Yona Amos wa Tanzania Prisons ambaye amepta zali la kugeuka namba moja baada ya kuondoka Hussein Abel aliyetimkia KMC kabla ya kuibukia Simba kwa sasa.

Mwanaspoti limefanya mahojiano maalumu na kipa huyo ambaye amefunguka safari yake kisoka hadi kufikia kwa Maafande wa Tanzania Prisons na kurithi nafasi ya Abel na kukata kiu ya timu hiyo. Hata hivyo kuna watu walihisi atafeli kwenye eneo hilo.

AANZIA MAWENZI, ATIMKIA MALAWI

Watu wengi wamemuona Yona akiwa kwenye kikosi cha Tanzania Prisons kuanzia msimu uliopita lakini kumbe kipa huyo amekaa misimu miwili kwenye Ligi Daraja la Kwanza sasa Championship kwa msimu mmoja na nusu (2019/2020 na 2020/2021 nusu msimu).

Kipa huyo anasema baada ya kukaa Mawenzi aliamua kwenda kujaribu maisha ya kulipwa nje ya nchi na akatimkia Malawi na kupata timu ya Karonga United.

“Haikuwa kitu rahisi kupata nafasi kule, nilienda kufanya majaribio na baada ya kuvutiwa na huduma yangu ndio wakanipa mkataba, tulikuwa tupo wengi,” anasema Yona.

Yona alidumu katika klabu hiyo kwa msimu mmoja na nusu baada ya hapo alipata ofa ya kurudi tena Tanzania.

PRISONS YAMUONA

Akiwa katika harakati zake za maisha Malawi, viongozi wa Tanzania Prisons walipata habari zake na kuanza kumfuatilia na walikubali kiwango chake fasta wakamnasa.

“Mkataba wangu ukiwa kule uliisha na kuna baadhi ya sehemu ya malipo tulishindwana, vilevile niliona bora nibadili mazingira kwanza;

“Malipo ya Prisons pia yalikuwa mazuri kuliko kule, ila nisiwe muongo kuna utofauti mkubwa wa soka la nyumbani na kule Malawi ukiachana na pesa.”

Yona anasema pesa ilikuwa jambo la kwanza lakini pili ni namna ambavyo soka la hapa nyumbani linavyokua kwa kasi ameona ni sehemu ya kusogea mbele zaidi.

“Soka letu lina wadhamini wengi na ni ligi bora kuliko ile ya Malawi kuna kitu kikubwa zaidi hapa nyumbani kwa mtu anayeweza kwenda mbele.”

KIPA LA SIMBA

Maisha ndivyo yalivyo akitoka mmoja kwenye nafasi basi mwingine anaingia na hilo ndio lililotokea kwa Yona baada ya kujiunga Prisons.

Yona akiwa Prisons, kipa namba moja Hussein Abel alipata dili la kujiunga na KMC baada ya kuvutiwa na huduma yake.

Akizungumzia kupata nafasi na maisha yake pamoja na Abel, Yona anasema walikuwa vizuri wakiishi bila tabu yoyote.

“Alikuwa anafanya vizuri (Abel) kwahiyo baada ya kupata nafasi nilikuwa najua kutakuwa na presha kwangu, Ila nilijiamini nikiwa golini,” anasema Yona.

Yona anasema presha ya kubaki Ligi Kuu ilikuwa kubwa lakini kama timu walipambana kuhakikisha wanabaki na walilitimiza hilo.

“Kiukweli timu kiujumla tulikuwa na kitu kimoja na ndio maana tulipambana vya kutosha na tulifanikiwa, hakukuwa na motisha yoyote bali wachezaji tulijitoa.”

TINOCCO, MBISA NI SAFI TU

Katika kikosi cha Tanzania Prisons kuna makipa watatu, Yona, Benedict Tinocco na Mussa Mbisa ambao wana uzoefu wa kutosha katika ligi.

Msimu uliopita Yona alipata nafasi ya kucheza kwa sababu Mbisa alikuwa amevunjika mkono na alihitajika kukaa nje ya uwanja kwa miezi sita.

Akizungumzia kaka zake hao, Yona anasema ni changamoto kubwa kwake lakini kwa pamoja wanashirikiana kuhakikisha timu yao inafanya vizuri.

“Changamoto ipo na kikubwa ni kupambana tu ili niendelee kuaminiwa, kaka zangu wapo vizuri na wananisapoti kwa namna moja ama nyingnine,” alisema

AITAKA TAIFA STARS

Kama ilivyo ndoto za wachezaji wengi kuhitaji kupeperusha bendera ya timu ya taifa ndivyo ilivyo kwa kipa huyu wa Tanzania Prisons baada ya kuweka wazi ndoto yake ya kuicheza timu ya taifa.

Yona anasema kama mchezaji siku zote lazima ajiwekee malengo na yeye yupo Prisons akiwa na hesabu ya kucheza timu ya taifa kisha aweze kutoka nje ya nchi.

“Kila mchezaji lazima awe na malengo yake, kwangu natamani sana nicheze timu ya taifa kwa sababu itakuwa sehemu yangu ya kunifanya nitoke nje ya nchi na kuweza kuonekana.

Yona anongeza akisema; “Kitu kikubwa ni kupambana hadi hatua ya mwisho naamini kabisa kila kitu kitakuwa sawa na mambo yatakwenda vizuri,” alisema.

SOMA NA HII  ROBERTINHO MTEGONI SIMBA..... ISHU IKO HIVI USAJILI WAGUSIWA