Home Habari za michezo MASHABIKI WA SIMBA WANAVYOTESEKA NA SOKA LA ROBERTINHO

MASHABIKI WA SIMBA WANAVYOTESEKA NA SOKA LA ROBERTINHO

Habari za Simba SC

Simba inakwenda vizuri chini ya kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’. Majuzi imepata ushindi wa tatu mfululizo katika Ligi Kuu Bara. Ipo nafasi ya tatu nyuma ya Yanga na Azam kwenye msimamo.

Ushindi huo ulikuwa mwendelezo wa Robertinho kuongeza idadi ya mechi ambazo hajapoteza Ligi Kuu Bara. Tangu apewe kazi Januari, mwaka huu hajawahi kupoteza mchezo wa ligi. Ni rekodi nzuri sana kwake.

Anazidi kujipambanua kuwa ni kocha mzuri kwenye mbinu. Hapotezi kirahisi mbele ya wapinzani wake. Haijalishi anakutana na nani.

Katika wakati wake ndani ya Simba amekutana na timu ngumu kama Yanga, Azam na Singida Fountain Gate lakini zote hakupoteza. Inafurahisha.

Kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita aliipeleka Simba robo fainali. Akapoteza kwa penalti mbele ya Wydad Casablanca ya Morocco ambayo ilifika fainali.

Ukiachana na kipigo cha mchezo wa fainali kutoka kwa Al Ahly, hao Wydad wenyewe wanakiri Simba ilikuwa mpinzani mgumu zaidi kwao. Ndio sababu baada ya kupenya kwa shida wakamtimua kocha.

Kwanini Wydad wanakiri hivyo? Ni kwa sababu ya mbinu za Robertinho. Simba licha ya kuwa na kikosi dhaifu msimu uliopita walicheza kwa mbinu nzuri. Walitulia vizuri kwenye mipango ya mechi zao.

Hii ndio tabia ya makocha wenye mbinu nzuri kama Robertinho. Haijalishi ana timu ya aina gani bado atakushangaza.

Pamoja na yote bado mashabiki wa Simba hawafurahishwi na timu. Wanasema inashinda lakini haichezi vizuri. Kwa kifupi hawafurahishwi na kiwango cha timu kwa sasa.

Wanaamini ujio wa kina Luis Miquissone, Willy Onana, Che Malone, Fabrice Ngoma na wengineo unapaswa kuifanya Simba wawe hatari zaidi. Wacheze soka la kuvutia zaidi. Ndio hao wenye Simba yao sasa.

Wanaifananisha Simba ya sasa na ile ya Patrick Aussems. Wanaifananisha na ile ya Sven Vanderbroek. Wanataka icheze pira biriani na kushinda mechi.

Unafikiri wananishangaza? Hapana. Hili imekuwa kama imani kwa wana Simba wote tangu enzi na enzi. Wamekuwa wakitaka mpira mzuri na matokeo.

Ndio sababu makocha kama Joseph Omog, Pierre Lechantre na wengineo wamewahi kuachwa kwa sababu hiyo. Amewahi kufukuzwa Patrick Phiri kwa sababu hiyo. Walisema Simba yao inakata pumzi na kushindwa kucheza vyema kwa dakika zote 90.

Mashabiki wa Simba wanaamini kuwa mpira wa kucheza na kushinda bila kujali kiwango cha timu yao ni wa Yanga. Zinapigwa pasi ndefu, mabao yanafungwa. Simba hawataki hivyo. Bahati mbaya zaidi kwa sasa Yanga inacheza soka la kuvutia zaidi yao. Inaupiga mwingi na kushinda mechi zake. Hii inawavuruga sana Simba.

Wanaona kama soka lao limehamia Yanga na wao wanacheza kama mtani wao huyo.

Ila, mashabiki wa Simba wanasahau jambo kubwa la msingi. Lengo la kucheza mechi ni kupata ushindi. Viwango vitakuja tu.

Ingekuwaje kama Simba ingekuwa haichezi vizuri na inafungwa? Wangepoteana kabisa. Wangemkalia kooni Robertinho. Wasingeelewa kitu.

Lakini ndio mpira wa kisasa. Kuna nyakati unahitaji kushinda zaidi kuliko ufundi. Muhimu alama tatu zinapatikana.

Pia siku hizi timu nyingi zimeimarika kuliko zamani. Leo timu kama Ihefu, Tabora United, Coastal Union na nyingine zinafundishwa na makocha wakubwa na zina wachezaji wengi wa kigeni.

Makocha hawa nao wanajua namna ya kukabiliana na timu kubwa. Huwezi kuwafunga kirahisi tu.

Mfano Mwinyi Zahera wa Coastal Union ni muumini mkubwa wa soka la kukaba. Ndio sababu walipokuwa pungufu waliweza kuzuia kwa muda mwingi Simba isifunge bao na wakafanikiwa.

Makocha kama Robertinho wapo wengi tu katika soka la kisasa. Wanaamini zaidi kwenye mbinu kuliko mbwembwe za uwanjani. Hata ukicheza vizuri zaidi yake, yeye atapata matokeo mazuri.

Ndio sababu Robertinho mwenyewe anasema timu yake inacheza vizuri. Imaimarika zaidi. Kwanini? Kwa sababu kimbinu wanampa kile anachotaka.

Hata hivyo, Robertinho anatakiwa pia kuwaelewa mashabiki wa Simba. Utamaduni waliouzoea unawaumiza pia. Wamezoea burudani. Na ndio sababu wanampenda sana Clatous Chama. Anawapa furaha ndani ya mioyo yao.

SOMA NA HII  PAMOJA NA SIMBA KUPITWA NA YANGA KWA POINT 10...PABLO AVUNJA UKIMYA ...ATOA KAULI HII...